Jumatano, 11 Machi 2026

JAJI MKUU, MHE. GEORGE MASAJU AKUTANA NA MJUMBE MAALUM WA KATIBU MKUU UMOJA WA MATAIFA

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 11 Machi, 2026 amekutana na kufanya mazungumzo na Bw. Parfait Onanga-Anyanga,  Mjumbe Maalum  wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. António Guterres.

Bw. Onanga-Anyanga na ujumbe alioambatana nao waliwasili Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma majira ya Asubuhi na kupokelewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel na Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert.

Mjumbe huyo Maalum amefanya ziara nchini Tanzania kwa lengo la kuonana na Viongozi mbalimbali wa Serikali kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu amani, uimarishaji wa demokrasia na utawala wa sheria kwa ujumla.

Bw. Onanga-Anyanga yupo nchini Tanzania pia kusikiliza maoni ya wadau mbalimbali na kutathmini hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha utulivu wa kisiasa, mshikamano wa kitaifa na kuendeleza misingi ya utawala wa sheria kufuatia matukio ya uvunjifu wa amani ya kabla na wakati wa Uchaguzi Mkuu tarehe 29 Oktoba, 2025.

Aidha, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua inayoendelea kuchukua kufuatia matukio ya uvunjivu wa amani wakati na baada ya uchaguzi wa tarehe 29 Oktoba, 2025. Ameeleza kuwa hatua hizo ni pamoja na; kuunda Tume Huru ya Uchunguzi ya Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba, 2025, dhamira ya kufanya mazungumzo jumuishi na mchakato wa mabadiliko ya Katiba.

Bw. Onanga–Anyanga ameeleza kuwa Umoja wa Mataifa unaendelea kuitambua Tanzania kama nchi yenye historia ya muda mrefu ya amani na pia wanatambua umuhimu wa kuwa na taasisi imara mfano Mahakama kwa ajili ya ustawi wa Taifa.

Kwa upande wake Mhe. Jaji Mkuu amemshukuru Mjumbe huyo Maalum kwa kutambua juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania.

Aidha, Mhe. Masaju amemueleza Bw. Onanga-Anyanga kwamba, Mahakama ya Tanzania imeendelea kuwa huru na kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba mashauri yaliyofunguliwa kuhusiana na mchakato wa uchaguzi na pia baada ya uchaguzi yameshughuliwa ipasavyo.

Katika ziara hiyo Bw. Onanga-Anyang mbali na wajumbe wengine ameambatana pia na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), Bw. Shigeki Komatsubara.

Picha mbalimbali za ziara ya Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa (UN) katika Umoja wa Afrika, Bw. Parfait Onanga-Anyanga Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika, Bw. Parfait Onanga-Anyanga leo tarehe 11 Machi, 2026 ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma wakati alipomtembelea Jaji Mkuu. 

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akimpokea Bw. Parfait Onanga-Anyanga, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati yeye na ujumbe alioambatana nao walipowasili Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma kwa lengo la kuonana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) pamoja na Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert wakiongoza Ujumbe wa Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulipowasili Makao Makuu ya Mahakama kuonana na kufanya mazungumzo na Jaji Mkuu.


Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Parfait Onanga-Anyanga akisaini kitabu cha wageni alipowasili ofisini kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 11 Machi, 2026 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Mazungumzo kati ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju, Ujumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na sehemu ya Viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakiendelea na mazungumzo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akimpatia zawadi 
Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Parfait Onanga-Anyanga.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akimpatia zawadi Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), Bw. Shigeki Komatsubara.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Masaju akitoa zawadi kwa wajumbe walioambatana na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa waliomtembelea ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 11 Machi, 2026.







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni