Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali amewaagiza Viongozi wa ngazi mbalimbali za Mahakama katika Kanda hiyo kuhakikisha wanafanya kaguzi zenye tija katika Mahakama zilizo chini yao ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya utendaji kazi katika vituo hivyo lengo likiwa ni kuongeza ufanisi wa kazi za Mahakama.
Mhe. Mahimbali aliyasema hayo katika Kikao cha Menejimenti ya Mahakama Kanda ya Arusha kilichoketi hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha ambapo aliwaambia wajumbe wa kikao hicho kuwa ni lazima juhudi zao zijikite katika kuibua mikakati bunifu inayolenga kufanikisha malengo ya Mahakama ya kutoa haki kwa wananchi mapema ipasavyo na kwa ubora unaotakiwa.
“Tunapokagua Mahakama zetu, lazima tubainishe mafanikio, changamoto, njia au mbinu za kuondokana na changamoto hizo na kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha utendaji kazi katika mahakama zetu. Ni kwa kufanya kazi namna hiyo ndio tutafikia malengo ya kuondokana na mashauri ya mlundikano yasiyo na sababu za msingi,” alisisitiza Jaji Mahimbali.
Mhe. Mahimbali aliongeza kuwa, kwa kufanya hivyo kutasaidia na kusukuma usikilizaji wa mashauri unaojikita katika kumaliza idadi kubwa ya mashauri kuliko mashauri yanayosajiliwa.
Akiwasilisha Taarifa ya hali ya mashauri katika Kanda ya Arusha, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Sophia Massati aliwaeleza wajumbe kuwa, kasi ya usikilizaji wa mashauri ni nzuri na kwamba wameweza kumaliza kiasi kikubwa cha mashauri ya mlundikano na mikakati madhubuti imewekwa kuhakikisha kasi ya umalizaji mashauri inaongezeka na hivyo kudhibiti kiasi cha mashauri mlundikano mapya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na Mhe. Massati, hadi kufikia tarehe 26 Februari, 2026, Mahakama Kuu Arusha ilikuwa imebakiwa na mashauri mlundikano sita tu, na Kanda nzima ya Arusha zikiwemo Mahakama za chini kulikuwa na mashauri mlundikano 15 pekee.
Aliongeza kuwa, idadi hiyo ya mashauri mlundikano inatarajiwa kupungua kutokana na mikakati iliyowekwa na Kanda ya Arusha kumaliza mashauri kwa wakati.
Naye Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Bi. Grace Kapama aliwasilisha taarifa ya utendaji ambayo kwa kiasi kikubwa ilionesha mafanikio makubwa katika kuweka mazingira wezeshi kuwezesha usikilizaji mashauri kufanyika katika mazingira mazuri na rafiki zaidi.
Bi. Kapama alibainisha baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na ukarabati wa Mahakama za Mwanzo Likamba na Nkoanrua zilizopo wilayani Arumeru zilizokuwa zimefungwa kwa kipindi kirefu na hatimaye kufanikiwa kuzifufua na mpaka sasa zinafanya kazi.
Aidha, katika kikao hicho Wajumbe wamesisitizwa kuwa wabunifu zaidi katika usimamizi wa vituo vyao vya kazi na kuhakikisha huduma za Mahakama kwa wananchi zinakuwa bora zaidi na kutolewa mapema ipasavyo.
Kikao
hicho cha Menejimenti Kanda ya Arusha kilihudhuriwa na wajumbe mbalimbali
kutoka Mahakama Kanda ya Arusha ikiwemo wajumbe wa Mahakama Kuu, Mahakama ya
Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya Arumeru, Longido, Karatu, Monduli na
Ngorongoro.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali akiongoza Kikao cha Menejimenti Kanda ya Arusha kilichofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni