Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Kibaha
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi amesema Vikao vya Kusukuma Mashauri vinaleta tija katika umalizaji wa mashauri,hayo.
Mhe.
Mkhoi aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akiongoza kikao cha robo ya kwanza
cha Kusuma Mashauri katika Mkoa wa Pwani kilichohudhuriwa na Wadau wa Haki
jinai na Haki Madai.
Katika
kikao hicho, Mhe. Mkhoi alisema maazimio yanayofikiwa yanafanyiwa kazi kwa
wakati na ndio maana malengo yanatimia ya kumaliza mashauri kwa wakati
uliokubaliwa kwenye vikao.
Aidha,
Mfawidhi huyo ametoa mbinu mbadala ya kupatikana kwa mashahidi kuwa, ni
kuharakisha kuwaita waathirika kwanza kutoa ushahidi akiwa bado ana uchungu wa
kufanyiwa tukio, kwa kuwa upelelezi unakuwa umekamilika wakati shauri
linafikishwa mahakamani siku ya kusomewa shtaka mtuhumiwa asomewe na maelezo ya
awali ili tarehe inayofuata mashahidi waitwe na shahidi wa kwanza awe mwathirika
wa tukio.
“Mbinu
hii imetokana na maelezo ya Mwakilishi wa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Pwani, Mkaguzi
wa Polisi Erick Lubuva kusema kwamba mashahidi wamekuwa wagumu kuifika Mahakama
kutokana na ndugu wa watuhumiwa kuwatafuta na kuongea nao na kukubaliana
kuwalipa hivyo wanakataa kufika mahakamani mpaka wengine wanapeleka hati za
kukatwa na hata wakifika hawatoi ushirikiano,” alisema Mhe. Mkhoi.
Sambamba
na kikao hicho ilifanyika ziara katika Gereza la Mahabusu Mkuza ambapo Wadau wa
Haki Jinai walifika kusikiliza kero zinazowakabili mahabusu hao. Kabla ya kuzungumza
na mahabusu hao, Mkuu wa Gereza la Mahabusu Mkuza, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza
(SSP) Ibrahim Nyamka alitoa taarifa ya Mahabusu na wafungwa waliomo ndani ya
gereza hilo ambapo alisema kwa sasa wana idadi ya Wafungwa ambao ni Watanzania 44,
wafungwa ambao ni Raia wa Burundi watatu (03),mfungwa mmoja Raia wa Uganda, Mahabusu
ambao ni Watanzania 51, Mahabusu wawili Raia wa China na Mzuiwa mmoja Raia wa Ethiopia
na kufanya jumla yao kuwa 102 na kwamba Gereza hilo kwa sasa halina msongamano.
Akijibu hoja ya mahabusu kuhusu changamoto ya
watuhumiwa kuachiwa na Mahakama na kukamatwa tena katika maeneo ya Mahakama,
Mkuu wa Mashtaka Mfawidhi wa Mkoa wa Pwani, Bi. Fajara George alisema kuwa, ameshafanyia
kazi suala hilo la kukamatwa na kuachiwa siku hizi limepunguzwa kwa kiasi
kikubwa na kama ikitokea mtu kaachiwa na kukamatwa ni pale tu panapokuwa na
ulazima na anaendelea kushughulikia hoja hiyo ili kupunguza msongamano wa kuwa
na mashauri yasiyo na ulazima kwani kuachiwa pia ni haki ya Mshtakiwa.
Katika
kikao kilichopita cha tarehe 10 Oktoba, 2025 maazimio yalikuwa ni kumaliza
mashauri matatu yalikuwa yamepita muda wake na katika hayo mashauri mawili
yalimalizika, limebaki moja ambapo wameweka maazimio kufikia mwezi Juni liwe
limemalizika na hivyo kufanikiwa kwa asilimia 80.
Katika ziara hiyo, Wadau wa haki jinai walitembelea pia jengo litakalotumika kama Mahakama matandao ambapo jengo hilo limefika hatua za mwisho kukamilika.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe Joyce Mkhoi (kulia) ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao cha kusukuma mashauri akiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Bi. Anna Chimpaye ambaye alikuwa Katibu wa kikao hicho wakiwa katika kikao cha Kusukuma Mashauri kilichofanyika hivi karibuni.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi (kushoto) akiwa na Mkuu wa Gereza la Mahabusu Mkuza, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza, Ibrahim Nyamka (katikati) na Hakimu Mkazi, Mhe. Fredrick Shayo
walipokuwa wakikagua jengo litakalotumika kwa shughuli za Mahakama Mtandao.
.jpg)
.jpg)
.jpg)

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni