Jumanne, 10 Machi 2026

SUALA YA KUTOKOMEZA VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA LISHUGHULIKIWE KWA KUSHIRIKIANA; DKT. HOMERA

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (MB) amesema kuwa, Ukatili wa Kijinsia (GBV) si tu ukiukaji wa kisheria bali ni jeraha la kijamii linalokua kwa ukimya, hofu, pamoja na mila na desturi hatarishi kama vile ukeketaji hivyo ni jukumu la Majaji, Mahakimu wanawake na kila mmoja katika jamii kutokomeza vitendo hivyo na kuhakikisha haki inapatikana.

Akizungumza leo tarehe 10 Machi, 2026 wakati akifungua Kongamano Maalum la Kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake katika ukumbi wa ‘New Generation’ jijini Dodoma, Mhe. Dkt. Homera amesema kuwa Majaji na Mahakimu Wanawake si tu watekelezaji wa sheria, bali pia ni walinzi wa amani ya jamii na watetezi wa haki za binadamu.

Waziri huyo amesema, wakati waathirika wanapofika Mahakamani, wanabeba maumivu, aibu na mara nyingine kutokuwa na imani na wale wanaowazunguka, hivyo ameeleza, ninyi kama Majaji wanawake, uwepo wenu katika tasnia ya utoaji haki unatoa unatia faraja na kuleta tumaini la upatikanaji wa haki wanawake wengine walio tendewa vibaya.

Kwa upande wa Tanzania, Kaulimbiu ya maadhimisho hayo inasema, “Kutoka katika kuta za Mahakama hadi katika Jamii: Majaji Wanawake Wakiongoza Mapambano Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia,” Mhe. Dkt. Homera amesema kauli mbiu hiyo inaendana na kaulimbiu ya kimataifa inayosema: “Majaji Wanawake Ndani na Nje ya Mahakama: Wakilinda Upatikanaji wa Haki,”  

Waziri huyo amekipongeza Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) kwa kuipa uzito Siku ya Kimataifa ya Majaji Wanawake tangu mwaka 2023 baada ya Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa tarehe 26 Aprili 2021 huko Doha nchini Qatar.

Katika hatua nyingine, Mhe. Dkt. Homera ameupongeza uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa hatua kubwa ya mafanikio iliyopiga katika uboreshaji wa huduma za utoaji haki nchini.

‘Hapa napenda kutoa pongezi kwa Mahakama ya Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa George M. Masaju, Jaji Mkuu wa Tanzania, kwa mabadiliko makubwa yaliyoimarisha upatikanaji wa haki,’ amesema Waziri huyo.

Ameongeza kuwa, katika muda wangu mfupi tangu aanze majukumu yake Wizara Katiba na Sheria amevutiwa na maendeleo ya Mahakama katika suala zima la matumizi ya teknolojia katika utoaji wa haki ambapo amesema Mahakama imejizatiti kwa ajenda ya kisasa na mpango wa usikilizaji mashauri kwa njia ya Mahakama mtandao, ikitoka katika matumizi ya karatasi na kuelekea mfumo wa kidijitali.

Ametaja miongoni mwa mabadiliko yenye athari chanya kuwa ni pamoja na Mfumo wa kielektroniki wa kusajili na kuendesha Mashauri (JoT-eCMS) ambao umesaidia kuondoa ucheleweshaji wa usikilizwaji wa mashauri, kuongeza uwazi na kuimarisha usimamizi wa mashauri ya familia na ukatili wa kijinsia.

Waziri huyo amesema mabadiliko mengine ni uwepo wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs), ambapo ameeleza hadi sasa kuna vituo jumuishi zaidi ya tisa nchi nzima vilivyokwisha jengwa na vinavyoendelea kujengwa.

Ameongeza kwamba, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia  kilichopo Temeke mkoani Dar es Salaam kimetoa mafanikio makubwa ikiwa ni ushahidi wa maono ya Serikali kwa kushirikiana na Mahakama. Kwa mwaka 2025, Mahakama hiyo ilishughulikia mashauri zaidi ya 9,200, yakiwemo ya ukatili wa kijinsia na familia, lakini pia iliwezesha asilimia 61 ya wanawake kupata msaada wa kisheria jambo linaloonyesha wazi kuwa, zinapounganishwa huduma za Mahakama, Polisi, na Ustawi wa Jamii katika eneo moja, vizuizi vya upatikanaji wa haki kwa wanawake vinaanza kupungua.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Homera ameongeza mafanikio mengine ya Mahakam ani pamoja na kuwepo kwa Uwajibikaji Unaotegemea Takwimu kupitia mfumo wa kanzi data (Data Hub), Mahakama inaonesha jinsi inavyoshughulikia mashauri nyeti ya ukatili wa kijinsia (GBV) kwa wakati halisi na kuhakikisha mashauri hayo muhimu yanatatuliwa haraka.

Hata hivyo, Waziri huyo ametoa rai kwa Mahakama kuwa, panapo mafanikio hapakosi changamoto hivyo ni lazima iwe makini na changamoto zilizopo.

“Mnapaswa kushughulikia ubaguzi wa kidijitali, mnatakiwa kuipeleka haki hii hasa ya matumizi ya teknolojia katika hatua nyingine kwa kuhakikisha huduma hii si kwa watu wa mijini tu bali pamoja na watu walio pembezoni, vilevile ni muhimu kuhifadhi kumbukumbu nyeti za Mahakama kwa viwango vya juu vya ulinzi wa kanzi data ili kuepuka kuvujisha siri za waathirika,” ameeleza.

Ameihakikishia Mahakama kuwa, Wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na Mhimili huo kuhakikisha mifumo ya kisheria inaendana na ulinzi wa athari za teknolojia.

Kadhalika, Waziri huyo ameipongeza TAWJA na kuahidi kuendelea kuipa ushirikiano, kwa kuwa sehemu ya mabadiliko haya ya kidijitali kuwa ni mabadiliko yenye tija katika kutoa haki ya kijinsia.

“Mmepeleka sheria kutoka kwenye viunga vya Mahakama hadi kwenye jamii kwa kufanya yafuatayo, kuchangia katika uundaji na marekebisho ya sheria zinazolinda wanawake na watoto dhidi ya Ukatili wa Kijinsia (GBV), kuhakikisha sheria zetu ni za haki, jumuishi, na zinawalinda walioko hatarini,” amesema.

Jitihada nyingine zilizofanywa na Chama hicho ni pamoja na kupinga ubaguzi katika mali za ndoa na faragha kupitia sayansi ya sheria yenye msingi wa jinsia; kuwajengea uwezo wasichana na kuonesha kwamba uongozi katika tanuru la haki kupitia Mahakama unawezekana na kuandaa shughuli za jamii ili kuhakikisha Mahakama mtandao inafika hadi maeneo ya pembezoni ambayo ni maeneo ya vijijini.

Akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa Kongamano hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Mhe. Barke Sehel amesema hii ni mara ya tatu tangu Chama hicho kianze kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake.


Aidha, Mhe. Sehel ameshukuru kwa ushirikiano ambao wanapata kutoka Serikalini. Na vilevile alichukua fursa hiyo kumueleza Mhe. Dkt. Homera kuhusu Chama hicho na namna kinavyofanya kazi kwa kuwa ni mara yake ya kwanza kushiriki katika shughuli ya TAWJA.


"TAWJA ni Taasisi ya Kitaaluma isiyo ya Kiserikali na wala hatujihusishi na masuala ya siasa, yenyewe inawaleta pamoja Mahakimu na Majaji Wanawake kwa pande zote mbili Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar na wanachama wake wanatoka katika ngazi zote za Mahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo mpaka Mahakama ya Rufani na lengo kuu la Chama chetu  ni kukuza utawala wa sheria, kulinda haki za binadamu, kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa makundi yote...," amesema Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewapongeza Wanachama cha TAWJA na kusema kuwa anajivunia wanachama hao kwa kuwa ni watu makini.


"Pamoja na Ujaji na Uhakimu wenu, ninyi ni akina Mama, kila mwanadamu amezaliwa na mwanamke, mnafanya kazi kubwa sana," amesema Prof. Ole Gabriel.

Ameongeza kuwa, asilimia 80 ya tabia za watu zinatokana na wazazi, na kati ya asilimia hizo, Mama ana asilimia 64 ya kutengeneza tabia ya mtoto, hivyo mwanamke ni mtu muhimu katika ustawi wa jamii.

Kongamano hilo limehudhuriwa na Washiriki mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wanachama wa TAWJA kutoka matawi mbalimbali, Wjumbe Waalikwa wa TAWJA, Washirika wa Maendeleo na Wawakilishi wa Jamii ya Kiraia.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi  Homera (MB) akitoa hotuba wakati wa ufunguzi wa kongamano maalumu la kusherehekea siku ya kimataifa ya Majaji na Mahakimu wanawake (TAWJA) leo tarehe 10 Machi, 2026 katika ukumbi wa New Generation hall uliopo Kisasa jijini Dodoma.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi  Homera (Mb) akitoa hotuba wakati wa ufunguzi wa kongamano maalumu la kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake leo tarehe 10 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa New Generation hall uliopo Kisasa jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe.Barke Sehel akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa kongamano maalum la kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake  leo tarehe 10 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa New Generation hall uliopo Kisasa jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa salamu za Mahakama ya Tanzania wakati wa ufunguzi wa kongamano maalumu la kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake kwa upande wa TAWJA leo tarehe 10 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa New Generation hall uliopo Kisasa jijini Dodoma.

Sehemu ya Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu waliohudhuria sherehe ya Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wakati wa ufunguzi wa kongamano maalumu la kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA). Wa pili kulia ni Mhe. Joachim Tiganga, wa pili kushoto ni Mhe.Wilbert Martin Chuma na wa kwanza kushoto ni Mhe.Dkt Yose Joseph Mlyambina wakifuatilia mdahalo kwenye kongamano hilo.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa salamu za Mahakama ya Tanzania wakati wa ufunguzi wa kongamano maalum la kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake leo tarehe 10 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa New Generation hall uliopo kisasa jijini Dodoma.

Sehemu ya Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA) wakiwa wanafuatilia matukio mbalimbali ya ufunguzi wa kongamano maalumu la kusherehekea siku ya kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake leo tarehe 10 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa New Generation hall uliopo kisasa jijini Dodoma.

Sehemu ya Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wakiwa wanafuatilia matukio mbalimbali ya ufunguzi wa kongamano maalumu la kusherehekea Siku ya kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake leo tarehe 10 Machi, 2026 katika ukumbi wa New Generation hall uliopo Kisasa jijini Dodoma.


Sehemu ya Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA) wakiwa wanafuatilia matukio mbalimbali ya ufunguzi wa kongamano maalumu la kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake leo tarehe 10 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa New Generation hall uliopo Kisasa jijini Dodoma.

Sehemu ya Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wakiwa wanafuatilia matukio mbalimbali ya ufunguzi wa kongamano maalumu la kusherehekea siku ya kimataifa ya Majaji na Mahakimu wanawake (TAWJA) leo tarehe 10 Machi, 2026 katika ukumbi wa New Generation hall uliopo kisasa jijini Dodoma.

Sehemu ya Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu waliohudhuria sherehe ya Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA) wakati wa ufunguzi wa kongamano maalumu la kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake. katikati ni Mhe. Joachim Tiganga, wa pili kushoto ni Mhe.Wilbert Martin Chuma na kushoto ni Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina wakifuatilia mdahalo kwenye kongamano hilo.


Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi  Homera (Mb) (wa pili kulia) akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe.Barke Sehel (wa pili kushoto) wakati wa hafla hiyo. 

Meza Kuu ikiongozwa na Waziri wa Katiba na sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi  Homera (Mb) (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wanachama wa TAWJA ambao ni Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania waliohudhuria kongamano maalum la kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake.

Meza Kuu ikiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi  Homera (Mb) (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wanachama wa TAWJA ambao ni Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria kongamano maalum la kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake.
Meza Kuu ikiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi  Homera (Mb) (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Majaji Wafawidhi ambao ni walezi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) waliohudhuria kongamano maalumu la kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake.

Meza Kuu ikiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi  Homera (Mb) (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa TAWJA waliohudhuria kongamano maalum la kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake.

(Picha na INNOCENT KANSHA - Mahakama)

 
















Hakuna maoni:

Chapisha Maoni