Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda
ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano ametoa rai kwa watumishi wa Kanda hiyo kutumia
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na kuachana na matumizi ya kutumia
karatasi pamoja katika shughuli za uendeshaji wa ofisi hasa katika kusikiliza
mashauri Mahakamani
Mhe. Luambano aliyasema hayo tarehe 13
Machi, 2026 katika kikao alichofanya na watumishi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Njombe na Mahakama
za Wilaya za Mkoa Njombe ikiwemo Ludewa, Makete, Wanging’ombe na Mahakama za Mwanzo
kwa njia ya mkutano mtandao ‘Video Conference.’
Akiwa katika kikao hicho, Naibu Msajili
huyo alianza kwa kujitambulisha na kusema kuwa, kwa sasa Mkoa wa Njombe umeshakuwa
Kanda ya Njombe kufuatia kuanzishwa Mahakama kuu inayotarajiwa kuanza
kutoa huduma kwa wananchi hivi karibuni.
Mhe. Luambano aliwasihi Mahakimu wa
Mkoa wa Njombe, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo kwa kusema kwamba, “majalada
ya kesi katika usikilizwaji wa mashauri wanapokuwa mahakamani badala yake kila
hakimu anatakiwa kuwa na kompyuta mpakato (laptop) na wakati wa kusikiliza
mashauri vielelezo vinavyotolewa na kupokelewa mahakamani vinatakiwa viwe
nakala laini na kuhifadhiwa kwenye mfumo wa uendeshaji wa mashauri kuanzia
ngazi ya Mahakama za Wilaya pamoja na
kwenye kompyuta mpakato kwa ngazi ya Mahakama za Mwanzo.”
Aliongeza kuwaeleza watumishi hao huku akitoa mfano wa Masjala ndogo ya Mahakama Kuu Kanda ya Geita ambapo wamepunguza matumizi ya kutumia karatasi na kuwataka watumishi kujifunza kupitia Kanda hiyo na kuwasisitiza kutomuangusha hasa Mahakimu wa Ngazi zote pamoja na watumishi wengine na kwamba maana ya Masjala katika Kanda siyo tu Mahakama Kuu bali ni kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama Kuu.
Kadhalika katika kikao hicho, Naibu Msajili huyo ameomba ushirikiano kutoka kwa watumishi wa ngazi zote katika kuanzisha Masjala hiyo.
Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya
Njombe, Bw. Richard Mbambe alisisitiza kwamba kutotumia karatasi siyo tu kwa Mahakimu
bali watumishi wote wa Kada mbalimbali waweze kutumia nakala laini katika
utekelezaji wa majukumu yao na hasa katika matumizi ya barua pepe za ofisi ili kupunguza
matumizi ya karatasi pamoja na bajeti inayotengwa kwa ajili ya kununulia
karatasi na biki
Wakati wa kuhitimisha kikao hicho, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe. Liadi Chamshama alimshukuru Mhe. Luambano kwa ujio wake pamoja na kutoa msisitizo wa kuanza kwa utekelezaji huo wa kutotumia karatasi wakati wanaposikiliza mashauri Mahakamani huku naye akiwa kama msimamizi kwa Mahakimu walio chini yake na watumishi wengine aliwasisitiza kutomwangusha Naibu Msajili huo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mhe. Luambano amepangwa Masjala ndaogo mpya ya Mahakama Kuu Kanda ya Njombe ambapo Mahakama za Mkoa wa Njombe zilikuwa chini ya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano akizungumza na watumishi (hawapo katika picha) wa Mahakama za Mkoa wa Njombe tarehe 16 Machi, 2026.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano (aliyeketi katikati) akizungumza na
watumishi (hawapo katika picha). Kulia
ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe, Mhe.Liadi Chamshama na kushoto
ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya
Njombe, Bw. Richard Mbambe.
Kikao cha watumishi wa Mahakama za Mkoa wa Njombe kikiendeshwa kwa njia ya Mkutano Mtandao ambapo watumishi wa Mahakama za Wilaya Makete, Ludewa na Wanging’ombe wakimsikiliza Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano kwa umakini kwa njia ya video.
Watumishi wa Mahakama Kuu Njombe, Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe na Mahakama za Wilaya mkoani humo wakimsikiliza Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Njombe, Mhe. Joseph Luambano (hayupo katika picha).
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Mwanza)




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni