Jumatatu, 30 Machi 2026

JAJI MFAWIDHI MAHAKAMA KUU MASJALA NDOGO SINGIDA AWASILI KITUONI

Na EVA LESHANGE, Mahakama-Singida

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Singida, Mhe. Ayoub Mwenda leo tarehe 30 Machi, 2026 amewasili mkoani Singida ikiwa ni mara ya kwanza baada ya kupata uteuzi huo hivi karibuni wa kuiongoza Kanda hiyo mpya ya Mahakama Kuu.

Akiwa katika hafla ya ukaribisho wake alipata nafasi ya kusikiliza taarifa fupi ya utekelezaji iliyosomwa na Afisa Utumishi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Bi. Eva James Leshange. 

Mara baada ya kupokea taarifa hiyo, Mhe. Mwenda amewapongeza Viongozi na watumishi wote wa Mahakama Mkoa wa Singida kwa kazi nzuri wanayoifanya hasa katika usikilizwaji wa mashauri kwani hadi kufikia tarehe 27 Machi, 2026 Mkoa wa Singida haukuwa na shauri la mlundikano.

Aidha, Jaji Mfawidhi huyo amewashukuru watumishi kwa mapokezi mazuri na kuona watumishi wana ari na nguvu ya kufanikisha malengo ya Mpango Mkakati wa Mahakama.

“Nawashukuru sana viongozi na watumishi kwa ujumla kwa mapokezi mazuri na hongereni sana kwa kufanya kazi kwa bidii na ushiriano mkubwa hususan katika usikilizwaji wa mashauri ni kiashiria watu wanafanya kazi kwa ushirikiano,” amesema.

Vilevile amewasisitiza watumishi kuendela kuwa na nidhamu kwani, Mahakama inapokea wateja ambao wameumizwa na wanahitaji msaada hivyo wasaidiwe kuhudumiwa kwa heshima, pia amesisitiza kufanya kazi katika timu pasipo kuangalia vyeo ili kusiwe na mkwamo katika kutekeleza majukumu ya kila siku.

Baada ya kuzungumza na watumishi alipata wasaa wa kwenda kutembelea jengo jipya la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Singida na kufanya ukaguzi wa vyumba vya ofisi na kuona hatua ilipofikiwa.

 

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Singida, Mhe. Ayoub Mwenda (wa kwanza kushoto) akisalimiana na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida alipowasili ofisini hapo leo tarehe 30 Machi, 2026.

Afisa Utumishi Mwandamizi Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Bi. Eva Leshange akiwasilisha taarifa ya utekelezaji majukumu mbele ya Mhe. Ayoub Mwenda, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda Ya Singida (hayupo katika picha) leo tarehe 30 Machi, 2026 alipowasili katika Mahakama hiyo.

Sehemu ya watumishi waliohudhuria hafla fupi ya ukaribisho wa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda mpya ya Singida.


Sehemu ya watumishi ajira mpya wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Singida, Mhe. Ayoub Mwenda (aliyeketi katikati) . Aliyeketi kushoto ni Naibu Msajili, Mhe. Evodia Kyaruzi na kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Singida, Bw. Filbert Matotay. 

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Singida, Mhe. Ayoub Mwenda akikagua jengo jipya la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Singida.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni