Jumatatu, 16 Machi 2026

WANAFUNZI BULONGE KIGOMA WAJIFUNZA MCHANGO WA MAHAKAMA KATIKA KUKUZA SIASA, UTAWALA WA SHERIA

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma 

Wanafunzi wapatao 19 wa kidato cha sita kutoka Shule ya Sekondari Bulonge mkoani Kigoma wametembelea Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma ili kupata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali ya kisheria, mchango wa Mahakama katika kukuza siasa na Utawala wa Sheria nchini.

Akitoa elimu kuhusu namna Mahakama nchini inavyofanya kazi tarehe 13 Machi, 2026 kwenye ukumbi Mahakama ya wazi wa Mahakama Kuu Kigoma, Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola aliwaeleza wanafunzi hao kuhusu majukumu ya Mahakama katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na namna Mhimili huo unavyoshiriki kutoa haki katika mashauri mbalimbali ya uchaguzi na kutoa haki na amri mbalimbali zinazolinda na kuleta amani na ustawi wa Nchi. 

Aidha, wanafunzi hao walisisitizwa kufuatilia hotuba mbalimbali za Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju, hususani ya tarehe 31 Julai, 2025 jijini Dodoma wakati akitoa salamu kwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliokuwa wakishiriki katika Mafunzo ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi yaliyofanyika kwa njia ya Mahakama Mtandao (Virtual Court).

Kadhalika, Mhe. Msola aliwafundisha ni kwa jinsi gani Mahakama inatoa fursa kwa mgombea wa chama chochote ambaye hajaridhika na matokeo ya uchaguzi kuja Mahakama ya Wilaya husika kufungua shauri katika ngazi fulani ya uchaguzi, hata hivyo  anaweza kukata rufaa kwenda Mahakama Kuu au  ya Mahakama ya Rufani asiporidhishwa na hukumu ya Mahakama ya chini. 

Alisema kuwa, kwa Mahakama za Mwanzo zote, rufaa zake hupelekwa Mahakama za Wilaya na Mahakama za Wilaya rufaa zake hupelekwa Mahakama Kuu ya Tanzania na vilevile Mahakama Kuu rufaa zake huwasilishwa Mahakama ya Rufani ili kutoa haki iliyokosekana kutolewa kwa Mahakama za chini. 

“Kupitia mlolongo huo, mwananchi/wanasiasa wanayo fursa kubwa ya kutafuta haki aliyonyimwa na Tume ya Uchaguzi, kwa namna hiyo Mahakama inashiriki kikamilifu katika kukuza siasa na haki nchini,” alisisitiza Mhe. Msola. 

Aidha, aliwaasa wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kujituma huku wakikua katika maadili ya kuwa viongozi wasomi katika kada mbalimbali wanazopenda kusomea. 

Hata hivyo, aliwakaribisha katika tasnia ya sheria kwani ni miongoni mwa tasnia mahsusi katika kulinda na kutetea haki za kisiasa na masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi, na kuwasisitiza kusoma na kufaulu vizuri ili kuweza kupata fursa ya kufika elimu ya juu katika masomo yao ili kuja kuwa viongozi wenye tija kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza juu ya nia yao ya kujifunza kupitia Kazi Mradi (School Project), Kiongozi wa Wanafunzi hao, Bw. Sefu Hamis alibainisha kiu waliyokuwa nayo kujifunza masuala ya kisheria hususani sheria za siasa  ambapo alisema, “tunapenda kufahamu mchango wa Mahakama kukuza siasa na taratibu za kusikiliza mashauri hayo ili kulinda haki za wanasiasa.” 

Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola akisisitiza jambo fulani alipokuwa akitoa elimu kwa wanafunzi wa kidato cha sita Shule ya Sekondari Bulonge juu ya utaratibu wa usikilizwaji wa mashauri ya uchaguzi.

Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola akifundisha kwa vitendo wanafunzi wa kidato cha Sita Shule ya Sekondari Buronge namna ambavyo Mahakama huketi kusikiliza mashauri mbalimbali ikiwemo ya uchaguzi.

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Bulonge  Kidato cha Sita, Bi. Elizabeth Elifasi akisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 107 inayoainisha uanzishwaji wa Mahakama ya Tanzania wakati wakipatiwa elimu na Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola (hayupo katika picha).

Wanafunzi wapatao 19 wa Kidato cha Sita kutoka Shule ya Sekondari Bulonge wakisikiliza kwa makini mtoa elimu  Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola alipokuwa akitoa mada wakati walipotembelea Mahakama Kuu Kigoma.

Picha ya pamoja ya Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na  Wanafunzi wapatao 19 wa kidato cha sita Shule ya Sekondari Bulonge mara baada ya kupatiwa elimu.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Mwanza)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni