Jumanne, 31 Machi 2026

KITUO JUMUISHI CHA MASUALA YA FAMILIATEMEKE CHATOA MAFUNZO KWA WAJANE

Na DHILLON UISSO-Mahakama, Dar es Salaam

Kituo Jumuishi cha Masuala ya FamiliaTemeke tarehe 28 Machi, 2026 kiliendesha mafunzo maalum kwa wajane wa Wilaya ya Temeke kwa lengo la kuwajengea uelewa kwenye haki zao za kisheria, hususan katika masuala ya urithi na mirathi.

Halikadhalika, washiriki wa mafunzo hayo walipatiwa elimu ya kisheria itakayowasaidia kulinda haki zao na za watoto wao, kusimamia mali za marehemu kwa mujibu wa sheria na kuepuka migogoro ya mirathi katika familia na jamii

Mafunzo hayo yalifunguliwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa, ambaye alisisitiza umuhimu wa wajane kufahamu haki zao, kufungua mirathi kwa wakati na kutumia mifumo ya kisheria ili kuepusha migogoro ya kifamilia.

Mtandao wa Mashirika yanayotoa Msaada wa Sheria Tanzania (TANLAP), uliowakilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa TANLAP, Wakili Fransisca Silaya, ndiyo uliofadhili mafunzo hayo.

Wakili Silaya, akizungumza wakati wa mafunzo hayo, alionesha dhamira ya Taasisi hiyo kuendelea kuunga mkono juhudi za utoaji wa elimu ya kisheria kwa makundi maalum katika jamii.

Mafunzo hayo yalijumuisha mada kuu nne zilizowasilishwa na wakufunzi wenye uzoefu, ikiwemo Urithi na Mirathi na Sheria za Urithi Tanzania zilizowasilishwa na Mhe. Magdalena Malaba.

Nyingine ni Kufungua Mirathi na Nyaraka Muhimu na Wosia na Ulinzi wa Haki zilizowasilishwa na Mhe. Edna Mollel.

Katika mada hizo, washiriki walipata uelewa wa kina kuhusu taratibu za mirathi, haki zao za kisheria, umuhimu wa nyaraka sahihi pamoja na namna ya kuandika wosia na kulinda haki zao.

Mafunzo yalihusisha wajane kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Temeke, wakiwemo wanachama wa vikundi vya kijamii, hususan kikundi cha VIWOTA Women Group. Washiriki walionesha hamasa kubwa ya kujifunza na kuchangia mijadala.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi Temeke, Bw. Samson Mashalla, alifunga mafunzo hayo na kuwasihi washiriki wote kutumia maarifa waliyoyapata maarifa kwenye maisha yao na kuwafikishia wengine elimu hiyo kwani ni nyenzo ya kujikomboa dhidi ya dhuluma na kuhakikisha haki inatendeka.

“Napenda pia kuwakumbusha kuwa taasisi zetu za haki, ikiwemo Kituo Jumuishi Temeke, zipo kwa ajili yenu. Msisite kufika pale mnapohitaji msaada wa kisheria au ushauri,” alisema.

Bw. Mashalla alitumia fursa hiyo kuushukuru Mtandao wa Asasi za Msaada wa Sheria Tanzania (TANLAP) kwa mchango wao katika kufanikisha mafunzo hayo, kwani mchango wao umeleta mabadiliko chanya katika maisha ya washiriki.

Aliwashukuru pia wakufunzi kwa kujitolea kutoa maarifa na kwa uvumilivu wao katika kuhakikisha kila mshiriki anaelewa mada zilizowasilishwa. “Mafunzo haya yamekuwa ya manufaa makubwa na yamegusa moja kwa moja maisha yetu ya kila siku,” alisema.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa, akizungumza wakati anafungua mafunzo hayo (Picha na Maktaba).

Kaimu Mkurugenzi wa Mtandao wa Asasi za Msaada wa Sheria Tanzania (TANLAP), Bi. Fransisca Silaya.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya kwenye Kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Magdalena Malaba, akiwsilisha mada kwenye mafunzo hayo.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo kwenye Kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Moleli, akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.

Washiriki wa mafunzo wakifuatilia kilichokuwa kinajiri.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Kituo Jumuishi Temeke, Bw. Samson Mashalla, akizungumza wakati anahitimisha mafunzo hayo.

Picha ya pamoja ya washiriki wakati wa mafunzo hayo.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni