Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Lushoto
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti
wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Mhe. Dkt. Mustapher Siyani amesema
maadili, uwazi na uwajibikaji ni mambo ya muhimu yatakayoimarisha imani ya Umma
kwa Mhimili wa Mahakama.
Akifungua Mafunzo ya siku mbili ya Wajumbe wa Kamati ya
Maadili ya Maafisa Mahakama leo tarehe 16 Machi, 2026 katika Wilaya ya Lushoto Mkoa
wa Tanga, Jaji Kiongozi amesema miongoni mwa mambo ya kipaumbele kwa Mahakama
ni kuhakikisha inaendelea kujenga na kuimarisha imani ya umma kwa muhimili huo wenye
kauli ya mwisho katika utoaji wa haki nchini.
Alisema lengo kubwa la juhudi za Mahakama katika kuimarisha imani ya umma
ni kuifanya Mahakama kuwa Taasisi ya watu na inayowajibika kwa umma (Citizen
Centric Judiciary).
“Imani ndio mtaji wa taasisi yoyote inayotoa haki. Ili
kuwa na Mahakama inayoaminiwa na umma, masuala ya maadili, uwazi na uwajibikaji
ni ya muhimu na hayawezi kuwekwa kando. Kwa ujumla wake, watumishi wa Mahakama,
wanayo dhima ya kwanza ya kuwa waadilifu”, alisema Jaji Kiongozi.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa imani ya watumiaji wa huduma
za Mahakama haijengwi kwa uamuzi wa haki peke yake bali pia kwa tabia nzuri na mwenendo
usiotiliwa shaka wa watumishi wa Mahakama wakiwemo Majaji na Mahakimu.
Alisema matarajio ya umma kwa Maafisa
Mahakama (Majaji na Mahakimu) ni kuona kuwa wao swanakuwa ni mfano au tafsiri sahihi ya uadilifu, weledi na
uwajibikaji.
“Vitu hivi vitatu, vinajenga kwa pamoja dhana nzima ya
maadili. Kwa hiyo, ni muhimu Maafisa Mahakama kuwa na kiwango cha juu cha
uadilifu kwani huo ndio mtaji wa imani yetu kwa umma”, alisisitiza.
Alisema ili kulinda na kuimarisha maadili kwa Maafisa
Mahakama, Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama haina budi kusimamia na
kufuatilia mienendo na tabia za Maafisa hao na pia kuchunguza kwa umakini na
weledi wa hali ya juu wao wa utoaji wa uamuzi.
Aliwataka wajumbe hao kujifunza na kuelewa mambo ya
msingi ya kazi yao ili waweze kusimamia kikamilifu nidhamu na maadili ya
Maafisa Mahakama. Aliongeza kuwa mafanikio yao yatategemea weledi na ufanisi
katika uzingatiaji wa taratibu za kupokea malalamiko, kuchunguza tuhuma,
kusikiliza na kutoa uamuzi.
Alisema kuwa mafunzo haya ni muhimu kwa wajumbe wa
Kamati, kwani yatawajengea uwezo katika utekelezaji wa majukumu yao, na hivyo
kuboresha utendaji kazi wa Kamati.
Alisisitiza kuwa jukumu la Kamati ya Maadili ya Maafisa
Mahakama si kutoa adhabu pekee, Kamati hii inapaswa pia kuwa, kichocheo cha
uadilifu na uwazi ili kuimarisha imani ya umma kwa Mahakama.
Aidha, Jaji Kiongozi ameipongeza Tume ya Utumishi wa
Mahakama kwa kuona umuhimu wa kufanyika kwa mafunzo haya na kutaka yawe endelevu
na kujumuisha watumishi wote.
Tume ya Utumishi wa Mahakama imeandaa mafunzo ya siku
mbili ya Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuwajengea uwezo
wajumbe hao na kuimarisha utendaji kazi wa Kamati hiyo.
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (kulia) pamoja na Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa kwenye Mafunzo ya Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama jana tarehe 16 Machi, 2026.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Mhe. Dkt. Mustapher Siyani akiwa na Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama (waliosimama) mara baada ya kufungua Mafunzo yao jana wilayani Lushoto. Aliyekaa kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga Mhe. Katarina Mteule na kushoto ni Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Mbuya.
Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Mbuya akizungumza Neno la Utangulizi wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama jana tarehe 16 Machi, 2026 wilayani
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni