- Jaji Mkuu asema uwajibikaji, mageuzi ya kiutendaji ili kulinda imani ya wananchi
Na HALIMA MNETE & JAMES BUSANYA-Mahakama, Dodoma
Mkutano
wa kwanza wa mwaka 2026 kati ya Mahakama ya Tanzania na Wadau
wa sekta ya haki jinai umefanyika jana tarehe 2
Machi, 2026 katika ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania jijini
Dodoma.
Lengo la mkutano huo ni kupitisha tathmini ya utekelezaji wa mikakati iliyokubaliwa
hapo awali na kuweka mwelekeo wa pamoja katika kuimarisha ushirikiano na
mahusiano katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji haki mahakamani.
Mkutano
huo uliongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher
Mohamed Siyani, huku Mgeni Rasmi akiwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George
Masaju.
Akifungua
mkutano huo, Jaji Mkuu alisisitiza kuwa uimara wa mnyororo wa haki jinai
unategemea kwa kiasi kikubwa uwajibikaji wa kila Taasisi
katika kutekeleza wajibu wake kwa wakati, kwa kuzingatia Katiba na sheria za
nchi.
Alieleza
kuwa haki inapocheleweshwa huathiri si wahusika wa shauri pekee,
bali pia hupunguza imani ya wananchi kwa mfumo mzima wa utoaji haki.
Katika
kikao hicho, Wadau mbalimbali waliwasilisha taarifa za utekelezaji wa
majukumu yao pamoja na changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa
mkakati wa haki jinai.
Bi.
Singwa Mokiwa, aliyemwakilisha Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, alieleza kuwa Taasisi
ya Uhamiaji imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na
maadili ya utumishi wa umma.
Alisema
Taasisi hiyo inahakikisha watuhumiwa wanafikishwa mahakamani
kwa wakati, vielelezo vinawasilishwa ipasavyo na amri za Mahakama zinatekelezwa
bila kuchelewa.
Hata
hivyo, alibainisha changamoto zikiwemo ucheleweshaji wa usajili wa majalada
katika baadhi ya maeneo, upungufu wa wakalimani na ucheleweshaji wa upatikanaji
wa mashahidi, hali inayoweza kusababisha watuhumiwa kukaa mahabusu kwa muda
mrefu zaidi.
Kwa
upande wake, Bi. Alice Mtulo kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
aliwasilisha tathmini ya mashauri ya kikatiba na haki za binadamu yenye
viashiria vya jinai yanayosimamiwa na ofisi hiyo. Alieleza kuwa katika kipindi
cha Julai hadi Desemba 2025, ofisi ilisajili mashauri 1,693 ya madai, ambapo
216 yalikuwa mashauri ya kikatiba na haki za binadamu, yakiwemo mashauri ya
uchaguzi.
Bi
Alice pia alibainisha kuwa changamoto kubwa ni ucheleweshaji wa upatikanaji wa
taarifa kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali wakati wa kuandaa majibu ya
utetezi, pamoja na ufinyu wa muda wa siku 14 uliowekwa kwa mujibu wa kanuni za
mashauri ya kikatiba na haki za binadamu.
Aidha,
alieleza changamoto ya matumizi ya hati za dharura katika baadhi ya mashauri
bila kuwepo utaratibu madhubuti wa kuthibitisha udharura wake, jambo linaloweza
kuathiri maandalizi ya kina ya utetezi wa Serikali.
Ofisi
hiyo imeweka mikakati ya kuimarisha mafunzo kwa Mawakili wa Serikali, kuboresha
mawasiliano kupitia mfumo wa usimamizi wa mashauri (CMIS) na kuanzisha mifumo
ya kupata taarifa za mashauri kwa njia ya simu za kiganjani.
Vilevile,
Mkurugenzi Divisheni ya Uaimamizi wa Kesi na Uratibu wa Upelelezi, Bw.
Siraji Iboru, alisema kikao hicho kilipitia na kuthibitisha utekelezaji
wa mikakati minane iliyokubaliwa katika kikao kilichopita.
Alieleza
kuwa ofisi hiyo hufanya vikao vya kila Wiki kwa
ajili ya tathmini ya utendaji na utoaji wa maelekezo kwa watumishi wake.
Alibainisha kuwa mlundikano wa kesi umepungua na kiwango cha ushindi wa kesi
kimeongezeka na kufikia asilimia 84.
Hata
hivyo, alieleza kuwa bado kuna changamoto ikiwemo baadhi ya Wilaya
kukosa Magereza na uhaba wa Waendesha Mashtaka
katika maeneo kadhaa.
Naye
Kamishna wa Jeshi la
Magereza, Afande Nicodemus Tenga, alieleza kuwa Jeshi limeendelea kuimarisha
uwajibikaji kwa kuingiza maudhui ya uwajibikaji katika mitaala ya mafunzo ya
muda mrefu na muda mfupi kwa Askari na Maofisa
wake.
Aidha,
vituo 181 vya Magereza tayari vimeunganishwa na Mahakama kwa njia ya
mtandao, hatua inayorahisisha ufuatiliaji wa mashauri na upatikanaji wa taarifa
kwa wakati.
Jeshi
hilo pia linaendelea kusimika mfumo wa taarifa za Wafungwa
unaounganishwa na Taasisi mbalimbali, ikiwemo
NIDA, NECTA, Mahakama na Jeshi la Polisi. Pamoja na jitihada hizo, changamoto
ya ukosefu wa Magereza katika baadhi ya Wilaya
imeelezwa kuongeza gharama za usafirishaji wa Wafungwa.
Kwa
upande wake, Bw. Joseph Kisusi, ambaye ni Kamishna Msaidizi Kanda ya
Kati Dodoma na Mwakilishi wa Kamishna Jenerali, Mamlaka ya Kudhibiti na
Kupambana na Dawa za Kulevya, alisema ofisi hiyo imeendelea
kuwajengea uwezo watumishi wake na kuimarisha maadili katika utekelezaji wa
majukumu.
Alieleza
kuwa kamati maalum zimeanzishwa kwa ajili ya kufuatilia na kusimamia maadili ya
watumishi, huku wakisisitizwa kuheshimu hadhi na mamlaka ya Mahakama
wanapotekeleza majukumu yao.
Katika
mkutano huo pia, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Bonaventure
Mwabukusi, alisema chama hicho kimeendelea kusimamia kwa ukali maadili ya
taaluma ya uwakili, hususan kwa Mawakili
wanaochukua fedha za wateja bila kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa
makubaliano.
Alieleza
kuwa TLS imekuwa ikiwalazimisha Mawakili
watakaobainika kukiuka maadili kurejesha fedha kwa wateja wao pamoja na
kuchukuliwa hatua stahiki za kinidhamu kwa mujibu wa Katiba na kanuni za chama.
Alisisitiza kuwa chama hicho hakitavumilia vitendo vinavyodhalilisha taaluma ya
uwakili na kuathiri imani ya wananchi kwa mfumo wa haki.
Aidha,
alisema TLS inaendelea kutoa elimu ya maadili kwa Mawakili
ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Katiba, sheria na
kanuni za taaluma, pamoja na kuheshimu ukuu na hadhi ya Mahakama.
Alibainisha
kuwa chama hicho kimeimarisha ushirikiano na Wadau wa
mnyororo wa haki jinai, kinaendelea kutoa mafunzo ya maadili kwa Mawakili
wapya na kusisitiza umuhimu wa msaada wa kisheria kwa wasiojiweza ili
kuendeleza dhana ya usawa mbele ya sheria.
Wakili
Mwabukusi pia alisema TLS inakaribia kukamilisha matumizi ya mifumo ya
kidijitali itakayowezesha mawasiliano na ushirikiano wa karibu zaidi na Wadau
wa sekta ya haki jinai.
Hata
hivyo, alitaja changamoto zinazoikabili taaluma hiyo kuwa ni pamoja na vitisho
dhidi ya Mawakili, masuala ya ulinzi na uhuru wa taaluma ya uwakili.
Alisisitiza kuwa Wakili anapomtetea mteja mahakamani haimaanishi anahusika na
kosa analodaiwa mteja wake, bali anatekeleza wajibu wake wa kisheria wa
kuhakikisha haki inapatikana kwa mujibu wa sheria.
Kwa
ujumla, mkutano huo umeonesha dhamira ya pamoja ya kuimarisha uwajibikaji,
maadili na matumizi ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
katika Taasisi zote za mnyororo wa haki jinai.
Wadau
walikubaliana kuwa ushirikiano wa karibu, mawasiliano ya wazi na utekelezaji wa
majukumu kwa weledi ndivyo vitakavyoendelea kuimarisha utoaji haki na kulinda
imani ya wananchi kwa mfumo wa Mahakama nchini
Mkutano
huo umehitimishwa kwa msisitizo kwamba utoaji haki ni dhamana ya pamoja ya Taasisi
zote katika mnyororo wa haki jinai, na kwamba uwajibikaji, maadili na
ushirikiano wa karibu ndivyo vitakavyoendelea kuimarisha imani ya wananchi kwa
mfumo wa Mahakama nchini.
Kamishna Msaidizi Kanda ya Kati Dodoma na Mwakilishi wa Kamishna Jenerali, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Bw. Joseph Kisusi.
Mkurugenzi Divisheni ya Usimamizi wa Kesi na Uratibu wa Upelelezi, Bw. Siraji Iboru.
Wadau wakichukua kumbukumbu kwenye mkutano huo.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni