Ijumaa, 27 Machi 2026

MAHAKAMA KANDA YA KIGOMA YAPOKEA MTENDAJI MPYA

·       Ni Bw. Yusuph Mhoja Kasuka

·       Aonesha furaha ya kupangiwa Kituo hicho

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile amewaongoza Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda Kigoma kushuhudia makabidhiano ya Ofisi baina ya Bw. Filbert Matotay na Mtendaji mpya wa Kanda hiyo, Bw. Yusuph Mhoja Kasuka.

Makabidhiano yalifanyika tarehe 24 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Kigoma.

Akizungumza katika hafla ya chakula cha jioni kilichoandaliwa maalum kwa ajili ya ukaribisho wa Mtendaji huyo, Mhe. Rwizile alimueleza Bw. Kasuka kuwa, Mahakama Kanda ya Kigoma ina timu nzuri ya watumishi na vilevile ni sehemu nzuri ya kufanya kazi kwa kuwa ina mazingira na hali ya hewa nzuri.

“Tunakukaribisha sana Kigoma tuna ari kubwa ya kufanya kazi na watu wa Kigoma ni wema sana tutakupa ushirikiano mkubwa hivyo utafurahia maisha, ni vema ukawa na familia yako karibu kwa ajili ya utulivu wako katika majukumu mazito uliyoaminiwa nayo na kuletwa Kigoma kufanya kazi,” alisema Jaji Rwizile.

Vilevile, alitoa pongezi kwa Bw. Matotay aliyekuwa Mtendaji wa Mahakama hiyo kabla ya uhamisho, kuwa ni mchapa kazi,  mwenye ushirikiano mkubwa katika kazi zake za utendaji, hata hivyo amemtakia kazi njema katika kituo chake kipya cha Mahakama Kuu Kanda ya Singida.

Aidha kikao hicho kilihudhuriwa na watumishi  wa kanda ya kigoma kwa njia ya Mahakama Mtandao (Virtual Court) kutoka Mahakama za wilaya Kigoma, Kasulu, Kibondo, Uvinza, Buhigwe na Kakonko.

Picha ya makabidhiano ya Ofisi kati ya aliyekuwa Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma kutoka kwa  Bw. Filbert Matotay (kushoto) na  Bw. Yusuph Mhoja Kasuka Mtendaji mpya wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.

Mtendaji mpya wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Bw. Yusuph Mhoja Kasuka akipokea ua kutoka kwa mtumishi wa Mahakama hiyo, Bi. Regina Kija kama ishara ya ukaribisho mara baada ya Mtendaji huyo kuwasili katika viwanja vya Mahakama Kuu hiyo.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akitoa neno la ukaribisho kwa Mtendaji mpya wa Mahakama Kuu Kigoma, Bw. Yusuph Mhoja Kasuka (hayupo katika picha) wakati wa chakula jioni. Kushoto ni aliyekuwa Mtendaji wa Mahakama Kuu Kigoma ambaye amehamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Singida, Bw. Filbert Matotay.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (wa kwanza kushoto). Katikati ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi, kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza, kwa pamoja wakisoma kwa makini taarifa ya makabidhiano ya Ofisi ya Mtendaji wa Mahakama hiyo.


Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Yusuph Mhoja Kasuka akitoa neno la shukrani kwa mapokezi na kuahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na watumishi wote.

Watumishi wakifuatilia kwa makini uwasilishwaji wa taarifa ya makabidhiano ya Ofisi ya Mtendaji iliyokuwa ikiwasilishwa na Bw. Filbert Matotay.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni