Jumanne, 3 Machi 2026

SUMBAWANGA WASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Na. Fredrick Mahava- Mahakama, Sumbawanga

Watumishi Wanawake wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga wameshiriki katika Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali kama vile kufanya matendo ya huruma na kushiriki mafunzo ya ujasiriamali.

 Maadhimisho hayo ya mwaka 2026 yanafanyika na kuadhimishwa kuanzia ngazi ya Kata. Kwa upande wa Kata ya Katandala maadhimsho hayo yamefanyika tarehe 2 Machi 2026 yakiongozwa na Diwani wa Kata hiyo Mhe. Edwin Misasi.

Maadhimisho hayo yalianza kwa Maandamano yaliyoanzia Ofisi ya Kata ya Katandala kuelekea katika kituo cha kulelea watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi cha Bethania ambapo mahitaji mbalimbali ya watoto yalitolewa.

Kwa upande wake Mhe. Deontinta Kashaija ambaye alikuwa Mkuu wa Msafara wa Watumishi wanawake wa Mahakama Kanda ya Sumbawanga wakati anakabidhi mahitaji kwa watoto alisema, walichanga pesa ili kufanikisha upatikanaji wa mahitaji hayo na pia waliwashirikisha baadhi ya wanaume ambao waliguswa na kuchangia na hivyo kuweza kupatikana kwa mahitaji hayo.

Naye, Mkurugenzi wa Kituo cha Bethania aliwashukuru wanawake wote kwa kuwaletea watoto hao mahitaji muhimu ambayo yatawasaidia. Vilevile aliwaomba wawe wanakuja kuwatembelea watoto hao mara kwa mara kwani watoto hao wanafarijika wanapotembelewa na watu mbalimbali.

Aidha, alieleza kuwa wana Vituo viwili vya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu yaani kile cha watoto wadogo wa chini ya miaka 10 na kile cha watoto kuanzia miaka 10 na kuendelea.

Baada kumaliza kutoa mahitaji kwa watoto wa kituo cha Bethania maandamano hayo yalielekea katika Ofisi ya Tarafa ya Lwiche ili kuendana na kauli mbiu ya mwaka isemayo “Haki kwa wanawake na wasichana: msingi wa Maendeleo Jumuishi kufikia Dira 2050” Wanawake walikusanyika katika ukumbi uliopo ofisi ya taarafa ya Lwiche na kupewa mafunzo mbalimabali kuhusu ujasiliamali, elimu kuhusu malezi na makuzi ya watoto na elimu kuhusu fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo jamii.

Vilevile Taasisi za kifedha kama NMB walipata fursa ya kutoa elimu kwa wanawake kuhusu mikopo ya masharti nafuu inayotolewa kwa vikundi mbalimbali na namna gani wanawake wanaweza kunufaika na fursa hizo. Pia walipata wasaa wa kujua fursa ya mikopo inayotolewa na Serikali na kusimamiwa na benki ya NMB ambayo kipaumbele chake wanapewa wanawake.

Nao Jeshi ya Zimatoto na Uokoaji walitumia jukwaa hilo kutoa elimu kwa wanawake kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu namna ya kupambana na majanga ya moto kuanzia ngazi ya familia na kuelezea huduma muhimu zinazotolewa na Jeshi hilo  ikiwa ni pamoja namna ya kutoa taarifa kwa Jeshi hilo pindi unapopata majanga ya Moto.

Aidha, wakati wa Mafunzo hayo wanawake walipata wasaa wa kuuliza maswali mbalimbali kwa kila mada iliyofundishwa na wawezeshaji walitoa ufafanuzi ili kuongeza uelewa kwa washiriki wa mafunzo hayo. Baada  ya mafunzo wanawake walihimizwa kushiriki kilele cha siku ya wanawake duniani itayofanyika tarehe 08 Machi 2026.

Picha ya watumishi wanawake wa Mahakama Kanda ya Sumbawanga wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake katika Kata ya Katandala Sumbawanga Mjini.

Afisa kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji akitoa elimu kuhusu namna ya kupambana na majanga ya moto wakati wa sherehe ya siku ya wanawake kwa Kata ya Katandala Sumbawanga.

Picha ya Pamoja kati ya viongozi wa Kata ya Katandala na wanawake waliohudhuria katika siku ya wanawake.

Picha ya pamoja kati ya Watoto wa kituo cha Bethania na wanawake waliopeleka mahitaji mbalimbali kwa watoto hao.

Afisa Maendeleo ya Jamii Bi. Shukrani Sijaona akitoa mafunzo kuhusu ujasiliamali kwa wanawake waliohudhuria katika sherehe ya siku ya wanawake katika kata ya Katandala Sumbawanga

Diwani wa Kata ya Katandala Mhe. Edwin Misasi akifungua mafunzo kwa wanawake waliohudhuria katika sherehe ya siku ya wanawake katika kata ya Katandala Sumbawanga.

Mheshimiwa Deontina Kashaija akizungumza kwaniaba ya wanawake wakati wanakabidhi  mahitaji kwa watoto wa kituo cha bethania.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni