●
Wajadili nafasi ya wanamke katika kuimarisha utoaji haki na
kuifikia jamii
Na HALIMA MENETE, Mahakama-Dodoma
Kongamano maalumu la kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Majaji
na Mahakimu Wanawake limefanyika leo tarehe 10 Machi 2026 katika ukumbi wa New
Generation jijini Dodoma, likiwakutanisha Viongozi wa Serikali, Mahakama ya
Tanzania pamoja na wadau wa maendeleo kujadili nafasi ya Majaji na Mahakimu
wanawake katika kupambana na ukatili wa kijinsia.
Kongamano hilo lililobeba Kauli mbiu, “Kutoka Mahakamani
Kuifikia Jamii: Majaji na Mahakimu Wanawake Mstari wa Mbele Kuongoza Mapambano
Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia” lilihudhuriwa na mgeni rasmi Waziri wa Katiba
na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Prof. Elisante Ole Gabriel, Majaji na Mahakimu wa Mahakama ya Tanzania bara na
visiwani pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo UN Women, RITA, Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka.
Katika kongamano hilo pia, kulikuwa na nafasi ya utoaji mada
mbalimbali, ambapo moja wa mada ilihusu “Nafasi ya Mwanamke kama Kiongozi
katika Kuleta Mabadiliko kwenye Jamii kupitia Utoaji wa Haki unaozingatia
Masuala ya Kijinsia.”
Mada hiyo iliwasilishwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe.
Rehema Joseph Kerefu huku ikiendeshwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya
Dar es Salaam, Mhe. Salma Magimbi, na ilijadiliwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu
Moshi Mhe. Dkt Lilian Mongela, Naibu Msajiri Mhe. Upendo Ngitiri na Hakimu
Mkazi, Mhe. Juliana Mvungi.
Akifafanua kwa kina mada hiyo, Mhe. Kerefu amesema kuwa,
katika juhudi za kuimarisha usawa wa kijinsia katika utoaji wa haki, tayari
kuna misingi na nyenzo mbalimbali zilizowekwa kimataifa na kitaifa ambazo
zinaweza kusaidia katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Amesema miongoni mwa nyenzo hizo ni pamoja na maandiko ya
kitaaluma kama kitabu kilichoandikwa na Kosana Beker kinachojadili Gender
and Diversity in the Judiciary, ambacho kinaeleza kwa kina umuhimu wa
kuzingatia masuala ya kijinsia na utofauti katika mfumo wa utoaji haki.
Kwa mujibu wa Jaji Kerefu, uwepo wa vitendea kazi hivyo
unaonesha wazi kuwa, kuna uwanja mpana wa kuhakikisha haki za binadamu
zinalindwa ipasavyo na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vinatokomezwa.
Hata hivyo, ameeleza kuwa, pamoja na uwepo wa misingi hiyo
imara ya kisheria na kitaaluma bado kuna changamoto zinazotokana na baadhi ya
mila, desturi na tamaduni katika jamii ambazo wakati mwingine zimekuwa
zikikwamisha juhudi za kuimarisha usawa wa kijinsia.
Amesema baadhi ya mila na desturi hizo zimejikita katika
mfumo dume, hali ambayo wakati mwingine imekuwa ikiweka vikwazo kwa watoa haki
katika kuhakikisha misingi ya usawa wa kijinsia kama ilivyoainishwa katika
mikataba ya kimataifa, Katiba ya nchi na sheria mbalimbali zinazozingatia
masuala ya kijinsia zinatekelezwa kikamilifu.
Aidha, amesema licha ya maendeleo yaliyopatikana katika
kuimarisha haki za wanawake, bado kuna changamoto mbalimbali zinazoendelea
kujitokeza katika jamii ikiwemo ongezeko la mashauri ya ubakaji, unyanyasaji wa
kingono, ukatili wa majumbani pamoja na ndoa za utotoni.
Ameongeza kuwa, hata katika masuala ya umiliki wa mali na
mirathi bado kuna changamoto zinazowakabili wanawake katika jamii, huku baadhi
ya sheria zilizopo zikionekana kutokidhi kikamilifu matakwa ya usawa wa
kijinsia.
Ametolea mfano wa ‘Customary Law Declaration Order’ ya mwaka
1963 pamoja na baadhi ya vipengele vya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ambavyo
bado vinaibua mjadala kutokana na kuwepo kwa vipengele vinavyohusishwa na
ruhusa ya ndoa za utotoni.
Kwa upande mwingine, washiriki wa mada hiyo walieleza kuwa, changamoto
hizo zinapaswa kuwa chachu kwa wadau wa sekta ya sheria, hususan majaji na
Mahakimu wanawake, kuendelea kutumia elimu yao ya sheria pamoja na misingi
iliyowekwa kuhakikisha vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia vinatokomezwa.
Vilevile ilielezwa kuwa mapambano dhidi ya ukatili wa
kijinsia yanahitaji ushirikiano mpana wa taasisi mbalimbali, ikiwemo Mahakama,
Serikali, Wadau wa maendeleo pamoja na jamii kwa ujumla.
Akizungumzia uwakilishi wa wanawake katika Sekta ya Mahakama
duniani, Mhe. Kerefu alieleza kuwa baadhi ya nchi zimepiga hatua kubwa katika
kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi za kimahakama, akitolea mfano wa
Italia ambapo wanawake wanawakilisha zaidi ya asilimia 52.9 ya Majaji.
Hata hivyo, alisema bado kuna nchi ambazo uwakilishi wa
wanawake katika Mahakama uko chini, akitolea mfano wa Iraq yenye takribani
asilimia 7.6 na Nepal yenye asilimia 3.8.
Kwa upande wa Tanzania, washiriki wa kongamano hilo
walieleza kuwa, kumekuwa na mafanikio makubwa katika kuongeza uwakilishi wa
wanawake katika ngazi mbalimbali za Mahakama.
Imeelezwa kuwa Mahakama ya Rufani tangu ilipoanzishwa mwaka
1979 ilianza na Majaji watano wote wakiwa wanaume, lakini kwa sasa idadi hiyo
imeongezeka na kufikia Majaji 37, ambapo wanaume ni 25 na wanawake ni 12, idadi
inayozidi asilimia 30 ya uwakilishi wa wanawake.
Aidha, katika Mahakama Kuu kuna jumla ya Majaji 104 ambapo
wanaume ni 65 na wanawake 39, wakati Mahakama za Hakimu Mkazi zina jumla ya
Mahakimu 1,434 ambapo wanaume ni 746 na wanawake 688 sawa na takribani asilimia
48.
Kwa upande wa Mahakama za Mwanzo, kuna Mahakimu 189 ambapo
wanaume ni 111 na wanawake 78 sawa na asilimia 41.
Kwa upande wa Zanzibar, Mahakama Kuu ina jumla ya majaji 14
ambapo wanaume ni tisa na wanawake watano sawa na asilimia 35, huku katika
ngazi ya mahakimu kukiwa na jumla ya Mahakimu 66 ambapo wanawake ni 23 na
wanaume 43.
Washiriki wa kongamano hilo walieleza kuwa takwimu hizo
zinaonesha wazi juhudi za Serikali katika kuhakikisha wanawake wanapata nafasi
katika ngazi mbalimbali za uongozi ndani ya Mhimili wa Mahakama.
Hata hivyo, walisisitiza kuwa pamoja na ongezeko hilo la
uwakilishi wa wanawake, bado kuna umuhimu wa kuhakikisha kuwa nafasi hizo
zinatumika ipasavyo kuimarisha utoaji wa haki na kuchangia kikamilifu katika
mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni