Jumanne, 31 Machi 2026

MAHAKAMA KANDA YA MUSOMA YAFANYA KIKAO CHA MENEJIMENTI

Na FRANCISCA SWAI – Mahakama, Musoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya, amewapogeza Watumishi wa Mahakama Kanda ya Musoma kwa uwajibikaji mzuri uliowezesha Mahakama hiyo kuwa ya pili kitaifa kwa kasi nzuri ya umalizaji wa mashauri.

Mhe. Mtulya alitoa pongezi hizo katika kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma kilichofanyika hivi karibuni wilayani Serengeti katika ukumbi wa Ofisi ya Mashtaka.

Alisisitiza umuhimu wa vikao vya menejimenti ambavyo vinatumika kuweka mikakati mbalimbali ya kiutendaji pamoja na kusisitiza utekelezaji wa maelekezo ya Viongozi wa juu, jambo lililodhihirishwa kwa matokea mazuri ya usikilizaji na umalizaji wa mashauri.

Aidha, katika kikao hicho kinachoundwa na wajumbe kutoka Mahakama Kuu Musoma, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma na Mahakama za Wilaya za Musoma, Butiama, Bunda, Serengeti, Tarime na Rorya, ziliwasilishwa taarifa mbalimbali za utendaji kazi kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/26.

Kuliwasilishwa pia taarifa za Mkaguzi wa Ndani, Ofisa TEHAMA, miradi inayoendelea ndani ya Kanda na ushiriki katika matukio ya kijamii.

Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Monica Ndyekobora, alisisitiza utekelezaji wa maelekezo ya Viongozi wa Mahakama, ikiwemo ufungaji wa mirathi, kuendelea na utoaji wa adhabu mbadala pamoja na usikilizaji wa mashauri kwa wakati ili kuepuka kuzalisha mlundikano.

Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma, Bw. Leonard Maufi, alielezea mikakati mbalimbali ya Kanda, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu. Alisema kwa mwaka wa fedha, Kanda inaendelea na ukarabati mkubwa wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Nyaburongo iliyoko Wilayani Rorya kwa kutumia fedha za ndani.

Pia alielezea hatua iliyofikiwa katika miradi inayoendelea ya ujenzi wa Mahakama za Wilaya Serengeti na Tarime. Aidha, aliwaasa Watumishi kuendelea kuzingatia kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma.

Akihitimisha kikao hicho, Mhe. Mtulya aliwakumbusha wajumbe mafanikio yaliyopatikana ndani ya Kanda, ikiwemo kutovuka mwaka na mashauri mlundikano kwa miaka mitatu mfululizo na ukarabati wa majengo ya Mahakama, hasa za Mwanzo.

Alitaja mafanikio mengine kama ulinzi wa mipaka ya maeneo ya Mahakama, upatikanaji wa hati, umoja na ushirikiano wa kikanda kwenye kazi na matukio ya kijamii kma kushiriki matukio ya huzuni na furaha.

Hivyo aliwaasa wajumbe hao kwenda kuwasimamia vyema Watumishi katika maeneo yao ili, kwa pamoja waweze kufikia malengo ya Kanda yaliyowekwa.

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (katikati), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Monica Ndyekobora (kulia) na Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Leonard Maufi (kushoto), wakichambua kwa makini baadhi ya taarifa zilizowasilishwa na wajumbe wa kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma.

Wajumbe wa kikao cha Menejiment Kanda ya Musoma kutoka Wilaya mbalimbali wakiwasilisha taarifa za utendaji kazi katika vituo vyao vya kazi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Mhe. Veronica Mugendi (aliyesimama), akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa kituo chake katika kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma.

Afisa Tawala wa Mahakama Kuu Musoma, Bw. Kandana Lucas (aliyesimama), akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama Kuu Musoma pamoja na taarifa ya miradi inayotekelezwa ndani, huku wajumbe wakifuatilia kwa makini taarifa hiyo wakati wa kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma.

Mkaguzi wa Ndani wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Andala Odock (aliyesimama), akiwasilisha taarifa ya ukaguzi katika kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma.

Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Japhet Mnyetta (aliyesimama), akiwasilisha taarifa ya hali ya miundombinu na matumizi ya TEHAMA ilivyo ndani ya Kanda ya Musoma wakati wa kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Monica Ndyekobora, akiwasilisha taarifa ya hali ya mashauri ilivyo ndani ya Kanda ya Musoma wakati wa kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Leonard Maufi (aliyesimama), akifafanua jambo wakati wa kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma.

Mjumbe wa kamati ya utalii (matukio ya kijamii) ambaye ni Mhasibu wa Mahakama Kuu Musoma, Bi. Samira Nkya (aliyesimama), akiwasilisha taarifa ya ushiriki katika matukio ya kijamii ndani ya Kanda ya Musoma wakati wa kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (katikati), akisisitiza jambo kwa wajumbe wa kikao cha Mnenejimenti Kanda ya Musoma wakati wa kikao hicho.

Picha ya pamoja ya wajumbe wa kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma walipotembelea mmoja ya miradi inayoendelea ndani ya Kanda hiyo, ambayo ni ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Wilaya Serengeti, mara baada ya kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma kilichofanyika Wilayani Serengeti. 

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni