Na. Hilary Lorry – Mahakama, Lindi
Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Lindi wameombwa kuchukua mikopo katika Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa sababu
benki hiyo imeingia Mkataba maalumu na Mahakama ya Tanzania kutoa mikopo hiyo kwa
riba nafuu.
Taarifa hiyo ilitolewa hivi karibuni
wakati wa Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi
baina ya wataalam kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na watumishi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya ya Lindi.
Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa kikao
hicho Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Mhe. Consolata Peter
Singano alisema kuwa, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia mkataba maalum
na Mahakama ya Tanzania juu ya utoaji wa Mikopo yenye masharti nafuu kwa
watumishi wa Mahakama ya Tanzania.
Mhe.Singano aliwataka watumishi wa
Mahakama hizo kuchangamkie fursa hiyo ya mikopo yenye masharti nafuu kwaajili
ya kufanyia shughuli za maendeleo, kuliko kuchukua mikopo kwenye taasisi za
fedha zenye riba kubwa.
Naye, Meneja wa Benki ya Taifa ya Biashara
(NBC) Tawi la Lindi, Bw. Iovan Mapunda wakati wa uwasilishaji wa mada katika
mkutano huo alisema kwamba Benki hiyo ilianzishwa rasmi Mnamo mwaka 1967 huku
akipambanua kuwa benki hiyo ina hazina kubwa ya historia katika upande wa
utoaji wa huduma bora za kibenki hapa Tanzania, pia akieleza kuwa benki hiyo
ina bidhaa (products) nyingi za huduma kwa wateja wake.
Aidha, Meneja huyo alisisitiza kuwa endapo
Mtumishi wa Mahakama ataamua ku pitisha mshahara wake benki ya NBC atapata
Mkopo kwa asilimia 14 badala ya asilimia 17 ambazo zimezoeleka na zinazoonekana
katika mfumo wa watumishi portal (ess),vilevile alieleza kuwa mkopo huo unaenda
hadi miaka 65 kwa watumishi wa kawaida na miaka 80 kwa Majaji na yote hayo ni kutokana na Mkataba maalum
ulioingiwa kati ya benki hiyo na Mahakama ya Tanzania.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano kutoka
Makao Makuu ya Beki hiyo Bw. Peter Mwasomola, aliongeza kuwa benki hiyo inatoa
mikopo maalum kwa kuwakopesha watumishi wa Mahakama fedha kwa ajili ya kununua hati
fungani za Serikali.
Vilevile, aliongeza kuwa, benki hiyo
inatoa mikopo ya haraka (Chap chap loan) kupitia simu ya Mkononi yaani Salary Advance
hadi asilimia 50 ya mshahara wako na kikubwa zaidi unaweza kuchukua mkopo huo
kwa muda wa hadi miezi 12.
Bw.
Mwasomola aliwataka watumishi wa Mahakama ya Tanzania kufika katika ofisi za
NBC kuchukua mikopo hasa ya muda mrefu ili kuitumia katika shughuli zao za
maendeleo. “Kukopa siyo kubaya ila kukopa bila malengo ndiyo kubaya” alisistiza
Bw. Mwasomola.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi
Mhe.Consolata Peter Singano (aliyefunga kilemba katikati) akitoa neno wakati wa ufunguzi
wa Mkutano huo.
Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya ya
Lindi wakifuatilia mada zilizowasilishwa na wataalamu wa fedha kutoka benki ya
Taifa ya Biashara (NBC) kwa umakini Mkubwa.
Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi.Quip
Godfrey Mbeyela akitoa neo la utangulizi na ukaribisho kwa wataalamu kutoka
Benki ya Taifa ya Biashara na Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya
ya Lindi.
Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya ya
Lindi wakifuatilia mada zilizowasilishwa na wataalamu wa fedha kutoka benki ya
Taifa ya Biashara (NBC) kwa umakini Mkubwa.
.jpeg)
Meneja wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) tawi la
Lindi Bw. Iovan Mapunda aliyenyoosha
mkono akifafanua jambo wakati wa mkutano uliowakutanisha benki ya NBC na
watumishi wa Mahakama ya Lindi.




.jpeg)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni