Jumatano, 4 Machi 2026

JAJI KIONGOZI ASISITIZA UADILIFU, UELEDI NA UWAJIBIKAJI KWA MAHAKIMU

        Awakumbusha maneno ya Hayati Benjamin William Mkapa kuhusu bidii, maarifa na kufanya kazi kwa matokeo

Na. Halima Mnete – Mahakama, Dodoma

Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, amewataka Mahakimu kote nchini kuzingatia misingi ya uadilifu, ueledi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa bila kuzingatia nguzo hizo, haki haiwezi kutendeka kwa ufanisi.

Akizungumza mapema leo tarehe 4 Machi, 2026 katika hafla ya kuapishwa kwa Mahakimu Wakazi wawili (2) iliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma, ambapo kiapo hicho kilisimamiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju, Mhe. Dkt. Siyani awakumbusha maneno ya Hayati Benjamin William Mkapa kuhusu bidii, maarifa na kufanya kazi kwa matokeo.

Akizungumza mara baada ya kuapishwa kwa mahakimu hao, Mhe. Dkt. Siyani alisema kazi ya uhakimu si ya mazoea bali ni dhamana kubwa kwa umma, inayohitaji mtu mwenye maadili thabiti na uwezo wa kitaaluma.

“Sasa mambo haya yanabeba msingi kwa kazi mnayoenda kuifanya. Mtumishi yeyote wa Mahakama au wa Umma, hususani Hakimu au Jaji, anapaswa kuyachukua na kuyazingatia mambo haya matatu kama sehemu ya maisha yake. Kazi ya uhakimu bila uadilifu hautofika popote, bila ueledi na kuwajibika hamtafika popote,” alisema Mhe. Dkt. Siyani.

Aliongeza kuwa, Mahakimu hao wameomba wenyewe nafasi hiyo na kwa mapenzi ya Mungu wamefanikiwa kuipata, hivyo wanapaswa kuitumikia kwa moyo wa kujituma na kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao.

Katika kuimarisha msisitizo wake, Jaji Kiongozi alinukuu maneno ya Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa, aliyewahi kusema kuwa njia ya maendeleo imejaa jasho na vumbi, na kusisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii, maarifa, ubunifu na kujituma.

Aidha, Jaji Kiongozi alikumbusha kauli ya hayati Mkapa kwamba kilicho muhimu si muda anaotumia mfanyakazi kazini, bali ni kiasi cha kazi anachoweza kuifanya katika muda aliopewa. Alisema kauli hiyo ina umuhimu mkubwa hata kwa Mahakama ya Tanzania, hasa katika kuhakikisha mashauri yanamalizika kwa wakati na kwa ubora unaotarajiwa.

“Katika kuwajibika, si tu kufanya kazi kwa bidii, lazima mfanye kazi kwa ufanisi. Matokeo yanapatikana kwa kufanya kazi kwa weledi na kwa akili. Unaweza kufanya kazi usiku na mchana lakini usimalize kesi kama haufanyi kazi kwa mpangilio na kwa ufanisi,” alisisitiza.

Mhe.Dkt. Siyani aliwakaribisha rasmi Mahakimu hao katika utumishi wa Mahakama ya Tanzania na kuwahakikishia kuwa, licha ya kutopata fursa ya kukutana nao wakati wa mafunzo yao, watakutana katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku wakiwa sehemu ya taasisi inayosimamia haki na ustawi wa jamii.

Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, akitoa nasaha kwa Mahakimu Wakazi Wapya walioapishwa leo tarehe 04 Machi, 2026 jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. George Masaju (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mahakimu Wapya walioapishwa leo tarehe 04 Machi, 2026. Wengine ni Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (wa kwanza kushoto) na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Cho cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (wa pili kushoto), Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Cho cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) (wa kwanza kushoto), Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Mhe. Dkt Juliana Massabo (katikati), Jaji Mfawidhi wa Kituo cha Usuluhishi cha Mahakama ya Tanzania Mhe. Zahra Maruma (wa pili kulia), Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Mhe Abdi Kagomba (wa kwanza kulia). wakifuatilia tukio la uapisho wa Mahakimu Wakazi (hawapo pichani).



Sehemu ya Mahakimu Wakazi wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. George Masaju (hayupo pichani)

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni