Ijumaa, 20 Machi 2026

WAFUNGWA, MAHABUSU GEREZA LA KIGONGONI WAIPONGEZA MAHAKAMA, WADAU HAKI JINAI KWA KUHARAKISHA MASHAURI

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Pwani

Wafungwa na Mahabusu wa Gereza la Kilimo la Kigongoni lililopo Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani wameipongeza Mahakama na Wadau wa Haki Jinai kwa kuondoa kero zao.

Waliyasema hayo tarehe 18 Machi, 2026 walipotembelewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi katika ziara yake ya ukaguzi katika gereza hilo.

Kabla ya kupokea pongezi hizo, Jaji Maghimbi alipata taarifa kutoka kwa Mkuu wa Gereza hilo, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Hassan Lidenge ambaye alisema kuwa, Gereza la Kilimo Kigongoni lilianzishwa miaka ya 1970 ambapo shughuli kubwa inayofanyika ni kilimo na hasa kilimo cha mpunga. 

Alisema, Gereza hilo lina uwezo wa kuhifadhi Wafungwa na Mahabusu (Authorized Accommodation Capacity) 198. Idadi ya wahalifu waliokuwepo tarehe 18 Machi 2026, Wafungwa Watanzania wanaume walikuwa 26, Waethiopia watano, Raia wa Burundi 28, Mahabusu wanaume nane na Mahabusu wanawake watatu, jumla ya wafungwa na mahabusu wanawake na wanaume 70 na hivyo kueleza kwamba, katika Gereza hilo hakuna msongamano.

Mkuu huyo wa Gereza, alisema sambamba na huduma za kuwapeleka wafungwa/mahabusu katika Mahakama mbalimbali,  agizo la matumizi ya Mahakama Mtandao limetekelezwa kwa kutengwa chumba chenye vifaa kwa ajili ya shughuli za Mahakama mtandao, na kueleza kuwa, “tayari kesi za kuahirishwa au kutajwa zimefanyika kwa kutumia huduma hiyo.”

Aidha Mrakibu huyo Mwandamizi, amekiri kupata ushirikiano kutoka ngazi zote za Mahakama kila wakati wanapohitaji msaada ambapo amesema, “naomba kutumia fursa hii, kutoa shukrani kwako binafsi Jaji Mfawidhi na timu uliyoambatana nao kwa kuweka ratiba ya kutembelea Gereza hili.”

Mkuu huyo ametoa pongezi kwa ngazi zote katika Mhimili wa Mahakama kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakitimiza majukumu yao kwa weledi na kuwa sio tu chachu katika utoaji haki kwa jamii lakini utendaji wao umekuwa ni sababu ya kuondoa hali ya msongamano magerezani.

Baada ya kupokea  taarifa ya Mkuu wa Gereza hilo,  Mhe Maghimbi alizipokea pongezi hizo na kuzielekeza kwa Wasaidizi wake Mahakimu Wakazi Wafawidhi na kusema mara nyingi amekuwa akipata bahati ya kufanya kazi na Wafawidhi wanawake ambapo amejifunza kwamba wamekuwa na maadili mema kusema kuwa, “hivyo najisikia vizuri zaidi na ikizingatiwa huu ni mwezi wa wanawake.”

Lakini pia Jaji Mfawidhi huyo aliongeza kuwa, hata sasa anafanya kazi vizuri na Naibu Msajili Mfawidhi wa kiume ambaye ni Mhe. Livin Lyakinana na Mtendaji wa Kanda ya Dar es Salaam ambaye ni mwanaume, Bw. Sumera Manoti.

Akisoma risala kwa niaba ya wafungwa na mahabusu, Mahabusu namba 274/2025 Kassian Pomoni alitoa pongezi za dhati kwa wadau wote wa utoaji wa haki na haki jinai wakiongozwa na Mahakama.

Aliongeza kwa kusema kwamba, hatua hiyo inatokana na ukweli usiopingika kuwa, changamoto nyingi zilizokuwa zinawakabili huko nyuma zimefanyiwa kazi na kupungua kama sio kumalizika kabisa.

Akiainisha pongezi hizo, alieleza kuwa, hapo awali mashahidi walikuwa hawaletwi kwa wakati hali iliyokuwa ikisababisha mashauri kukaa kwa muda mrefu na kusababisha msongamano  wa Mahabusu gerezani na kukiri kuwa, “kwa sasa changamoto hiyo haipo tena kwa vile mamlaka  husika zinajitahidi kuhakikisha  mashahidi wanaletwa kwa wakati.”

Akizungumzia kuhusu Jeshi la Polisi kupitia Idara ya Upelelezi, Mahabusu hao wamesema mashauri yanachukua muda mfupi mpaka kukamilika kwa upelelezi tofauti na ilivyokuwa huko nyuma na kwamba hatua hiyo inawezesha mashauri kuamriwa mapema na wahusika kujua hatima zao.

Kwa upande wa Jeshi la Magereza, amesema jitihada za kutosha zimekuwa zikifanyika ili kuhakikisha Mahabusu wanahudhuria mahakamani kwa tarehe zilizopangwa.

Mahabusu hao walimshukuru Mhe. Maghimbi pamoja na wote alioongozana nao kwenda kuwatembelea na kuwasikiliza japo hawana changamoto zaidi bali ni pongezi na kuwatakia majukumu mema ya kutimiza wajibu na majukumu yao kwa weledi.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi  akisalimiana na Askari Magereza alipowasili tarehe 18 Machi, 2026 katika ziara ya ukaguzi katika Gereza la Kilimo la Kigongoni lililopo wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Gereza la Kilimo la Kigongoni lililopo wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani. 
Viongozi waliombatana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam katika ziara ya ukaguzi. Kutoka kushoto ni Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Livin Lyakinana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi na  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bagamoyo, Mhe. Yasinta Kingwala.

 
Mkuu wa Gereza la Kilimo Kigongoni, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Hassan Lidenge (kulia) akisoma taarifa mbele ya Jaji Mfawidhi (hayupo katika picha). Katikati ni Mwanasheria wa Serikali Mwandamizi, Bi. Bonisia Mollel na kushoto ni Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bi.Maria Mwakatobe. 

Jaji  Mfawidhi na Timu ya Wadau wa Haki Jinai  aliyoambatana nayo katika ziara ya ukaguzi wakipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Gereza la Kilimo Kigongoni wakiwa kwenye chumba cha Mahakama mtandao (virtual court) wakati walipofanya ziara ya ukaguzi katika gereza hilo. 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu y Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (aliyeketi katikati). Kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Livin Lyakinana na kushoto ni Mkuu wa Gereza la Kigongoni Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Hassan Lidenge.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni