Jumatano, 4 Machi 2026

JAJI MFAWIDHI MBEYA ASHIRIKI MAZISHI YA MTUMISHI WA MAHAKAMA

Na. MUKSINI NAKUVAMBA - Mahakama, Mbeya

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Mhe. Joachim Tiganga ameshiriki mazishi ya aliyekuwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Mikese, Kanda ya Morogoro, Mhe. Asajile Joshua Mhando. Mazishi hayo yamefanyika tarehe 20 Februari 2026 katika Kijiji cha Vwawa, Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe, ambako ndiko nyumbani kwa familia ya marehemu Asajile Mhando.

Awali, mwili wa marehemu uliagwa na viongozi pamoja na watumishi mbalimbali wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya katika viunga vya Mahakama hiyo, wakiwemo Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania waliokuwa wakiendelea na vikao vya mashauri ya rufani katika Kanda hiyo na baadaye mwili wa marehemu ulisafirishwa kwenda Kijiji cha Vwawa, Mkoa wa Songwe, kwa ajili ya kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele.

Akizungumza wakati wa mazishi hayo, Mhe. Tiganga, alitoa salamu za pole kwa mjane, familia na ndugu wa marehemu, pamoja na kutoa shukrani kwa uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro na Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha kumpumzisha aliyekuwa mtumishi hodari wa Mahakama ya Tanzania.

“Ninafahamu hiki ni kipindi kigumu kwa mjane, familia na hata watumishi wenzake, lakini hatuna budi kukubali kwani ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu; aliyemtoa ndiye aliyemtwaa. Wajibu wetu sisi ni kumuombea ili Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani,” alisema Mhe. Tiganga.

Aidha, Mhe. Tiganga aliwasisitiza wanafamilia kufuatilia stahiki za marehemu kutoka kwa mwajiri mara baada ya kumaliza msiba, ikiwemo kukaa kikao cha familia na kumteua msimamizi na mfuatiliaji wa stahiki hizo.

Kwa upande wa Uongozi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro ulitoa shukrani zao kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Joachim Tiganga, pamoja na Uongozi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha katika kumpumzisha aliyekuwa mtumishi mwenzao kutoka Kanda ya Morogoro.

Mhe. Asajile Joshua Mhando alifariki Dunia mchana wa tarehe 17 Februari 2026 katika Hospitali ya Platinum, mjini Morogoro, alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kujisikia vibaya akiwa kazini. Marehemu atakumbukwa kwa ucheshi wake, busara, unyenyekevu na ari ya kuchapa kazi, kwani hadi umauti unamfikia hakuwa na shauri lolote la mlundikano; alikamilisha mashauri yote aliyopangiwa kwa wakati.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga akizungumza machache katika mazishi hayo.

Viongozi, Majaji wa Mahakama ya Rufani na sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya wakitoa pole kwa wafiwa na kuaga mwili wa Marehemu Mhe. Asajile Mhando katika viunga vya Mahakama Kuu Kanda Mbeya walipopita katika Kanda hiyo wakitokea Mkoani Morogoro

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe Mhe. Francis Kishenyi (aliyesimama) akitoa neno la shukurani katika Mazishi hayo.


Mwili wa aliyekuwa hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Mikese Kanda ya Morogoro Mhe. Asajile Joshua Mhando ukiagwa huko kijijini kwao Vwawa wilaya ya Mbozi mkoa wa Songwe.


Viongozi na sehemu ya watumishi wa Mahakama kutoka Morogoro, Mbeya na Songwe walioshiriki mazishi hayo wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga (wapili kushoto waliosimama mbele)

Sehemu ya waombolezaji katika mazishi hayo.




Viongozi na sehemu ya watumishi wa Mahakama kutoka Morogoro, Mbeya na Songwe walioshiriki mazishi hayo wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga (wapili kushoto kwa waliokaa mbele)

Viongozi na sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya wakitoa pole kwa wafiwa na kuaga mwili wa Marehemu Mhe. Asajile Mhando katika viunga vya Mahakama Kuu Kanda Mbeya walipopita katika Kanda hiyo wakitokea Mkoani Morogoro






Mwili wa aliyekuwa hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Mikese Kanda ya Morogoro Mhe. Asajile Joshua Mhando ukiagwa huko kijijini kwao Vwawa wilaya ya Mbozi mkoa wa Songwe.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni