Jumatano, 11 Februari 2026

KIKAO KAZI CHA MAPITIO, MAREKEBISHO YA KANUNI ZA MAHAKAMA ZA WATOTO CHAFANYIKA

Na ASHA JUMA-Mahakama, Morogoro

Mahakama imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha utoaji wa haki kwa watoto kwa kuandaa kikao kazi maalum,  kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), ili kupitia kanuni za Mahakama za Watoto  za mwaka 2016 kwa ajili ya kuziboresha.

Uboreshaji huo unalenga kuzifanya kanuni hizo ziendane na mabadiliko ya sheria yaliyotokea, kuongeza ufanisi, tija na weledi katika usikilizaji na uamuzi wa mashauri ya watoto.

Kikao kazi hicho cha siku tano kilianza tarehe 9 Februari, 2026 kikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha,  Mhe. Nyigulila Mwaseba, kikihusisha mijadala ya kina, mapendekezo ya kitaalamu pamoja na kubadilishana uzoefu juu ya utekelezaji wa sheria na  kanuni hizo.

Aidha, kikao hicho  kinafanyika katika ukumbi wa mkutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki  (IJC) Morogoro na  kimewakutanisha wataalamu mbalimbali wa haki za mtoto, wakiwemo Naibu Wasajili, Mahakimu,Wizara za Kisekta, Taasisi za Kiserikali na Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa wa Jeshi la Polisi, pamoja na Mawakili na Wanasheria kutoka Taasisi mbalimbali za kisheria.

Mwenyekiti wa kikao hicho,  alieleza kuwa Kanuni za Mahakama ya Watoto hazijawahi kufanyiwa mapitio tangu kuanza kutumika mwaka 2016. Alibainisha kuwa hali hii imezua changamoto katika utekelezaji wake kutokana na mabadiliko ya kisheria yaliyotokea baada ya kipindi hicho. Aliweka msisitizo mkubwa katika umuhimu wa kuzingatia ulinganifu wa kanuni hizi na sheria mama pamoja na misingi ya maslahi bora ya mtoto.

“Nadhani sheria hizi hazijawahi kufanyiwa marekebisho tangu mwaka 2016, nimekua nikiona changamoto mbalimbali haswa kutokana na mabadiliko ya teknolojia na sheria mbalimbali,” alisema Mhe. Mwaseba.

Kwa ujumla, kikao kazi hiki kinatarajiwa kuwa chachu ya maboresho makubwa katika mfumo wa utoaji haki kwa watoto nchini, kwa kuhakikisha kuwa sheria zinazotumika zinaendana na mahitaji ya sasa ya kijamii, kisheria na kiteknolojia, huku maslahi ya mtoto yakiendelea kuwa kipaumbele cha juu.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha,  Mhe. Nyigulila Mwaseba akifungua kikao hicho.

Picha ya kikao kazi wakiwa wanajadili maboresho ya kanuni hizo.

Picha ya pamoja ya kikao kazi hicho.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Mbeya.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni