Jumamosi, 7 Machi 2026

JAJI MAGHIMBI AWAFUTURISHA WATUMISHI KANDA YA DAR ES SALAAM

  •  Achukua fursa hiyo kuwakumbusha watumishi kufanya kazi kwa bidii

 Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi ameandaa Iftar maalum kwa ajili ya kuwafuturisha Watumishi wa Kanda hiyo. 

Mhe. Maghimbi aliyasema hayo wakati wa hafla ya iftar aliyoiandaa kwa ajili wa watumishi wa Kanda hiyo iliyofanyika jana tarehe 06 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Dar es Salaam. 

Aidha, Mhe. Maghimbi amewaasa watumishi wa Kanda hiyo kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo.

Akizungumza wakati wa kuwakaribisha Majaji na watumishi wengine  kwa ajili ya kufuturu, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Aziza Mbadjo alisema kwa muda sasa, Jaji Mfawidhi huyo amekuwa akiandaa iftar kwa watumishi wa Dar es Salaam, lakini safari hii amepanua wigo na kuwaalika Wafawidhi, mtendaji wa Mkoa wa Pwani na Maafisa na kujumuika pamoja katika Iftar hiyo.

“Tumekuwa tukifanya kwa kuwaalika Wafawidhi wa Dar es Salama tu  pamoja na viongozi wengine lakini safari hii tumeongeza wigo Mahakimu Wafawidhi Mkoa wa Pwani, Watendaji pia pamoja na Maafisa wao,” alisema Mhe. Mbadjo.

Hafla hiyo ilitanguliwa na dua ya kuwaombea watumishi wawili wa Kanda hiyo waliotangulia mbele ya haki na dua hiyo iliongozwa na Msaidizi wa Kumbukumbu kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Khalid Kawiza.

Akitoa shukrani baada kushiriki iftar hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Arnold Kirekiano alisema anamshukuru Mungu kwa ajili ya Jaji Mfawidhi kwa kutoa sadaka hiyo kwa watumishi maana inaleta umoja baina ya watumishi, ameomba kwa wakati mwingine ifanyike mahali pengine na kwa namna nyingine ambayo Mungu atawajaalia.

Aidha, Mhe. Kirekiano alisema, siku hiyo imewapa fursa ya kutafakari pamoja kutokana na ratiba za kazi na mfungo huo hawajaweza kuonana, lakini kwa jambo hilo wameweza kukaa kwa pamoja.

Kadhalika, Jaji Kirekiano amemtakia heri Mhe. Maghimbi lakini pia watumishi wote walioshiriki jambo hilo ili ikawe heri kuwasaidia katika kuwatumikia wananchi.

Amewakumbusha kwamba wanakutana kwa ajili ya kazi za kuwahudumia wananchi na Jaji Mfawidhi ameonesha ukarimu, nao wanaweza kulipa kwa kuonesha ukarimu kwa wateja wanaowahudumia kwa upendo na kwa furaha.

Mhe. Maghimbi amekuwa na utaratibu wa kuandaa iftar kila mwaka kwa takriban miaka mitatu mfululizo.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akitoa neno kabla ya kupata Iftar jana tarehe 06 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama hiyo. Aliyeketi kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Butamo Phillip  na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale.

 Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakiwa katika hafla ya Iftar iliyoandaliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (wa tatu kushoto).





 Majaji na Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam wakipata Iftar.


Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Livin Lyakinana (katikati) na Mhe. Aziza Mbadjo (wa pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Jiji, Ubungo, Ilala na Temeke mara baada ya kufuturu iftari iliyoandaliwa na Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Salma Maghimbi.

 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi (katikati) akiwa na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya Kibiti, Mkuranga,Bagamoyo na Kibaha Baada ya Iftar iliyofanyika jana tarehe 06 Machi, 2026 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Msaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Khalid Kawiza akitoa dua wakati wa hafla ya Iftar.

Watumishi wakifuatilia dua kabla ya Iftar.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Arnold Kirekiano akitoa neno la shukrani baada ya Iftar.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni