Na JENIFER MALISA-Mahakama, IJC Temeke
Majaji na Mahakimu katika Kituo Jumuishi cha Masuala
ya Familia Temeke, hivi karibuni walikutana kufanya mafunzo mafupi kuhusu
makosa yanayojitokeza katika uendeshaji wa mashauri ya ndoa (common
pitfalls in matrimonial proceedings).
Katika mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa
Mikutano wa Mahakama hiyo, Majaji na Mahakimu pia walishirikishana uzoefu wa
elimu kuhusu masuala hayo.
Kaimu Jaji Mfawidhi, Mhe. Sharmillah Sarwatt,
alifungua mafunzo hayo ya ndani na kusisitiza; “Umuhimu wa mafunzo hauepukiki
na tunapopata wasaa kama huu tunapata muda wa kuongeza ujuzi wetu.”
Pamoja na kujadili masuala ya ndoa na makosa
yanayojitokeza katika uendeshaji na uamuzi wa mashauri ya ndoa, mjadala pia ulijikita
zaidi katika masuala ya dhana ya ndoa na mgawo wa mali, masuala ya matunzo na
malezi ya watoto.
Washiriki wa mafunzo hayo pia walijadili hangamoto
au makosa mbalimbali yanayoweza kujitokeza au yaliyowahi kujitokeza wakati wa
uendeshaji au uamuzi wa mashauri ya ndoa na kusababisha au kubatilisha mwenendo
mzima na hukumu au kuwaathiri wadaawa kwa namna moja ama nyingine.
Washiriki pia walijadili na kuazimia namna bora ya
kuepuka makosa hayo ili kuboresha utendaji wa kazi katika utoaji haki.
Watoa mada wakati wa mafunzo hayo walikuwa Hakimu Mkazi Mkuu, Mhe. Magdalena Malaba na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Mhangwa
Yunge.
Baada ya uwasilishaji wa mada hizo, Majaji wa Mahakama Kuu IJC Temeke, Mhe. Asina Omari na Mhe. Sarah Mwaipopo, walitoa uzoefu wao.
Katika mafunzo
hayo, washiriki walishauri kuwa ilikuwa ni mjadala wa namna ya kuamua mtoto
akae kwa nani katika ya baba na mama, ni vema maslahi
ya mtoto yakaangaliwa kwa mapana yake,
ikiwemo matakwa ya sheria ya mtoto pamoja na taarifa kutoka kwa Ofisa Ustawi
wa Jamii.
Hata hivyo,
washiriki walishauri ni vema masharti ya kumuona mtoto yawe wazi na
yanayotekelezeka ili haki kwa pande zote zizingatiwe pale mtoto anapokaa chini
ya usimamizi wa mzazi mmoja wapo.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni