Jumatano, 4 Machi 2026

WATUMISHI KUPATA HUDUMA BORA ZA KIBENKI NA MIKOPO YA RIBA NAFUU

Na. MUKSINI NAKUVAMBA - Mahakama, Mbeya.

Afisa wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Bi. Agatha Masao kutoka Makao Makuu ya benki hiyo amefanya kikao na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya na kusema kuwa, benki hiyo imejipanga kuwahudumia watumishi wa Mahakama kwa kutoa huduma bora za kifedha pamoja na mikopo yenye riba nafuu.

Kikao hicho kilifanyika tarehe 02 Machi 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mahakama Kuu Mbeya, chini ya Mwenyekiti ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Joachim Tiganga.

Bi. Agatha Masao aligusia kuhusu makubaliano ya kibiashara na uwekezaji yaliyoingiwa kati ya Mahakama ya Tanzania na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), yenye lengo la kuimarisha ushirikiano na kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa watumishi wa Mahakama.

Aidha, alifafanua kuwa makubaliano hayo yanawawezesha watumishi kupata mikopo yenye riba nafuu pamoja na unafuu wa huduma za kifedha, hususani kwa watumishi watakaopitisha mishahara yao kupitia benki hiyo. Pia alibainisha uwepo wa huduma ya mikopo ya haraka kupitia simu za mkononi (salary advance) inayofikia hadi asilimia 50 ya mshahara.

Vilevile, Bi. Agatha alitoa elimu kuhusu bidhaa nyingine zinazotolewa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), ikiwemo uwezeshaji wa watumishi wa Mahakama kununua hatifungani za Serikali, ambapo mtumishi hulipia asilimia 25 pekee, huku asilimia iliyobaki ikifadhiliwa na benki hiyo.“Matatizo yako mwachie NBC, wewe songa na maisha.” Alisisitiza Bi. Agatha

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Joachim Tiganga, alitoa shukrani zake za dhati kwa ujio wa maafisa hao kutoka NBC kwa elimu waliyoitoa kwa watumishi.

“Ninawashukuru sana kwa ujio wenu. Bidhaa zenu ni nzuri, na nina imani mna lengo jema. Ni matumaini yangu kuwa watumishi wetu watanufaika zaidi na huduma mnazotoa,” alisema Mhe. Tiganga.

Aidha, kikao hicho kilihusisha watumishi kutoka Mahakama Kuu Mbeya, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mahakama ya Wilaya Mbeya, pamoja na Mahakama za Mwanzo zilizopo Mbeya Mjini.

Kwa upande mwingine, kikao hicho pia kilitumika kuwakaribisha watumishi wa ajira mpya waliopangiwa vituo mbalimbali mkoani Mbeya katika kada tofauti, zikiwemo maafisa ugavi, wapishi, wasaidizi wa ofisi, madereva na walinzi.

Katika hafla hiyo ya ukaribisho, watumishi walikata keki kwa pamoja kuonesha umoja na mshikamano miongoni mwa watumishi wa kada zote. Pia, pongezi zilitolewa kwa watumishi waliokuwa na siku za kuzaliwa katika miezi ya Januari na Februari, kama ilivyo desturi ya Kanda hiyo kila inapofika mwisho wa mwezi.

Ugeni huo wa maafisa wa NBC uliongozwa na Afisa Utumishi wa Mahakama ya Tanzania kutoka Makao Makuu, Bi. Viviene Kishembo, aliyeambatana na Meneja wa NBC Tawi la Mbeya, Bw. Asumisye Edward; Meneja wa NBC Tawi la Mwanjela, Bw. Khalid Omary; Afisa Mikopo kutoka NBC Tawi la Mbeya, Bw. Alex Elias; pamoja na maafisa wengine.

Sehemu ya Maofisa kutoka Benki ya Taifa ya Biashara NBC waliokwenda kutoa elimu ya masuala ya kifedha kwa watumishi wa Mahakama Mbeya.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe, Joachim Tiganga (watatu kulia) akitoa neno la shukurani kwa Maofisa wa NBC katika kikao hicho, wengine ni Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Judith Lyimo (wa kwanza kulia), Jaji wa Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Mussa Pomo (wa pili kulia), wanne kulia ni Mtendaji wa Mahakama kuu kanda ya Mbeya Bi. Mervis Miti.

Afisa Utumishi Mahakama ya Tanzania Makao Makuu Bi. Viviene Kishembo (aliyesimama) akitambulisha ugani aliokuja nao.

Sehemu ya watumishi katika kikao hicho.

Sehemu ya watumishi walioshiriki katika kikao hicho.


Sehemu ya watumishi walioshiriki katika kikao hicho.

Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Mussa Pomo akilishwa keki kwa niaba ya Majaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga akimlisha keki mmoja wa watumishi waliozaliwa kati ya mwezi Januari na Februari ambaye ni Mwandishi mwendesha ofisi Mahakama ya Wilaya Mbeya.

Watumishi wa Mahakama waliozaliwa mwezi Januari na Februari wakikata keki ya pamoja

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni