Alhamisi, 5 Machi 2026

MWANANCHI MKOA WA GEITA WAPATIWA ELIMU KUHUSU UTEKELEZAJI WA AMRI ZA MAHAKAMA

Wananchi wa Mkoa wa Geita wamenufaika na mpango wa utoaji elimu kwa Umma ulioratibiwa na Mahakama Kuu Masjala ya Geita.

Utoaji huo wa elimu ulifanyika tarehe 03 Machi, 2026 katika Ukumbi wa Elimu kwa Umma, Kituo Jumuishi (IJC) Geita.

Mada iliyowasilishwa ilikuwa Utekelezaji wa Amri za Mahakama, ikiwa na lengo la kuwajengea wananchi uelewa kuhusu taratibu za kisheria baada ya hukumu kutolewa.

Elimu hiyo ilitolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Geita, Mhe. Mujuni Muchunguzi, ambaye alieleza kwa kina hatua zinazofuatwa katika utekelezaji wa amri za Mahakama mara baada ya hukumu kutolewa.

Katika mafunzo hayo, Mhe. Muchunguzi alifafanua kuwa utekelezaji wa amri za Mahakama hufanyika kwa njia mbalimbali, ikiwemo kukamata na kuuza mali za mdaiwa, kuamrisha jambo fulani litendeke ili kumpatia mdai haki yake, au utekelezaji wa kifungo cha madai pale inapobidi. Alieleza kuwa taratibu zote hufuata misingi ya kisheria ili kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote zinazohusika.

Aidha, wananchi walipata fursa ya kuuliza maswali kuhusu migogoro ya ardhi, zuio litolewalo na Mahakama na masuala ya dhamana katika mikopo ya benki.

Akijibu hoja hizo, Mhe. Muchunguzi alisisitiza kuwa endapo mali itauzwa kwa thamani kubwa kuliko deni, kiasi kinachozidi hurudishwa kwa mdaiwa.

Aliongeza kuwa migogoro ya ardhi inapaswa kuanzia Baraza la Ardhi la Kata kwa usuluhishi na baadaye kama hawajaelewana kupeleka mgogoro wa ardhi kwenye Baraza la Ardhi Nyumba na Makazi Wilaya kwa mujibu wa sheria.

Alisema kwamba ni kosa la kukaidi amri ya Mahakama, ambapo anayekiuka zuio halali anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria.

Wananchi walieleza kufurahishwa na elimu hiyo, wakisema imewasaidia kuelewa haki na wajibu wao katika masuala ya kisheria. Mahakama imeueleza Umma huo kuwa itaendelea kutoa elimu kama hiyo mara kwa mara ili kuongeza uelewa wa sheria na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa jamii.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina, akiwahutubia na kuwasalimia wananchi, huku akiwaalika wale wote wenye changamoto au wanaohitaji msaada wa kisheria kujitokeza ili wasikilizwe na kupatiwa msaada stahiki.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilayya Geita, Mhe. Mujuni Muchunguzi akiendelea kutoa elimu kwa wananchi Mkoa wa Geita.

Wananchi Mkoa wa Geita wakiendelea kupata mafunzo katika ukumbi wa mafunzo wa Mahakama Kuu Geita.

Hakimu Mfawidhi, Mhe. Mujuni Muchunguzi akiwa katika picha ya pamoja na Wananchi baada ya mafunzo.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni