Jumamosi, 7 Machi 2026

MSAJILI MKUU AFUNGA MAFUNZO YA MAHAKIMU WAKAZI 92

.Awasisitiza kuzingatia maadili, kuimarisha weledi na kutumia TEHAMA katika utoaji wa haki

Na. James Busanya & Halima Mnete – Mahakama, Dodoma

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, amewasisitiza Mahakimu Wakazi wapya kuzingatia maadili ya kazi, kuongeza weledi wa kitaaluma na kulinda taswira ya Mhimili wa Mahakama katika utoaji wa haki kwa wananchi.

Mhe. Nkya ametoa wito huo jana tarehe 6 Machi 2026 katika ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, wakati akifunga rasmi mafunzo elekezi ya siku kumi kwa Mahakimu Wakazi wapya 92, mafunzo yaliyoandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Nkya amesema ana furaha kushiriki hitimisho la mafunzo hayo na kueleza matumaini kuwa siku kumi za mafunzo zimewajengea washiriki uwezo mpana kuhusu majukumu ya uhakimu na misingi ya utoaji wa haki kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Amesema kazi ya uhakimu ni wito unaohitaji umakini mkubwa kwa kuwa sehemu kubwa ya majukumu yake inahusiana moja kwa moja na utoaji wa haki kwa jamii, hivyo Mahakimu wanapaswa kutambua uzito wa dhamana waliyopewa na kuitumikia kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu.

Katika kusisitiza hilo, alimnukuu Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyewahi kusema kuwa zipo kazi nyingi zinazoweza kufanywa na mtu yeyote, lakini kazi ya uhakimu si mojawapo kutokana na uzito wake na mahitaji ya juu ya kitaaluma pamoja na kimaadili.

Aidha, Mhe. Nkya aliwakumbusha Mahakimu hao kuwa uhuru wa Mahakama upo pale Hakimu anapozingatia kiapo chake cha kazi na kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria bila kuingiliwa na mtu au chombo chochote.

Msajili Mkuu huyo, aliwataka kushirikiana na wadau wa sekta ya haki pamoja na viongozi wengine katika maeneo watakayopangiwa kazi, akieleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuboresha utendaji kazi na kuongeza ufanisi wa huduma ya utoaji haki kwa wananchi.

Vilevile, Mhe. Nkya aliwataka Mahakimu hao kuzingatia Kanuni za Maadili ya Mahakama za mwaka 2020 ndani na nje ya Mahakama kwa kusoma, kuelewa na kuzifuata kikamilifu, akibainisha kuwa Mahakama imara hujengwa na watumishi wenye uadilifu.

“Mahakama imara hujengwa na watumishi wenye uadilifu na kosa la Hakimu mmoja linaweza kuchafua taswira ya Mhimili mzima wa Mahakama,” alisisitiza Mhe Nkya.

Kwa upande wa maendeleo ya kitaaluma, Msajili Mkuu aliwahimiza Mahakimu hao kuendelea kujifunza na kujielimisha ili kuongeza weledi wao katika utoaji wa haki na kuepuka makosa yanayoweza kuepukika katika utendaji wao wa kazi.

Pia aliwataka kujiepusha na vitendo vya rushwa, upendeleo na ubaguzi, kuzingatia nidhamu ya kazi, kutumia lugha ya staha kwa wadau wa Mahakama pamoja na kutumia rasilimali za ofisi kwa ufanisi.

Katika hatua ya kuimarisha utendaji kazi wao, Mahakimu hao walikabidhiwa vitendea kazi ikiwemo kompyuta mpakato zitakazowasaidia katika uandishi wa hukumu na uendeshaji wa mashauri mbalimbali kwa njia ya kidijitali.

Mhe. Nkya pia aliwahimiza kuwakilisha ipasavyo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kazi zao za kila siku ili kuongeza ufanisi na kasi ya utoaji wa haki.

Aidha, Mhe. Nkya aliwataka Mahakimu hao kulinda taswira ya Mahakama wakati wote na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha kukutana katika mafunzo hayo, huku akiwaombea mafanikio mema katika utekelezaji wa majukumu yao mapya ya kuhudumia jamii kupitia Mhimili wa Mahakama.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Kiaki Nkya, akifunga rasmi mafunzo elekezi ya siku 10 kwa Mahakimu Wakazi wapya 92, yalioandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania jana tarehe 6 Machi, 2026 katika Ukumbi wa mikutano Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.

Sehemu ya Mahakimu Wakazi wapya waliomaliza mafunzo ya siku 10 wakisikiliza hotuba ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya (hayupo pichani)

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Kiaki Nkya (Katikati) akiwa Meza Kuu na Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo Bi. Patricia Ngungulu (wa kwanza kulia) wakati wa kufunga mafunzo hayo elekezi kwa Mahakimu Wakazi Wapya 92.

Sehemu ya Mahakimu Wakazi wapya waliomaliza mafunzo ya siku 10 wakisikiliza hotuba ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya (hayupo pichani)

 (Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni