Jumanne, 3 Machi 2026

KAZI KUPATA KAZI, ITUNZENI KAZI ILI MUWE WATUMISHI WENYE TIJA MAHAKAMANI; JAJI RWIZILE

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile amewataka watumishi wapya wa Mahakama hiyo kuzingatia maadili na umoja katika kutimiza majukumu yao huku wakitanguliza mbele uwajibikaji wa kiwango cha juu katika utumishi wao.

Mhe. Rwizile ametoa wito huo leo tarehe 03 Machi, 2026 ofisini kwake katika mazungumzo aliyofanya na watumishi hao wapya tis awa kada mbalimbali mara baada ya kupokelewa.

“Ninyi ambao mmepata kazi leo mmeona ilivyo kazi kupata kazi, hivyo itunzeni kazi kwa maadili ya hali ya juu, mkiwa kielelezo kazini na mtaani ambapo jamii inatarajia kuona mtumishi wa Mahakama mwenye maadili mazuri na mfano kwa watu wengine,” amesema Mhe. Rwizile.

 Jaji Mfawidhi huyo amesisitiza kuwa, mtumishi yoyote wa Mahakama anayo dhamana katika mnyororo wa utoaji haki, ambalo ni jukumu zito linalohitaji nidhamu, uaminifu na weledi wa hali ya juu, na kuwa watumishi wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya sheria, kuepuka tabia zisizofaa kwa mtumishi wa umma.

Aidha, amewataka pia watumishi hao kujenga umoja na mshikamano na kuwahimiza kujifunza kwa watumishi watakaowakuta katika vituo watakavyopangiwa kazi, huku akisisitiza kuwa nguvu ya Mahakama ipo katika ushirikiano, uwajibikaji na kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa.

Kwa upande wake Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay amewahakikishia watumishi hao mazingira wezeshi ya kazi ikiwemo vifaa na miundombinu itakayowawezesha katika utendaji kazi wao pahala pa kazi.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Yohana Mbelwa, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay na Afisa Utumishi Mwandamizi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Festo Sanga.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile  akizungumza na watumishi wapya wa Mahakama wa Kada mbalimbali walioajiriwa hivi karibuni na kupangiwa Mahakama Kigoma (hawapo katika picha).

Sehemu ya Watumishi wapya wa Mahakama waliopangiwa Kigoma wakifuatilia kwa makini maelekezo aliyokuwa akiyatoa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (hayupo katika picha).

Mtumishi mpya wa Mahakama Kanda ya Kigoma wa Kada ya Udereva, 
Bw. Azizi Saburi Gilla akijitambulisha kwa Viongozi wa Kanda hiyo.

Sehemu ya watumishi wapya tisa wakifuatilia maelekezo ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (hayupo katika picha).

Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay (kulia) akiteta jambo  na Afisa Utumishi Mwandamizi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Festo Sanga wakati wa mazungumzo na watumishi wapya wa Mahakama Kanda hiyo leo tarehe 03 Machi, 2026.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni