Ijumaa, 20 Machi 2026

JAJI MFAWIDHI MOSHI AHAIDI KUKAMILISHA UANZISHWAJI WA MAHAKAMA YA MWANZO KWAKOA

Na PAUL PASCAL-Mahakama, Moshi

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Lillian Mongella, tarehe 18 Machi, 2026 alifanya ziara kwa ajili ya kuzungumza na Viongozi wa Serikali na Wananchi wa Kata ya Kwakoa juu ya ombi lao kuhusu kupatiwa huduma ya Mahakama katika eneo lao.

Katika ziara hiyo, Mhe. Dkt. Mongela aliambatana na Viongozi wa Mahakama Kuu Moshi na Mahakama ya Wilaya Mwanga, kufuti ombi la Wananchi hao kutoka Kijiji cha Ngulu kilichoko Kata ya Kwakoa, Wilayani Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro.

Kwenye ombi hilo waliloliwasilisha kwenye Ofisi ya Jaji Mfawidhi, wananchi walieleza hitaji la kupata huduma za kimahakama kutokana na adha wanayoipata kwa kufuata huduma hiyo umbali wa zaidi ya kilometa 40.

Akisoma taarifa fupi ya Kata ya Kwakoa, Diwani wa eneo hilo, ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata, Mhe. Kiende Mvungi, alieleza kuwa kwenye Kata nne zinazounda ukanda kwenye eneo lao hakuna hata moja yenye huduma ya kimahakama.

“Naomba nikufahamishe kuwa Kata yetu ya Kwakoa inaundwa na Vijiji viwili; Kijiji cha Kwakoa na Kijiji cha Ngulu. Ukanda huu umeundwa na Kata nne; Toroa, Kigonigoni, Jipe na Kwakoa na katika Kata zote, hakuna yenye Mahakama ya Mwanzo. Wananchi wote wa Kta hizi wanafuata huduma za kimahakama katika Mahakama ya Mwanzo Lembeni, ambayo iko zaidi ya kilometa 40 kutoka hapa,” alisema Mhe. Kiende.

Diwani huyo alibainisha kuwa katika kata yao wana Kituo cha Polisi, lakini mnyororo wa utoaji haki hauwezi kukamilika pasipo kuwepo kwa Mahakama ambayo ndiyo yenye jukumu la kutafsiri sheria za nchi na kwa kuliona hilo Serikali ya Kata ya Kwakoa ikawasilisha ombi la kuanzishwa Mahakama ya Mwanzo Kwakoa ili iweze kuhudumia Kata zote nne katika ukanda huo.

“Tumetenga eneo lenye ukubwa wa ekari nne kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Mahakama na makazi ya Watumishi kwa mpango wetu wa muda mfupi, tunaomba tuwakibidhi jengo la kuanzia kutoa huduma za kimahakama katika eneo hili, wakati michakato ya muda mrefu wa ujenzi ukiendelea ili nasi tupate huduma tuliyoikosa katika eneo letu tangu tulipopata uhuru,” lisema Mhe. Kiende.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi aliwashukuru Wananchi na Viongozi wa Kata ya Kwakoa kwa kutambua na kuwa na imani na Mahakama. Alipongeza juhudi katika kuhakikisha huduma zote muhimu zinapatikana ndani ya Kata pasipo kuzifuata mbali.

“Tumefurahishwa na jitihada zote mlizofanya ili muweze kupata huduma ya Mahakama katika eneo lenu, niwaahidi kwa juhudi hizi jambo lenu linakwenda kukamilika, tunakwenda kutekeleza matakwa ya kisheria ya uanzishaji wa Mahakama ya Mwanzo ndani ya miezi mitatu. Tutahakikisha michakato yote inakamilika na huduma za kimahakama katika Kata hii zinaanza,” alisema.

Katika ziara hiyo, Jaji Mongella aliambatana na Naibu Msajili Mahakama Kuu Moshi, Mhe. Sekela Mwaiseje, Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Moshi, Bi. Maria Itala na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Mwanga, Mhe. Marium Mfanga.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Lillian Mongella akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kufika katika Kata ya Kwakoa wilayani Mwanga.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Lillian Mongella akisalimiana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngulu, Kata ya Kwakoa, Bw. Said Mvungi mara baada yakuwasili katika ziara yake.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Lillian Mongella akizungumza na Wananchi wa Kata ya Kwakoa wilayani Mwanga (hawako pichani) wakati wa ziara yake.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Lillian Mongella akiongozana na Viongozi wa Serikali ya Kata ya Kwakoa kukagua jengo kwa ajili ya kutolea huduma za  Mahakama ya Mwanzo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Lillian Mongella (aliyesimama mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Kata ya kwakoa mbele ya jengo linalotazamiwa kutumika kutolea huduma za Mahakama ya Mwanzo.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni