Jumanne, 31 Machi 2026

JAJI RWIZILE AWASISITIZA VIONGOZI WA MAHAKAMA KIGOMA KUZINGATIA MAMBO SITA MUHIMU

Na AIDAN ROBERT - Mahakama Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile amewataka Mahakimu pamoja na Viongozi  wengine wa Mahakama Kigoma kufanya kazi kwa kuzingatia mambo sita muhimu ya maadili ambayo ni Uadilifu, kuwa viongozi bora kwa wengine, kujali stahili za watumishi, Ubunifu katika kazi, Mahusiano mazuri kazini na mawasiliano ya karibu katika utendaji wa shughuli za kiutawala.

Mhe. Rwizile aliyasema hayo tarehe 28 Machi 2026 wakati akifungua Kikao cha Uongozi kwa robo ya tatu ya mwaka kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mahakama ya Wilaya Buhigwe ambapo alitumia fursa hiyo kuwakumbusha kuhusu majukumu ya kila siku na kubaini mapungufu, changamoto na kuona mapendekezo na njia sahihi za kutatua changamoto hizo.

“Fanyeni kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na nidhamu kama Sheria ya  Utawala wa Mahakama inavyotutaka katika ibara (237), ambapo Sheria hii ina maboresho yake imeeleza wazi utendaji wa Viongozi wa Mahakama katika mnyororo wa haki na hasa fungu la (11) ambapo linaeleza wazi jinsi ambavyo utawala katika muhimili wa Mahakama unapaswa kuwa, ni vema mkaisoma vizuri ili kuongeza weledi katika eneo la utawala,” alisema Jaji Rwizile.

Aidha, alisisitiza pia kifungu cha (65) cha sheria hiyo kinachotoa namna ambavyo watendaji wanafanya kazi wakishirikiana na Ofisi ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, ikiwataka kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha shughuli za kiutawala zinasimamiwa vema kwa ajili ya kuhakikisha mnyororo wa usikilizwaji wa mashauri katika Mahakama zote haukwami kwa namna yeyote.

Hata hivyo, aliwasisitiza viongozi hao kuongeza kasi katika umalizaji wa mashauri kwa kuzingatia lengo mama la Mahakama ya Tanzania ambalo ni kusikiliza mashauri na kuyatolea uamuzi mapema ipasavyo. Vilevile Mhe.Rwizile aliwaasa Viongozi kuendelea kudumisha ushirikiano mzuri uliopo eneo la kazi.

Sambamba na hayo Jaji Rwizile, alizindua chumba cha Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kasulu Mjini kilichokarabatiwa kwa fedha ya ndani ili kusaidia kusogeza huduma na kuongeza kasi ya usikilizwaji wa mashauri kwa Mahakama za Mwanzo.

Aidha, wajumbe wa kikao hicho walipata fursa ya kupanda miti ya matunda katika eneo la wazi lililopo katika Mahakama ya Wilaya Buhigwe.

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. John Francis Nkwabi, alitoa pongezi kwa Viongozi wa Mahakama za Wilaya Kanda ya Kigoma kwa jinsi wanavyoshirikiana kwa karibu na watumishi wa kada zote kuhakikisha usikilizwaji wa mashauri na kutunza miundombinu ya Majengo na TEHAMA inaendelea kuboreshwa ili utendaji wa kazi za watumishi uendelee kuwa rahisi, sambamba na ubunifu unaoleta tija katika shughuli za kila siku.

Katika ziara hiyo iliyoambatana na Kikao cha Uongozi, Jaji Mfawidhi, Mhe. Rwizile aliambatana na Viongozi wengine wa Mahakama akiwemo Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Projestus Kahyoza, Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka na Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Singida, Bw.Filbert Matotay, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo, Mahakimu Wakazi Wafawidhi kutoka Wilaya za Kigoma, Kasulu, Kibondo, Uvinza, Buhigwe na Kakongo pamoja na Wakuu wa Vitengo wa Mahakama Kuu Kigoma.


Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine  Rwizile akisisitiza jambo wakati alipokuwa akifungua Kikao cha Uongozi wa Mahakama Kanda ya Kigoma kilichofanyika tarehe 28 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa Mahakama ya Wilaya Buhigwe.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Kigoma, Mhe.Augustine
 Rwizile akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Ofisi ya Hakimu. Pamoja naye wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. John Francis Nkwabi, wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Projestus Kahyoza na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu na walisimama nyuma wakishuhudia ufunguzi huo viongozi wengine wa Mahakama pamoja na watumishi wa Mahakama Kasulu. 

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. Augustine Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Wakuu wa Vitengo Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma. Wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Projestus Kahyoza, wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili Mahakama Kuu-Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa na wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Yusuph Mhoja.

Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. Augustine Rwizile akipanda mti wa matunda katika eneo la Mahakama ya Wilaya Buhigwe mara baada ya Kikao cha Uongozi kumalizika.

 
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. John Nkwabi akipanda mti wa matunda katika eneo la Mahakama ya Wilaya Buhigwe mara baada ya kikao cha uongozi kumalizika.

  
Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa akipanda mti wa matunda katika eneo la Mahakama ya Wilaya Buhigwe.
 
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Yusuph Mhoja akipanda mti wa matunda katika eneo la Mahakama ya Wilaya Buhigwe.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. Augustine Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya na Mwanzo Kasulu (waliosimama) mara baada ya uzinduzi wa chumba cha Hakimu. Kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi, kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

 

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni