- Msajili Mkuu asema ushirikiano, mahusiano imara ni msingi wa utoaji haki
Na Halima Mnete-Mahakama,
Dodoma
Msajili Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, jana tarehe 2 Machi, 2026 amezungumza na Waandishi
wa Habari kuhusu mkutano wa kwanza wa mwaka 2026 kati ya Mahakama na Wadau wa
haki jinai, uliolenga kuimarisha ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa
majukumu ya utoaji haki mahakamani.
Akizungumza katika
mkutano huo katika ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Nkya
alisema kuwa kikao hicho ni mwendelezo wa makubaliano yaliyofikiwa tarehe 24
Septemba, 2025. Katika kikao hicho, Mahakama na Wadau walikubaliana kuweka
mikakati tisa ya pamoja, ikiwemo kufanya vikao mara nne kwa mwaka ili
kuimarisha uratibu na mawasiliano katika mnyororo wa haki jinai.
Alisema kuwa mkutano huo
wa kwanza kwa mwaka 2026 umejikita katika tathmini ya utekelezaji wa mikakati
iliyowekwa pamoja na kuweka mwelekeo wa pamoja kwa mwaka, kwa lengo la
kuhakikisha mashauri yanashughulikiwa kwa ufanisi na kwa wakati.
“Utoaji haki ni jukumu la
pamoja, Mahakama haiwezi kufanya kazi peke yake bila ushirikiano madhubuti wa Wadau
wote katika sekta ya haki jinai. Mahusiano yetu ya kikazi ndiyo msingi wa
kuongeza ufanisi na kuimarisha imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama,” alisema.
Akiwasilisha mafanikio
yaliyopatikana kupitia ushirikiano huo, Msajili Mkuu alieleza kuwa katika
kipindi cha Septemba hadi Desemba 2025, mashauri 30,076 yalifunguliwa huku
mashauri 38,639 yakimalizika, sawa na asilimia 128 ya mashauri yaliyofunguliwa
katika kipindi hicho.
Kwa mwaka mzima wa 2025,
mashauri ya jinai 138,368 yalifunguliwa katika ngazi zote za Mahakama na
mashauri 145,467 yalimalizika, sawa na asilimia 105 ya mashauri
yaliyofunguliwa. Kutokana na hali hiyo, Mahakama ilifunga mwaka ikiwa na
mashauri 14,172 pekee yanayoendelea, ambapo asilimia 75 ya mashauri hayo yana
umri usiozidi miezi sita.
Aidha, Mhe. Nkya alieleza
kuwa ushirikiano huo umeimarisha matumizi ya mifumo ya kidigitali, hususan
mfumo wa JOT-eCMs ambao umeunganishwa na mifumo ya Wadau mbalimbali ili
kurahisisha usimamizi na ufuatiliaji wa mashauri. Kupitia mfumo wa Mahakama Mtandao,
mashauri 24,662 yalisikilizwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2025.
Vilevile, aligusia
kutungwa kwa Kanuni katika Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya, ambazo zimempa
haki mshtakiwa kupewa ushahidi wa upande wa mashtaka mapema, hatua ambayo
imeongeza uwazi na kuharakisha usikilizaji wa mashauri.
Akihitimisha, Msajili
Mkuu alisisitiza kuwa Mahakama itaendelea kuimarisha mahusiano ya kikazi na Wadau
wake kwa mwaka 2026, kwa lengo la kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati, kwa
uwazi na kwa kuzingatia misingi ya sheria, huku akiipongeza vyombo vya habari
kwa mchango wao katika kuhabarisha umma kuhusu masuala ya haki na sheria.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni