Jumatatu, 2 Machi 2026

JAJI MKUU ASISITIZA UTAWALA WA SHERIA NA USHIRIKIANO WA KIKATIBA

Na HABIBA MBARUKU, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju amezitaka Taasisi za Haki Jinai kudumisha ushirikiano katika kutekeleza mikakati ya Haki Jinai ili kuendelea kufanikisha upatikanaji wa Haki kwa haraka katika jamii sambamba na kudumisha utawala wa sheria na ushirikiano wa kikatiba ili kuleta amani, ustawi na maendeleo katika Taifa.

Mhe. Masaju ameyasema hayo leo tarehe 02 Machi, 2026 alipokuwa akifungua na kufunga mkutano wa kwanza kwa Mwaka 2026 wa Wadau wa Haki Jinai, uliofanyika katika ukumbi wa Mkutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Mkuu ameeleza kuwa, ushirikiano uliopo umejengwa katika wajibu wa kila Taasisi na kwamba wajibu wa Kikatiba na Kisheria wa kila Mdau wa Haki Jinai ndio unaozalisha ushirikiano huo, huku akirejea Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13 mnamo tarehe 14 Novemba, 2025 ambapo Rais Samia  alisema kwamba, "msingi wa mafanikio yote ya nchi unategemea utawala wa sheria ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Mahakama ya Tanzania ili haki ipatikane kwa wote mapema ipasavyo."

“Ushirikiano huu tulionao pia umejengwa katika wajibu wetu, wote hapa wajibu wetu ni wa kikatiba na kisheria, utekelezaji wa Sheria au Katiba unazalisha ushirikiano, lakini pia tunashukuru kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa mujibu wa Katiba pia ndiye Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu amekuwa akisistiza juu ya ushirikiano huu wa Mahakama na Wadau wake,” amesisitiza Mhe. Masaju.

Kadhalika, Jaji Mkuu ameendelea kuutambua mchango wa Jukwaa la Haki Jinai katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu kama ambavyo Mhe. Dkt. Samia alivyosisitiza katika hotuba yake ya kufungua Bunge kuhusu umuhimu wa jukwaa la Haki Jinai ambapo alisema kwamba, Serikali itaendelea kufanya mageuzi na maboresho katika Taasisi zote zinazoshughulikia masuala ya Haki Jinai ili ziweze kukabiliana na vitendo vya uhalifu jambo linaloonesha umuhimu wa Taasisi hizi katika utekelezaji wa Utawala wa Sheria ambao umewekwa kwenye Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Mhe. Masaju amesisitiza kuwa, Mahakama iko tayari kuendelea kushughulikia changamoto ambazo zimeonekana kukwamisha utekelezaji wa mikakati iliyowekwa, kwa kuzingatia mikakati iliyowekwa ili kushughulikia changamoto hizo na kila Taaasisi inahusika kuzirekebisha changamoto hizo mapema ipasavyo.

“Tutaendelea kuwa tayari kushughulikia zile changamoto ambazo tulikuwa tunaziona zinatukwamisha lakini kwa kuzingatia ile mikakati ambayo tumeiweka ya kushughulikia hizo changamoto kwa hiyo hizo changamoto zinazojitokeza kila Taasisi inayohusika twende tukazirekebishe mapema ipasavyo na matokeo au tija yaanze kuonekana mapema,”ameeleza Jaji Mkuu.

Ameongeza kuwa, kila mtu katika jamii anao wajibu wa kuifuata na kuitii Katiba na Sheria za nchi, kwa kufuata utaratibu uliowekwa, kadhalika kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na Sheria za nchi, huku akiwataka Mawakili wa Kujitegemea wanapowakilisha watu fulani, wasichukuliwe kama wahusika wa tuhuma, bali wapewe ushirikiano ili na wao waweze kutimiza majukumu yao ya kikatiba.

Akirejea hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kwa mwaka 2026 tarehe 02 Februari mwaka huu alisisitiza kuhusu wadau kushirikiana na Mahakama katika suala la utoaji haki, huku akizitaja faida zake kuwa ni, kuongeza kasi ya utoaji haki, kulinda uhuru na ukuu wa Mahakama na heshima yake, kupunguza migogoro ya kiutendaji ambayo waathirika ni wananchi, kuimarisha imani ya umma kwa mfumo wa utoaji haki, kukuza Utawala wa Sheria, kuzuia migogoro ya kimaslahi.

Faida nyingine alizozitaja ni pamoja na kurahisisha utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama ambapo lengo kuu ni ustawi wa wananchi kama ambavyo inaelezwa vizuri katika Ibara ya 8(1)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inasema lengo kuu la Serikali ni ustawi wa wananchi, huku ripoti ya Msajili Mkuu ya utendaji wa shughuli za kazi za Mahakama kwa mwaka 2025 ikithibitisha faida zilizoletwa na mahusiano na ushirikiano mzuri baina ya Mahakama na Wadau katika kuyafikia mafanikio.

Aidha, Mhe. Masaju ameongeza kuwa, ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu si jambo la hisani wala maelewano ya kirafiki bali ni takwa la kikatiba, kisheria na kisera hivyo wadau wote watenge muda wao kuhudhuria katika vikao, isipokuwa kwa sababu za msingi za kutohudhuria na ikitokea hivyo watume wawakilishi kwa sababu katika vikao ndipo changamoto za utekelezaji na mafanikio ya kila Taasisi yanapoonekana.

Akizungumza kuhusu maana ya haki, Jaji Mkuu ameeleza kuwa, Haki ni uamuzi unaofanywa na Mahakama kwa kuzingatia na kutekeleza masharti ya Katiba na Sheria kwa mujibu wa ushahidi ulioletwa mahakamani huku akisisitiza Taasisi zinazohusika kujitahidi ushahidi uwe unaojitosheleza.

“Kwa maana hiyo, basi tujitahidi kwa Taasisi zinazohusika zinapokusanya ushahidi, ushahidi uwe ule unaotosheleza kufanya kesi iende mahakamani na Mahakama inapofanya maamuzi kama mtu hakuridhika akate rufaa vinginevyo Mahakama ndio ina jukumu la kutamka hiyo haki,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Akisisitiza kuhusu ushirikiano, Mhe. Masaju amesema kwamba, majukumu ya utoaji haki hayaihusu Mahakama peke yake, hivyo kila Taasisi inapaswa kutekeleza wajibu wake akirejea hotuba ya Rais Samia katika Siku ya Sheria mwaka 2026 ambapo alisema na kuagiza kutoa haki kwa kuzingatia masharti yaliyoainishwa katika Ibara ya 107A(2)(a)(e) na 107B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuheshimu na kuulinda uhuru wa Mahakama bila kuutumia vibaya, kutotumia uhuru huo kama kichaka cha kuficha uzembe na vitendo visivyo vya haki.

Pia kutenda kwa uadilifu na kwa uwazi, kuendeleza suala la usimamizi wa dhamana ili kuhakikisha kuwa, watuhumiwa wenye stahili ya kupata dhamana wanapata dhamana kwa mujibu wa sheria, pia wadau wote wa Mahakama katika suala la dhamana kuunga mkono jitihada za Mahakama katika suala la dhamana.

Kadhalika kuendeleza kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia, pia wadau wa haki kuendelea kushirikiana na Serikali na Mahakama katika utoaji wa msaada wa kisheria kwa wasioweza kumudu gharama, kuimarisha ushirikiano kwa utoaji huduma za kisheria mapema ipasavyo na kwa ufanisi, pia kuendelea kushirikiana na Mahakama katika kuimarisha Utawala wa Sheria pamoja na Taasisi za Haki Jinai kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai.

Kadhalika, Jaji Mkuu amewashauri wadau wengine kurejea mapendekezo mbalimbali ya Mhe. Dkt. Samia kuhusu utoaji haki na kujiridhisha endapo wameshayatekeleza na kuchukua hatua kwa sababu jukumu hilo ni jukumu mtambuka, jukumu jumuishi, la pamoja ambalo haliwezi kuwa jukumu la Mahakama peke yake.

Ameongeza kuwa, kila jamii yoyote lazima iwe na Viongozi kwa ajili ya kusimamia Utawala wa Sheria na mambo mengine, "kwa hiyo ni vyema kuwa tayari na hasa sisi watumishi wa umma kuwa tunafuatilia kunasemwa nini kwenye sekta yetu lakini na Viongozi Wakuu wa Serikali ngazi ya Taifa wanasema nini."

Amesema kuwa, masuala ya jinai yanapodhibitiwa kwa ufanisi ipasavyo yanawezesha wananchi kushiriki shughuli zao za kiuchumi, kisiasa na kijamii ipasavyo na hivyo kuimarisha uwepo wa ustawi  na maendeleo ya Taifa, jambo linalodhihirisha mchango wa Mahakama katika ustawi na maendeleo ya Taifa kama ilivyo kaulimbiu ya Mahakama kwa mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju ameeleza kuwa, msingi mkuu wa Dira ya Maendeleo 2050 ni Utawala, Amani, Usalama na Utulivu ambapo ndipo umuhimu wa Sekta ya Sheria unaonekana, Mahakama na Wadau wake wa Haki Jinai, kwa sababu kama huo ndio msingi mkuu unaowezesha mengine yote kutekelezwa.

Aidha, amefafanua kuwa, katika hotuba ya Rais, Mhe. Dkt. Samia  ya Siku ya Sheria mwaka 2026 alieleza kuwa, Mahakama ina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 na kuelekeza mambo kadhaa yafanyike ikiwa ni pamoja na  kuendelea kulinda haki na misingi ya Katiba, ambapo alihimiza  Mahakama isitoke katika misingi yake na jukumu lake, kuhakikisha migogoro ya kiuchumi, kibiashara na kijamii inatatuliwa kwa haraka na kwa haki, kujenga imani ya wananchi na wawekezaji katika mfumo wa kisheria wa nchi, kukuza uwajibikaji  na nidhamu katika utumishi wa umma na wa sekta binafsi.

Vilevile, kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa ambao ni msingi wa maendeleo endelevu, kuwezesha mazingira bora ya uwekezaji na ukuaji  wa uchumi kwa kuhakikisha Utawala wa Sheria unazingatiwa, kulinda haki za makundi maalumu wakiwemo Wanawake, Watoto na watu wenye mahitaji maalumu, kuzuia migogoro inayoweza kuwa chanzo cha mgawanyiko wa kijamii au kisiasa.

Pia, kuharakisha utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo kwa kutoa tafsiri ya kisheria iliyo wazi na thabiti, kujenga na kuimarisha utamaduni wa kuheshimu sheria, haki na taasisi za umma, kuchangia katika mapambano dhidi ya rushwa na matumzizi mabaya ya madaraka kwa kutoa haki bila upendeleo pamoja na kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa kwa kuwahakikishia ulinzi wa haki zao za kisheria.

Mhe. Masaju amebainisha kuwa, Mahakama inaendelea kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi, pamoja na kufanya  ugatuzi wa Mahakama ya Rufani, ambapo mwezi Aprili Mahakama zinazoanzishwa katika Kanda za Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Tabora pamoja na Makao Makuu Dodoma zitaanza kufanya kazi.

"Sambamba na hilo, Kanda za Mahakama Kuu nazo zinafunguliwa mapema mwezi huu ambazo ni Mahakama Kuu Singida, Mahakama Kuu Songwe, Mahakama Kuu Katavi, Mahakama Kuu Njombe na Mahakama Kuu Lindi, hii ikiwa ni hatua kubwa inayopigwa na Mahakama katika kutambua umuhimu wa utawala wa sheria katika ustawi na maendeleo ya taifa letu," ameeleza Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amehitimisha kwa kushauri na kuhimiza kuwa, mikutano itapimwa kwa utekelezaji wa majukumu ipasavyo na si kwa idadi na wingi wa mikakati.

“Niwashauri na kuwahimiza kuwa mikutano yetu hii itapimwa si kwa idadi ya wingi wa mikakati bali kwa ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yetu ipasavyo hususan katika jukumu la utoaji haki mapema ipasavyo, kila aliye na wajibu wa kutekeleza atekeleze,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza na  Wadau wa Utekelezaji wa Mkakati wa Haki Jinai kuhusu ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji haki Mahakamani uliofanyika leo tarehe 02 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa Jaji Mkuu- Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika Mkutano wa Wadau wa Utekelezaji wa Mkakati wa Haki Jinai. Aliyeketi kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani na kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amiri Mruma. 

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akizungumza jambo na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani wakati wa mawasilisho ya Utekelezaji wa Mkakati wa Haki Jinai kwa Wadau na Taasisi zinazohusika, katika mkutano wa kwanza kwa mwaka 2026 uliofanyika leo tarehe 02 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa Mkutano wa Jaji Mkuu, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. 

 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, Mhe. Abdi Kagomba akifuatilia mawasilisho ya utekelezaji wa mikakati ya Haki Jinai wakati wa mkutano huo uliofanyika leo tarehe 02 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa Mkutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akifuatilia kwa makini mawasilisho kutoka kwa Wadau wa Mnyororo wa Haki Jinai katika mkutano uliofanyika leo tarehe 02 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa Mkutano wa Jaji Mkuu- Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Sehemu ya Wadau wa mnyororo wa utekelezaji wa Mkakati wa Haki Jinai walioshiriki katika mkutano huo.

 

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya akifuatilia mawasilisho katika mkutano huo.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Arusha)



 


 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni