Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe.
Salma Maghimbi ametoa wito kwa viongozi wanawake ngazi mbalimbali kuwa walezi
na walimu kwa kuwaongoza wanawake wenye nia na bidii katika kuleta maendeleo
kwa taasisi na taifa kupitia majukumu ya kazi wanazozifanya.
Mhe. Maghimbi alitoa wito huo tarehe 13 Machi 2026 wakati wa kutaniko la wanawake watumishi wa Mahakama wa Dar es Salaam lililofanyika kwenye ukumbi wa PSSSF Golden Jubilee Tower.
Alieleza kuwa, chanzo cha Maadhimisho ya Siku ya Wanamke Duniani yalianza 1911 ambapo lengo lilikuwa ni kuikumbusha jamii kuhusu nafasi, haki na mchango wa mwanamke katika maendeleo ya jamii, ambapo alisema, “katika maadhimisho haya wanawake wamekuwa wakikutana kufanya majadiliano ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto wanazokabiliana nazo pamoja na kuelimishana kuhusu namna bora ya kujikomboa kiuchumi.”
Aidha, Jaji Mfawidhi huyo alisema anayo furaha kushiriki maadhimisho ya
siku hiyo muhimu ambapo imebebwa na Kauli mbiu isemayo, ‘Haki na usawa
kwa wanawake na wasichana; msingi jumuishi kufikia Dira 2050.’
Alisema kuwa, kaulimbiu hiyo inawakumbusha kwamba wanawake na wasichana wanalo jukumu la kujifunza zaidi katika maeneo wanayofanyia kazi kama vile sheria, TEHAMA, utawala na kadhalika ili waweze kuongeza ujuzi wao na hatimaye kuongeza tija na ufanisi katika kutenda haki kwenye majukumu yao ya kila siku wanayofanya.
Ameeleza kuwa, takwimu zinaonesha Mahakama ya Tanzania ina jumla ya watumishi 6,959 ambapo wanaume ni 3,549 na wanawake 3,410 sawa na asilimia 49, hiyo inaonesha kwamba dhana ya haki na usawa inatekelezwa kwa kiwango kikubwa ndani ya Mahakama ya Tanzania.
Aliongeza kwamba, mwaka 1979 Mahakama ya Rufani Tanzania ilikuwa na Majaji watano wote wanaume lakini kwa sasa Mahakama ya Rufani ina Majaji 37 ambapo wanaume ni 25 na wanawake ni 12 sawa na asilimia 32. Mahakama Kuu ina jumla ya Majaji 104 ambapo wanaume ni 65 na wanawake ni 39 sawa na asilimia 37, kwa upande wa Wasajili, Msajili Mkuu ni mmoja na ni mwanamke, Naibu Wasajili wapo 82 ambapo wanaume ni 40 na wanawake ni 42 sawa na asilimia 51.
Kwa upande wa Watendaji wa Mahakama, jumla wapo 40 ambapo wanaume wapo
28 na wanawake 12 sawa na asilimia 30, pia idadi ya Mahakimu wa Mahakama za
Hakimu Mkazi, Wilaya na Mwanzo ni 1,623 ambapo
wanaume ni 857 na wanawake ni 766 sawa na asilimia 47.
Mhe. Maghimbi alisema katika Mahakama za Wilaya 12 za Kanda ya Dar es Salaam, Mahakimu Wafawidhi 12 kati yao 11 ni wanawake ambapo ameeleza kwamba hiyo ni hatua kubwa wanayojivunia kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kadhalika, Jaji Mfawidhi huyo amewakumbusha wanawake na wasichana hao kuwa, mwanamke anayo nguvu ya asili katika malezi na uongozi kwa jamii na Taifa kwa ujumla, hivyo wanapotekeleza majukumu yao ya ofisi wakumbuke pia wana wajibu katika jamii ikiwemo malezi ya familia zao kama Mama, Dada, Shangazi na kadhalika kwa kufanya hivyo itasaidia kuwa na Taifa lenye maendeleo jumuishi ifikapo 2050.
Mhe. Maghimbi alitoa wito kwa wanawake na wasichana kuwa na moyo wa kujituma na kujiendeleza kitaaluma, ambapo ujuzi watakaoupata utawasaidia kuongeza maarifa kazini na kwa mazingira yanayowazunguka kwa ujumla katika hatua ya kuelekea kuweka msingi jumuishi kwa maendeleo kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Katika hatua nyingine, Jaji Maghimbi alitoa wito kwa Majaji Wafawidhi kuanzisha programu ya kuwafundisha watumishi wanawake katika vituo vyao kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050 ili waielewe.
Kadhalika Jaji Mfawidhi huyo ametoa rai kwa Menejimenti ya Mahakama ya
Tanzania kuendelea kuwapa ushirikiano, kuwaamini na kuwapa fursa nyingi za kazi
ikiwemo nafasi za utoaji haki kwa jamii.
Hafla hiyo ilipambwa na mdahalo ulioongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kituo Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma na wachangia mada walitoka katika kada mbalimbali tofauti na kada ya sheria kutoka Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara na Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia- Temeke.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na watumishi wanawake wa Kanda ya Dar es Salaam kutoka Mahakama Kuu Divisheni zote na Mahakama za chini.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wanawake kutoka Mahakama Kuu Divisheni
ya Ardhi.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wanawake wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke.
Meza Kuu wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wanawake kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Meza kuu katika picha ya pamoja na watumishi wanawake kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam-Kisutu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Zahra Maruma (kushoto) akiongoza mdahalo katika hafla hiyo. Anayefuata ni Bi. Joyce Ndosi kutoka Mahakama ya Biashara, Bi. Christina Nchimbi kutoka Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Bi. Bernadina Tayali kutoka Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia- Temeke na Bi. Anitha Kabwogi kutoka Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Mwanza)









Hakuna maoni:
Chapisha Maoni