Jumatatu, 9 Machi 2026

MAHAKAMA YA TANZANIA, ZANZIBAR WAANZA MAFUNZO YA KUBADILISHANA UZOEFU DODOMA

  • Washiriki watakiwa kuimarisha maadili, matumizi ya TEHAMA katika usimamizi wa mashauri

Na HALIMA MNETE & JAMES BUSANYA-Mahakama, Dodoma.

Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, leo tarehe 9 Machi 2026 amefungua mafunzo ya kubadilishana uzoefu kati ya Maofisa wa Mahakama ya Tanzania na wenzao kutoka Mahkama ya Zanzibar, yaliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo mbele ya washiriki kutoka Zanzibar wakiongozwa na Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar, Mhe. Ibrahim Mzee Ibrahim, Mhe. Tengwa alisema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kimfumo kati ya Taasisi hizo mbili katika kuboresha utoaji wa haki kwa wananchi.

Alisema Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Zanzibar zimeona umuhimu wa kuendelea kubadilishana uzoefu ili kuimarisha weledi, uadilifu na uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa Mahakama, hali itakayosaidia kuongeza imani ya wananchi kwa Mhimili wa utoaji haki.

“Nawapongeza washiriki wote kutoka Zanzibar kwa kufika Dodoma salama. Mafunzo haya ni fursa muhimu ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuimarisha uwezo wetu katika utoaji wa huduma bora za Mahakama,” alisema Mhe. Tengwa.

Aliongeza kuwa uchaguzi wa Dodoma kama eneo la kufanyia mafunzo hayo umezingatia mazingira yake tulivu yanayofaa kwa kujifunza na kujadiliana masuala muhimu yanayolenga kuboresha utendaji wa Mahakama.

Katika hotuba yake, alieleza kuwa mafunzo hayo yatajadili mada mbalimbali muhimu ikiwemo ukaguzi wa shughuli za Mahakama, utekelezaji wa majukumu ya msingi, maboresho ya huduma za Mahakama, maadili na namna ya kushughulikia malalamiko ya kimaadili, usimamizi wa mashauri, matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika usimamizi wa mashauri pamoja na kuharakisha umalizaji wa mashauri.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia usawa wa kijinsia katika utoaji wa huduma za Mahakama, akieleza kuwa Mahakama inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha haki na usawa vinazingatiwa kwa vitendo katika jamii.

Mhe. Tengwa alinukuu kauli ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa, aliyewahi kusema kuwa mtu hawezi kujua kama mama yake ni mpishi mzuri hadi pale atakapoonja chakula kilichopikwa na mama mwingine, akieleza kuwa mfano huo unaonesha umuhimu wa kujifunza kutoka kwa wengine.

Alisema kuwa kupitia mafunzo hayo washiriki wanatarajiwa kuwa mabalozi wa kuimarisha utatuzi wa migogoro kwa wakati, kuboresha huduma za Mahakama kupitia ukaguzi pamoja na kuimarisha maadili na usawa wa kijinsia katika utendaji wao.

Mafunzo hayo ya siku tano yatahitimishwa tarehe 13 Machi, 2026, yakilenga kuongeza ufanisi katika usimamizi na utoaji wa haki kwa wananchi.

Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, akizungumza wakatia anafungua mafunzo hayo. Picha chini ni washiriki wa mafunzo yanayofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.




Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni