Ijumaa, 20 Machi 2026

WAFUNGWA, MAHABUSU WAIPONGEZA MAHAKAMA MUSOMA

Na FRANCISCA SWAI - Mahakama Musoma

Wafungwa na Mahabusu katika Magereza tofauti ndani ya Mkoa wa Mara, wameipongeza Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Musoma, kwa namna inavyotoa huduma zake.

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa ukaguzi wa Magereza uliofanywa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya.

Katika ziara hiyo, Mhe. Mtulya alitembelea na kukagua Magereza ya Tabora B, Gereza Mugumu na Gereza Musoma. Aliambatana na Wadau wa Haki Jinai kwa ajili ya kusikiliza na kutatua changamoto.

Pamoja na pongezi hizo, Wafungwa na Mahabusu waliibua na kujibiwa changamoto zao mbalimbali, hasa wanazokutana nazo kutoka kwa Wadau kuhusiana na namna wanavyokamatwa, upelelezi unavyofanyika na uletaji wa mashahidi mahakamani.

Naye Mkuu wa Gereza la Musoma, Afande John Murya, alimshukuru Jaji Mtulya kwa namna Mahakama inavyowapa ushirikiano. Alieleza kuwa katika Gereza hilo wanaendelea na ujenzi wa jengo litakalotumika kwa ajli ya Mahakama Mtadao (Virtual Court).

Aidha, katika ukaguzi huo Mhe. Mtulya alitoa pongezi kwa Jeshi la Magereza kwa namna wanavyokaa na Wafungwa na Mahabusu hao na namna wanavyowasaidia kwa kuwapa elimu juu ya masuala mbalimbali ya kisheria na kijamii.

Zaidi aliwapongeza kwa ushirikiano wao katika matumizi ya Mahakama Mtandao ili kuhakikisha utoaji wa haki unafanywa kwa wakati kwakuwa jukumu la utoaji haki ni la pamoja kati ya Mahakama na Wadau wake wote.

Jaji Mfawidhi pia aliwaasa Wafungwa na Mahabusu hao pale watakapomaliza kutumkia adhabu zao, wakawe raia wema, wazingatie sheria na taratibu za nchi ili kuleta amani na ustawi kwa Taifa na familia zao.

 







Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (katikati) akiwa pamoja na Viongozi wa Mahakama Kuu Musoma; Naibu Msajili, Mhe. Monica Ndyekobora (wa pili kulia), Mtendaji wa Mahakama Musoma, Bw. Leonard Maufi (wa kwanza kushoto) na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Serengeti, Mhe. Jacob Ndira (wa kwanza kulia). Wengine katika picha ni Kaimu Mkuu wa Gereza, Afande Malele (wa pili kushoto), Watumishi wa Mahakama Serengeti na  Wadau wa Haki Jinai.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (mbele) akiwa anasisitiza jambo katika taarifa iliyosomwa kwake na Kaimu Mkuu wa Gereza la Wafungwa Tabora B, Afande Majuto Mabele (wa kwanza kulia kwa Mhe. Mtulya) pamoja na Viongozi, Wadau na Watumishi wa Mahakama.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (mbele) akiwa anafuatilia na kusisitiza taarifa iliyotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Monica Ndyekobora (aliyesimama), wakati wa kujadili changamoto za Wafungwa katika kikao chake na watumishi wa Mahakama Serengeti pamoja na Wadau wa Haki Jinai walipotembelea Gereza la Wafungwa Tabora B.

Jengo linaloendelea na ujenzi kwa ajili ya kutumiwa kwa shughuli za Mahakama Mtandao katika Gereza Musoma.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

 

  

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni