Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile
amewataka Mahakimu Wakazi wapya wa Mahakama za Mwanzo kuzingatia utu, uadilifu
na tabia njema katika kutimiza majukumu yao ya uhakimu huku wakimtanguliza
Mungu mbele katika kuenenda vema.
Mhe. Rwizile
alitoa wito huo tarehe 13 Marchi, 2026 mara baada ya kuwapokea Mahakimu Wakazi
wapya wanne wa Mahakama za Mwanzo wakati wa mazungumzo yaliyofanyika katika
ofisi yake.
“Ninyi ambao
mmepangiwa kufanya kazi Kanda hii mmependelewa sana kwakuwa Kigoma tunafanya
tofauti hivyo dhamana ya utoaji haki ni jukumu zito linalohitaji nidhamu,
uaminifu, weledi na tabia njema ya kiwango cha juu na tunaamini kazi hiyo ni
adilifu na wito kwenu na ndio matarajio ya jamii, kwani kazi ya uhakimu ni tofauti
na kazi zingine,” alisisitiza Jaji Rwizile.
Katika hatua
nyingine, Jaji Mfawidhi huyo, alimshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George
Masaju kwa kuongeza nguvukazi na kuwafunda kwa
kiasi cha kutosha Mahakimu hao wapya.
Mhe. Rwizile
amewasisitiza Mahakimu hao kuyaishi maelekezo aliyoyatoa Jaji Mkuu tarehe 23
Februari, 2026 mara baada ya kuwaapisha.
Kadhalika
Jaji Mfawidhi huyo, amewataka Mahakimu hao kutofungwa na masharti ya kiufundi,
kelele za mamlaka au maneno ya
mitandaoni, msukumo wa kihisia, upendeleo wa wazi na kutoa hukumu bila
kuzingatia haki itadhoofisha utendaji kazi wao huku akiwasisitiza kwamba wana
wajibu wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kujiamini.
Sambamba na
hayo, Mhe. Rwizile amewaasa Mahakimu hao kutumia vizuri muda wao kusoma na
kuongeza ujuzi, weledi juu ya kazi yao, huku wakifanya tafiti mbalimbali kabla
ya kufanya maamuzi katika kazi zao.
Naye, Jaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi, amewapongeza Mahakimu
hao kupata kazi na amewasisitiza kuhusu umuhimu wa kuwa waadilifu pamoja na kuwa na uwezo wa
kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kwakuwa, wananchi wanatarajia kuona
mashauri yakisikilizwa na kuamuliwa mapema ipasavyo bila ucheleweshaji usio wa
lazima huku akiweka wazi kuwa kuchelewa kwa haki kunaweza kuathiri imani ya
wananchi kwa Mahakama na kusababisha mlundikano wa kesi mahakamani.
kwa upande
wake Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza
amewataka Mahakimu hao kujenga umoja na mshikamano katika maeneo yao ya kazi na
kuwahimiza kujifunza kwa watumishi watakaowakuta katika maeneo watakayopangiwa
kazi, huku akisisitiza kuwa wajifunze kutoka Kanda mbalimbali kwakuwa nguvu ya
Mahakama ipo katika ushirikiano, uwajibikaji na kufanya kazi kwa kuzingatia
sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Ameongeza
kuwa, kila Hakimu anapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika jamii kwa matendo na
maamuzi mbalimbali, huku wakitumia maarifa na uzoefu wao katika kuchambua
masuala na kutoa maamuzi sahihi kwa kuzingatia sheria kwakuwa kazi ya uhakimu
ni wito.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa, Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Festo Sanga ambao wote kwa nyakati tofauti wamewasisitiza Mahakimu hao kujifunza kwa haraka matumizi ya mifumo ya Mahakama ili kwenda na kasi ya Mahakama katika Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akisisitiza jambo alipokuwa
akifanya mazungumzo na Mahakimu Wakazi wapya wanne wa Mahakama za Mwanzo. Mazungumzo hayo yalifanyika katika ofisi yake ya Mahakama Kuu Kigoma.
Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Mwanzo wapya wanne wakisikiliza kwa makini maelekezo mbalimbali waliyokuwa wakitoa Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma wakati wa mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Kigoma, Mhe. John Nkwabi akisisitiza jambo wakati akitoa nasaha kwa Mahakimu
Wakazi wapya wanne wa Mahakama ya Mwanzo waliopangiwa mkoani Kigoma.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza akizungumza jambo na Mahakimu Wakazi wapya wanne wa Mahakama ya Mwanzo.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa (kulia) akifanya utambulisho wa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wapya wanne mbele ya Majaji. Kushoto ni Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Festo Sanga.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Mwanza)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni