Na. Ally Ramadhani - Katavi
Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mkoa wa Katavi Mhe. Silivia S. Lushasi
tarehe 5 Machi, 2026 amefanya kikao na wadau wa Mahakama cha maandalizi ya uanzishaji
wa masjala ndogo ya Mahakama Kuu, Kanda ya Katavi na kuwapongeza wadau kwa
ushiriki wao kwa kuhakikisha masjala hiyo inaanza kuwatumikia wananchi.
Akizungumza
katika kikao, Mhe. Lushasi amesema, taarifa itatolewa kwa wananchi muda wowote ya
kuanza kupata huduma za Mahakama Kuu Mara tu itakapokuwa imetangazwa rasmi kwenye
Tangazo la Serikali.
Naibu
Msajili huyo amesema, Mahakama Kuu itakapoanza mkoani Katavi, mashauri yote
yaliyo sajiliwa Mahakama Kuu Sumbawanga yataendelea huko huko ila yale mapya
yatasikiliziwa masjala mpya ya Katavi na kuongeza kuwa, dira ya Mahakama ya
Tanzania ni kutoa haki kwa wakati na mapema kadri iwezekanavyo.
Aidha,
Mhe. Lushasi aliongeza kuwa, wadau waliopo kwenye mnyororo wa haki Jinai
inabidi kuendana na kasi ya Mahakama kidijitali kwa kuboresha na kuimarisha
miundombinu.
Mhe. Lushasi ameongeza kuwa, nguzo ya pili ya Mpango Mkakakati wa miaka
mitano wa Mahakama ya Tanzania inasisitiza utoaji haki kwa wakati. Mahakama ya
Tanzania inatekeleza mpango huo kwa kuboresha mazingira ya utoaji haki na
kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi kwa kujenga miundombinu
bora na wezeshi itakayochangia ufanisi mzuri wa utekelezaji wa nguzo hiyo.
Kwa
upande wake, Mwakilishi kutokea TANESCO Mhandisi Victor Ng’wigulu alisema, kwa sasa
Taasisi zote za umma ikiwemo Mahakama tumeziweka kwenye kipaumbele cha kwanza
katika kuhakikisha zinapata nishati ya umeme.
“Tuliwashauri
Mahakama ya Tanzania Mkoa wa Katavi wapate kangavuke (Standby Generator) na
nitumie nafasi hii kuwashukuru kwa kupata kangavuke zuri na la kisasa tumeliona
lipo, hivyo ikitokea changamoto za umeme wa TANESCO naamini shughuli za
kimahakama zitaendelea ila tumejipanga vizuri kama TANESCO Mkoa kuendelea kutoa
huduma bora kwa Taasisi zote.
Wadau
wa Mahakama waliohuduria kwenye kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi ni pamoja na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,
Takukuru, Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali Sumbawanga, Ofisi ya Magereza Katavi,
Chama cha wanasheria Tanganyika (TLS) Katavi, Baraza la Ardhi na Nyumba,
Hifadhi ya Taifa Katavi, Afisa Ustawi wa Jamaii Katavi, Mahakimu Wafawidhi,
Tanesco, Tume ya Usuluhishi na Upatanishi (CMA) Katavi, Ofisi ya Mganga Mkuu
Katavi, Mwanasheria wa Halmashauri za Mpanda, Mlele na Tanganyika.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Silivia S. Lushasi (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wadau wa Mahakama ya Tanzania mkoa wa Katavi mara baada ya kikao cha wadau wa Mahakama.
Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Katavi Bi. Flavia F. Shiyo akichangia hoja wakati wa Kikao cha Wadau wa Mahakama Katavi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni