Jumatatu, 30 Machi 2026

MTENDAJI WA MAHAKAMA PWANI AWATAKA WATUMISHI WA KANDA YA DAR ES SALAAM KUITHAMINI MICHEZO

  • Asema michezo ni haki ya msingi kwa ustawi na ufanisi katika utendaji kazi
Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani

Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Bw. Nestory Mujunangoma amewataka watumishi wa Mahakama Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani kuifanya michezo kuwa haki kwa kila mtumishi.

Bw. Mujunangoma aliyasema hayo tarehe 28 Machi, 2026 wakati akifungua Bonanza lililofanyika katika viwanja vya Zimamoto Kibaha Mkoa wa Pwani. Bonanza hilo lililoandaliwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani ambalo liliwashirikisha watumishi wa Mahakama Mkoa wa Dar es Salaam ambao wanaunda Kanda ya Dar es Salaam.

Alisema kuwa, kushiriki katika michezo ni haki ya kila mtu na kwamba michezo ni furaha, inaleta umoja na mshikamano na ndio maana wako pamoja, hivyo ni amewasisitiza kuongeza bidii kushiriki katika michezo kwakuwa michezo ni haki yao. 

Aidha, akifafanua kauli hiyo alisema kila mtumishi wa Mahakama aione michezo kama haki yake na kwamba ana uhakika kama watashiriki kwa wingi na kwa umoja huo licha ya kuimarisha afya zao, furaha zao na mshikamano wao hata utendaji kazi wao utakuwa na ufanisi zaidi maana wakiwa na michezo akili zitakuwa vizuri.

“Kadhalika umoja utakuwepo mipango itapangika na watakuwa karibu na Viongozi wao na watakachokipanga kitaeleweka na kitafanyiwa kazi kinachotakiwa ni kupata ufanisi wa kazi katika Taasisi,” ameeleza Mtendaji huyo. 

Kadhalika aliwapongeza Viongozi wa Kitaifa wa Mahakama Sports Club kwa kujumuika katika Bonanza hilo na kusema kwamba, uwepo wa Viongozi wa michezo kitaifa inaonesha kuwa shughuli hiyo haitaishia hapo bali itakuwa endelevu.

Alisema pia, kwa Mkoa wa Pwani, imekuwa ni heshima kubwa kwa kufanya bonanza hilo na pia ameomba ushirikiano huo waliouonesha Dar es Salaam na Pwani uendelee.

Amewaomba Uongozi wa Kitaifa kushirikiana na Uongozi wa Pwani na Dar es Salaam kufanya kitu kikubwa zaidi na kitu kitakachofahamika zaidi na kuitangaza Mahakama kwa upana  mkubwa Zaidi. “Sasa tujiandae kutakapokuwa na Bonanza linalofuata  maana yake tuwe na timu nyingine za Taasisi nyingine kwa hiyo lazima tuwe na maandalizi makubwa zaidi,” alisema Bw. Mujunangoma.

Bonanza hilo lilihusisha mchezo wa mpira wa miguu ambapo mpaka dakika zote 90 walitoka kwa sare ya kufungana goli moja kwa moja na walipoenda kwenye matuta Pwani walipata penati sita wakati Dar es Salaam walipata penati saba hivyo Dar es Salaam kupata ushindi kwa upande wa mpira wa miguu.

Kwa upande wa Mpira wa Pete Pwani waliibuka kidedea kwa kuwafunga Dar es Salaam magoli 10 kwa nane, wakati mchezo wa kuvutana kwa kwamba wanaume na wanawake Dar es salaam waliibuka kidedea.

Mchezo wa riadha kwa wanaume Dar es Salaam wameibuka kidedea wakati upande wa wanawake Pwani wameibuka kidedea na mchezo wa kufukuza kuku wanawake na wanaume Dar es Salaam wamefanikiwa kuchukua kuku wote wawili.


Mgeni rasmi Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Bw. Nestor Mjunangoma  (aliyesimama) akizungumza wakati wa ufunguzi wa Bonanza tarehe 28 Machi, 2026 katika viwanja vya Zimamoto Kibaha Mkoa wa Pwani. Kulia ni Mwenyekiti wa Mahakama Sports Club, Mhe. Martin Mushi na kushoto ni Naibu Katibu, Mahakama Sports Club, Bi. Eva Mapunda.

 Mgeni rasmi Mtendaji wa Mahakama Pwani,  Bw. Nestory Mujunangoma  akikagua kikosi cha Mpira wa Miguu cha Pwani. Kushoto ni Nahodha wa Kikosi hicho ni Bw. Isihaka Mgude.

Mgeni rasmi Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Bw. Nestory Mujunangoma (mwenye kofia)  akikagua kikosi cha Mpira wa Miguu cha Dar es Salaam. Kulia kwake ni Nahodha wa Kikosi hicho, Abdi Sasamalo.

Washindi wa kukimbiza kuku, kulia ni Stanley Sirikwa na kushoto ni Bi. Patricia Patrick.

 Kikosi cha Kamba Wanaume Dar es Salaam wakijiandaa na pambano.

Vikosi vya Kamba Wanawake Pwani na Dar es Salaam wakisikiliza maelekezo kabla ya pambano.

Matukio katika picha Bonanza la Michezo lililoandaliwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni