Na NOEL SYLIVESTER - Mahakama Kuu, Songea
Uongozi wa Mahakama Kanda ya Songea, hivi karibuni ulikutana na Mahakimu wote kujadili mpango mkakati wa
kimahakama na kiutawala kwa mwaka 2026 ili kuboresha utendaji kazi, uadilifu na
ushilikiano.
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Taasisi ya Kupamba na Kuzuia
Rushwa (PCCB) wilayani Songea mkoani Ruvuma, kiliongozwa na Jaji Mfawidhi, Mhe.
James Karayemaha na kuhudhuriwa na Viongozi wengine wa Mahakama kwenye Kanda
hiyo.
Viongozi hao ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Mhe. Emmanuel Kawishe,
Naibu Msajili, Mhe. Elizabeth Nyembele pamoja na Mtendaji wa Mahakama, Bw. Allan
Mwela.
katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho, Jaji Mfawidhi alielezxa
kuwa wamekutana kujadili mpango huo kuhusu mashauri na masuala ya kiutawala kwa
mwaka 2026, ambao unalenga kuimarisha utoaji wa haki kwa wakati, kwa uwazi, kwa
usawa na kwa kuzingatia misingi ya sheria.
‘Tunatarajia mpango huu utatusaidia kupunguza mlundikano wa mashauri,
kuboresha usimamizi wa mashauri, kuimarisha nidhamu ya kazi na kuongeza ufanisi
katika utawala wa Mahakama zetu. Tukifanya mipango yetu vizuri hatutakuwa na msongo
wa mawazo, tutajijengea uaminifu, tutaboresha namna ya kutoa uamuzi na tutapata
matunda tunayoyatamani,’ alisema.
Mhe. Karayemaha aliongeza kuwa wakati wa kutekeleza jukumu la utoaji
haki lazima kukumbuka viapo vyao vya kutoa uamuzi wa haki kwa kuzingatia
matakwa ya Ibara ya 4, 107A na 107B ya Katiba.
‘Msingi wake ni kuimarisha amani na udugu wa wananchi. Kwa hiyo, sisi
waamuzi inatupasa kuzingatia sheria na maadili ya utumishi wetu. Tukifanya kazi
yetu ipasavyo bila woga tutadumisha utawala wa sheria, ambalo ni jukumu letu
pia. Hii sio hiari, tumeelekezwa na Ibara ya 26 ya Katiba kuwaadhibu na
kuwawajibisha ipasavyo wanaokiuka masharti ya Katiba na sheria zetu,’ alisema.
Aliwakumbusha Mahakimu hao kuwa wanalo pia jukumu la kulinda uhuru wa
Mahakama unaolindwa na kuhifadhiwa katika Ibara ya 30(2)(d) ya Katiba
ikichagizwa na Kifungu cha 114 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Jaji Mfawidhi alibainisha kuwa pale inapotokea uhuru wa Mahakama
umechokonolewa au kupakwa matope kwa kauli au vitendo, wanapaswa kumama imara
kuwakumbusha hao kuhusu heshima na uhuru wa Mahakama.
‘Woga ni sumu ya mafanikio na mabadiliko na inakinzana na malengo ya
Mwenyezi Mungu, ni matarajio yangu kuwa katika kikao hiki tutajadili kwa uwazi
changamoto zilizopo katika mashauri na utawala, tutoe mapendekezo ya vitendo na
kujenga mikakati itakayotekelezeka kwa ufanisi katika mwaka 2026 na kuendelea,’
Mhe. Karayemaha alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni