Jumanne, 17 Machi 2026

JAJI MKUU ASHIRIKI KUMBUKIZI MIAKA MITANO YA HAYATI DKT. JOHN POMBE MAGUFULI

  •   Asema Hayati Dkt. Magufuli alikuwa mnyenyekevu, mwenye huruma na mchapakazi

  • Apongeza Kanisa kwa kuhimiza usalama wa jamii, maadili ya jamii, amani katika jamii, umoja wa kitaifa na maslahi ya Taifa

Na MARY GWERA, Mahakama-Chato

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju, Viongozi wengine wa Serikali, Wanafamilia na Watanzania kwa ujumla leo tarehe 17 Machi, 2026 kwa pamoja wameungana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kuadhimisha miaka mitano ya Kumbukizi ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  

Katika Kumbukizi hiyo, Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Nchimbi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan huku Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa Mgeni Maalum.

Ibada Maalum ya Kumbukizi ya miaka mitano ya Kifo cha Hayati Dkt. Magufuli imefanyika katika Viwanja vya JS Chato vilivyopo katika Kijiji cha Kilimani mkoani Geita.

Aidha, shughuli za Maadhimisho hayo zilianza majira ya saa 3:30 Asubuhi kwa Adhimisho la Ibada Takatifu iliyoongozwa na Maaskofu mbalimbali wakiongozwa na Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara.

Mara baada ya ibada kukamilika, Viongozi mbalimbali walipata wasaa wa kutoa neno miongoni mwao akiwemo Jaji Mkuu, Mhe. Masaju ambaye ameishukuru familia ya Hayati Magufuli kwa mwaliko wa kushiriki katika Kumbukizi hiyo.

“Nashukuru Mama Janeth kwa ukarimu wako na kutualika, hii ni fursa ambayo inatukutanisha, lakini yatosha tu kusema kwamba nikushukuru Mhashamu Baba Askofu kwa ibada kubwa hii na muhimu uliyoifanya, ninawashukuru Kanisa kwa kuendelea kuhimiza usalama wa jamii, maadili ya jamii, amani katika jamii, umoja wa kitaifa na maslahi ya Taifa,” amesema Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu ameeleza kuwa, alimfahamu Hayati Magufuli wakati akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alipokuja kusoma Shahada ya Pili wakati yeye (Mhe. Masaju) akiwa anasoma Shahada ya kwanza.

Aidha, Mhe. Masaju amesema kuwa, baadaye mwaka 2015, Hayati Magufuli alimteua kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mara baada ya kuwa ametumika kama Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa uteuzi wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Jaji Mkuu ameongeza kuwa, alifanya kazi na Hayati Dkt. Magufuli kwa miaka miwili katika nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na baadaye alimteua kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na hatimaye Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akamteua kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania Juni, 2025.

“Ninawashukuru sana Viongozi hawa, Rais Kikwete, Rais Magufuli, Rais Samia, Rais Mwinyi ‘Senior’ na Rais Mkapa wana mchango mkubwa sana katika utumishi wangu,” ameeleza Mhe. Masaju.

Kadhalika, Jaji Mkuu amebainisha kuwa, Hayati Magufuli alikuwa na huruma, mnyenyekevu na mchapakazi.

“Hayati Magufuli alikuwa mchapakazi na uchapakazi ule ndio maana tunayashuhudia haya aliyoyafanya na ambaye mrithi wake ambaye mimi naamini ilikuwa timu nzuri ameyakamilisha na mengine ameendelea kuyaibua na kuyafanya. Huu ni utaratibu mzuri kwa Taifa letu,” amesisitiza Mhe. Masaju.

Jaji Mkuu alitumia nafasi hiyo pia kuitakia heri familia ya Hayati Magufuli kuendelea kwa kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu kuwabariki katika maisha yao, katika utumishi wao na katika shughuli zao.

“Tunajua hili ni pengo, Mwanadamu yeyote anapofariki anaacha pengo kubwa ambalo halizibiki lakini pia linaloumiza kwa sababu pia kila mwanadamu ana utambulisho wake, faraja yangu mimi kwenu ni kwamba Mungu yupo pamoja na ninyi,” amesema Mhe. Masaju huku akimsihi Mama Janeth Magufuli kuendelea kuwa imara katika kuisimamia familia huku akimtanguliza Mungu.  

Viongozi mbalimbali waliopata nafasi ya kuzungumza wakiongozwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Nchimbi wamemuelezea Hayati Magufuli kwa mema aliyoyafanya enzi za uhai wake na kutoa rai kwa Watanzania kuyaenzi yote mema aliyoyafanya.

Wakati wa kumbukizi hiyo, Makamu wa Rais ameendesha Harambee maalum ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Parokia ya Mlimani-Chato ambayo ilikuwa ndoto ya Hayati Magufuli ambapo imepatikana Ahadi za jumla ya Shilingi 474,000,000/=.

Shughuli ya Kumbukizi imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Mawaziri, Viongozi Waastafu, Wanafamilia na Wananchi kwa ujumla.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju akitoa neno wakati wa Kumbukizi ya miaka mitano ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo tarehe 17 Machi, 2026 katika Viwanja vya JS Chato vilivyopo katika Kijiji cha Kilimani mkoani Geita.



Meza Kuu ikiongozwa na Mgeni Rasmi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi (katikati) aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wengine wa Serikali wakiwa katika Maadhimisho ya Kumbukizi ya miaka mitano ya Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Viongozi wa dini wakiingia tayari kwa ajili ya kuendesha Ibada maalum ya Kumbukizi ya miaka mitano ya Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 17 Machi, 2026 katika maadhimisho ya Kumbukizi ya miaka mitano ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Picha za makundi mbalimbali ya Viongozi wa Serikali, wa Dini, Wanafamilia pamoja na Wananchi kwa ujumla wakiwa katika Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka Mitano ya Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maadhimisho hayo yamefanyika leo tarehe 17 Machi, 2026 katika Viwanja vya JS Chato vilivyopo katika Kijiji cha Kilimani mkoani Geita.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Griffin Mwakapeje wakiwa katika Kumbukizi ya miaka mitano ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiweka shada la ua katika kaburi la Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa ni ishara ya kumkumbuka na kumuenzi.  Kulia kwa Jaji Mkuu ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi na baadhi ya Viongozi wengine.


(Picha na Jeremia Lubango, Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni