Jumatano, 11 Machi 2026

UADILIFU NDIO NGUZO KUU YA UTENDAJI; PROF. NDALICHAKO

Na HABIBA MBARUKU, Mahakama-Dodoma

Mbunge wa Kuteuliwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake, Prof. Joyce Ndalichako amewaeleza Majaji na Mahakimu Wanawake wa Tanzania kuwa, weledi na uadilifu ndizo nguzo kuu na muhimu za utendaji hivyo hawana budi kuzizingatia wakati wanapotimiza wajibu wao.

Prof. Ndalichako aliyasema hayo jana tarehe 10 Machi, 2026 alipokuwa akifunga Kongamano Maalum la Kusheherekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake, lililofanyika katika ukumbi wa New Generation Hall Kisasa jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa kufunga Kongamano hilo, Prof. Ndalichako amesema kuwa, ameridhishwa na mjadala wenye afya na nia ya dhati ya kujenga na kuimarisha haki na usawa wa kijinsia, pamoja na maazimio yaliyowekwa ambayo watakwenda kuyatekeleza.

Aliongeza kuwa, lengo la kuanzishwa kwa TAWJA ni kutambua mchango wa Majaji Wanawake duniani na kuhimiza usawa wa kijinsia katika Mhimili wa Mahakama, hivyo kongamano hilo ni tukio muhimu la kubadilishana maarifa kuonesha uongozi, ujasiri na dira ya mabadiliko pia ni mwanga unaoangaza nuru na kazi kubwa wanayoifanya ambayo inaakisiwa hadi nje na si ndani ya kumbi za Mahakama pekee bali katika jamii nzima.

Prof. Ndalichako amesisitiza kuwa uadilifu ni nguzo kuu ya utendaji, hivyo ni vema Majaji na Mahakimu Wanawake kuendelea kuzingatia uadilifu katika masuala ya haki, huku akinukuu maneno ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati alipokuwa akiwaapisha Majaji ambapo alisema, “uzoefu umeonesha kuwa Majaji wanawake huwazidi wenzao wa kiume katika utendaji unaozingatia masuala ya uadilifu.”

Aliongeza kuwa, anavutiwa na weledi, mshikamano na kujitoa kwa Majaji na Mahakimu wanawake hali inayoleta mabadiliko ya kijamii kwa kuzingatia utawala wa haki unaoleta usawa wa kijinsia.

Aidha, amesema kuwa haki haitoshi kutolewa bali inapaswa ieleweke na iguse mioyo ya watu pamoja na kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama, hivyo Majaji na Mahakimu Wanawake wana nafasi muhimu katika kuhakikisha sheria inazungumza kwa haki na uadilifu.

Katika hatua nyingine, Prof. Ndalichako alizungumzia kuhusu umuhimu wa kuimarisha mifumo ya Taasisii ili kulinda afya ya kisaikolojia ya Mahakimu ambapo ameeleza kuwa mtu hawezi kuponya wengine ikiwa yeye mwenyewe ana maumivu, hivyo ni vema kulinda afya ya akili ili kuimarisha utendaji.

“Mmesisitizwa pia kuhusu umuhimu wa kulinda mifumo ya Taasisi ili kulinda afya ya kisaikolojia ya Mahakimu, huwezi kuponya jamii wakati wewe mwenyewe unaumia kimyakimya, ni vema kuendelea kuhakikisha kwamba tunalinda afya za akili ndani ya Makahama ili iendelee kutoa haki endelevu,” alisisitiza Mwenyekiti huyo.

Kadhalika, alisema kuwa, ni vema kuepuka kuwajeruhi upya wahanga na manusura wa ukatili wa kijinsia na kusisitiza kuwa, manusura wanastahili kujisikia salama na kuheshimiwa, hivyo haki lazima irejeshe utu na si kufungua tena majeraha.

Alieleza kwamba, teknolojia inakua kwa kasi hivyo ni vema itumike katika kuwalinda waathirika wa masuala ya ukatili wa kijinsia hasa ukatili wa mitandaoni, hivyo ubunifu ni lazima uendelee kutumika ili kuimarisha ulinzi wa waathirika na kuongeza uwajibikaji kwa kutumia Mahakama mtandao.

Alisema kuwa, yeye kama Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake anawahakikishia kuwa, Bunge pamoja na Wabunge wengine wataendelea kushirikiana katika kuimarisha sheria zinazolinda wanawake na watoto, hivyo ujumbe alioubeba katika mijadala ya leo utatumika ili kuendelea kukuza usawa wa kijinsia. 

Katika hatua nyingine, Prof. Ndalichako ameeleza kuwa mojawapo ya mafanikio makubwa kwa Mahakama na Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) ni kufikia usawa wa asilimia 50 kwa 50 kwa Majaji jambo ambalo ni la msingi katika kukuza imani kwa wananchi.

Kama Kaulimbiu ya mwaka huu inavyokumbusha, amewataka Majaji na Mahakimu hao wanawake kutoka mahakamani na kwenda kwenye jamii wakitoa haki kwa uadilifu huku wakijihusisha kikamilifu katika shughuli za uelimishaji hususan kupitia vyombo vya habari, kuzalisha maarifa na kujengeana uwezo jambo litalaojenga uaminifu kwa jamii ya watoto wa kike kuwa ndoto zao ni halali na matarajio yanawezekana na mustakabali wa maisha yake hauna mashaka.

Kauli mbiu ya Kongamano hilo kwa mwaka huu ni “Kutoka mahakamani kuifikia jamii: Majaji na Mahakimu wanawake mstari wa mbele kuongoza mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Awali, kongamano hilo lilifunguliwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Juma Homera, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi. Kongamano hilo lilihudhuriwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, UN Women, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na wageni wengine waalikwa.


Mbunge wa Kuteuliwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Joyce Ndalichako akizungumza alipokuwa mgeni rasmi wakati wa kufunga Kongamano maalum la Kusheherekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake lililofanyika kwenye ukumbi wa New Generation Hall jijini Dodoma. 


Mbunge wa Kuteuliwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Joyce Ndalichako (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya wajumbe wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) baada ya kufunga Kongamano Maalum la Kusheherekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake lililofanyika kwenye ukumbi wa New Generation Hall jijini Dodoma. Aliyekaa kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa TAWJA, Mhe. Barke Sehel na kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Winifrida Korosso. 


Mbunge wa Kuteuliwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Joyce Ndalichako (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya wajumbe wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) baada ya kufunga Kongamano Maalum la Kusheherekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake lililofanyika kwenye ukumbi wa New Generation Hall jijini Dodoma. Aliyekaa kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa TAWJA, Mhe. Barke Sehel na kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Winifrida Korosso. 


Mgeni rasmi Mbunge wa Kuteuliwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Joyce Ndalichako (kushoto) akifuatilia kinachojiri wakati wa kufunga Kongamano maalum la Kusheherekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake. Kushoto kwake ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano hilo, Mhe. Winifrida Korosso.

Mgeni rasmi wakati wa kufunga Kongamano Maalum la Kusheherekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake, Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa Majaji Wanaume waliohudhuria katika Kongamano hilo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni