Ijumaa, 27 Machi 2026

JAJI MKUU AZINDUA KITABU CHA SHERIA HATIA NA ADHABU KATIKA MAKOSA YA JINAI...

 ·       Kitabu hicho chaandikwa na Jaji wa Rufani, Mhe. Paul Ngwembe

·       Kinatoa pia Tafakari ya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana

·       Hafla ya uzinduzi yashuhudiwa na Majaji wa Rufani, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Kiongozi, Viongozi wa Mahakama na wageni waalikwa

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 27 Machi, 2026 amezindua kitabu kiitwacho “Hatia na Adhabu katika Makosa ya Jinai: Kwa Kadri ya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana” kilichoandikwa na Jaji wa Mahakama Rufani Tanzania, Mhe. Paul Joel Ngwembe.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Kitabu hicho iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Masaju amempongeza Jaji Ngwembe kwa hatua hiyo kubwa ya kuandika kitabu hicho.

“Ninakupongeza Mhe. Ngwembe kwa hatua hii kubwa ya kuandika kitabu hiki licha ya majukumu makubwa yaliyopo mbele yako,” amesema Jaji Mkuu.

Kadhalika, Mhe. Masaju amempongeza pia Jaji Ngwembe kwa kuandika Kitabu hicho kwa Lugha ya Kiswahili, ambapo amesema kuwa, amefanya vizuri kutumia Lugha ya Taifa.

Aidha, Jaji Mkuu ametoa rai kwa Majaji wengine kutumia maarifa na ujuzi walionao katika kazi zao kuandika vitabu kwa manufaa ya Majaji, Mahakimu na Sekta ya Sheria kwa ujumla na kuwahakikishia kuwa, Mahakama iko tayari kutoa ushirikiano utakaohitajika kwa Majaji au Mahakimu walio tayari kwa uandishi wa vitabu.

Mhe. Masaju amesema kuwa, Watunga Sera wana wajibu wa kuangalia sheria zilizopo na zinazotungwa ili ziende sambamba na kuziunganisha na mila na desturi za jamii.

Akitoa neno la utangulizi, naye Jaji Ngwembe amesema, Kitabu hicho alichoandika ni matokeo ya utafiti wa muda mrefu wa Sheria zenye Adhabu za Chini (Minimum sentence) ikiwa ni pamoja na adhabu za Makosa ya Kujamiiana uliofanywa ili kubaini mahusiano ya Jamii ya Tanzania na Misingi ya Utungaji wa Sheria nchini.

“Utafiti huo wa muda mrefu umeunganishwa na uzoefu wa kusilikiza mashauri yanayohusu makosa hayo.  Hivyo Kitabu hiki ni matokeo ya utafiti na uzoefu wa kusikiliza mashauri mbalimbali katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, ni kitabu kilichobeba mifano halisi siyo nadharia pekee,” amesema Mhe. Ngwembe.

Amesema kuwa, ameandika Kitabu hicho ili kuongeza wigo wa vitabu vya Sheria katika jamii ya Watanzania na pia kuhimiza wasomi na Majaji kuona haja ya kuandika michango yao katika ustawi wa nchi.

“Mahakama na Wasomi walioko kwenye taaluma za Sheria wanakutana na mambo mengi ambayo wakati mwingine yanakinzana na dhamiri (Counscience). Lakini kwa asili ya kazi za Ujaji au Uhakimu hawawezi kulalamika au kuzigomea Sheria hizo, badala yake wanakaa kimya. Basi Kitabu hiki kinalenga kushawishi  na kuwahamasisha Wasomi wetu kutafiti na kuandika kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo” ameeleza Jaji Ngwembe.  

Amesema kwamba, ameandika kitabu hicho kwa Lugha ya Kiswahili rahisi kinachoeleweka kwa mtu yeyote anayejua kusoma na kuandika kwa lugha ya Kiswahili.

“Nimelenga kitabu hiki kiwafikie Wanazuoni wa vyuo vikuu, Majaji na Mahakimu wa ngazi zote, Wanasheria, Watunga Sheria na Watungiwa Sheria,” amesema.

Ameongeza kuwa, Kitabu hicho kimechambua kwa mtiririko wa Kihistoria, misingi ya Jamii na utunzi wa Sheria zinazoongoza jamii husika, Changamoto ya mifumo mbalimbali ya jamii katika mabadiliko  chanya yaliyoletwa na maendeleo ya Kisasa.

Aidha, Mhe. Ngwembe amesema kuwa, kupitia kitabu hicho amechambua kwa uwazi mifano hai ya madhara hasi ya sheria zinazotungwa bila utafiti wa kina wa mahitaji halisi ya jamii. Vilio visivyo kwisha vya kuwepo kwa sheria zilizotungwa bila ushirikishwaji wa jamii na nje ya mahitaji halisi ya jamii na mwisho kimetoa mapendekezo na maoni ya jumla.

Katika hatua nyingine, Jaji Ngwembe amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na afya njema hadi kufika siku hii muhimu na vilevile amemshukuru Jaji Mkuu kwa utayari wake kuwa mgeni rasmi katika tukio hilo adhimu. 

Kadhalika amewashukuru Majaji wenzake wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu kwa kuacha kazi zao na kuitikia mwaliko wake, sambamba na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na watendaji wake kwa kubeba jukumu hilo.

Amewashukuru pia Maprofesa wote wakiongozwa na Profesa Ilomo wa Chuo Kikuu cha Iringa aliyeshiriki kuhariri kitabu hicho pamoja na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Nangela kwa uchambuzi alioufanya kuhusu Kitabu hicho.

Vitabu vingine alivyowahi kuandika Jaji Ngwembe ni pamoja na Kitabu cha Historia ya Kijiji cha Nyanyembe (1900 - 2019) Mapinduzi chanya Yaliyoletwa na Kanisa na Serikali ambacho kilizinduliwa mwaka 2020, Kitabu cha tafakari ya Familia ya Joel Ngwembe Tulikotoka, Mafanikio, Changamoto na Tunakokwenda (1921 - 2022)  kilichozinduliwa 2023, Tafakari ya Maisha ya Jesse Jonathan Mtisi, alikuwa mkandarasi aliyejenga Mahakama za Mwanzo nyingi na kukarabati Jengo la Mahakama Kuu Tanga na pia alijenga Cathedraw ya Dayosisi ya Mufindi na pia  anakamilisha Kitabu cha Historia ya Wilaya ya Mufindi, Utawala, Uchumi na Utamaduni.

Matukio katika picha, hafla ya uzinduzi wa Kitabu kiitwacho “Hatia na Adhabu katika Makosa ya Jinai: Kwa Kadri ya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana” kilichoandikwa na Jaji wa Mahakama Rufani Tanzania, Mhe. Paul Joel Ngwembe.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju (wa tatu kushoto) akizindua kitabu kiitwacho “Hatia na Adhabu katika Makosa ya Jinai: Kwa Kadri ya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana” kilichoandikwa na Jaji wa Mahakama Rufani Tanzania, Mhe. Paul Joel Ngwembe. Hafla hiyo imefanyika leo tarehe 27 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Mwarija, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mwandishi wa Kitabu hicho, Mhe. Paul Ngwembe, wa kwanza kulia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari na wa kwanza kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza leo tarehe 27 Machi, 2026 wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu kiitwacho “Hatia na Adhabu katika Makosa ya Jinai: Kwa Kadri ya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana” kilichoandikwa na Jaji wa Mahakama Rufani Tanzania, Mhe. Paul Joel Ngwembe. Hafla hiyo imefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani.


Jaji wa Mahakama Rufani Tanzania, Mhe. Paul Joel Ngwembe akitoa neno kuhusu Kitabu alichoandika kiitwacho “Hatia na Adhabu katika Makosa ya Jinai: Kwa Kadri ya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana.”


Sehemu ya makundi mbalimbali ya watu waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho wakiwemo Majaji, Viongozi wengine wa Mahakama, Watumishi na Wageni waalikwa waliohudhuria katika hafla hiyo.

    Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Kitabu kilichoandikwa na Jaji Ngwembe.Wa pili kushoto ni Jaji wa Rufani na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Mwarija, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Paul Ngwembe, wa kwanza kulia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari na wa kwanza kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt Mustapher Mohamed Siyani.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha za pamoja na makundi mbalimbali ya washiriki waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa kitabu.

Mchambuzi wa kitabu ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Deo John Nangela akitoa neno wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu 
kiitwacho “Hatia na Adhabu katika Makosa ya Jinai: Kwa Kadri ya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana” kiichoandikwa na Jaji Ngwembe.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya akitoa neno wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu kilichoandikwa na Jaji Ngwembe.

Mhariri wa Kitabu 
kiitwacho “Hatia na Adhabu katika Makosa ya Jinai: Kwa Kadri ya Sheria ya Makosa ya Kujamiiana” kilichoandikwa na Jaji wa Mahakama Rufani Tanzania, Mhe. Paul Joel Ngwembe, Profesa Falres Ipyana Ilomo akitoa neno wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho.










 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni