- Wanawake mkoani humo waaswa kuchangamkia fursa zilizopo kuboresha uchumi wa familia na taifa letu
Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo aliwaongoza
wanawake wa Mahakama Kanda ya Kigoma kujumuika na wanawake wenzao waliojitokeza
wilayani Kakonko kwenye sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani
ambayo kimkoa ilifanyika katika Wilaya hiyo.
Mgeni Rasmi katika sherehe hizo zilizofanyika tarehe 08 Machi, 2026 alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mhe. Dinah Mathamani aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro.
Akizungumza na wanawake waliofika katika viwanja hivyo, Mhe. Mathamani, alisema kuwa, kupitia Kauli mbiu yam waka huu ya Siku ya Wanawake Duniani isemayo, "Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050," Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira rafiki yanayowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, uchumi na uongozi kupitia sera, programu na fursa mbalimbali za uwezeshaji.
Amewahimiza wanawake kwamba, wanao wajibu mkubwa wa kusimamia maadili ya familia na kulea kizazi kijacho na kwamba Serikali inaendelea kufungua fursa za kiuchumi na kuboresha miundombinu muhimu ya Afya, Elimu, Kilimo, Biashara na Uchukuzi katika kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Alieleza kuwa, uboreshaji wa huduma ya afya kutoka Hospitali za Wilaya na Halmashauri tatu, na kufikia tarehe 08 Machi zilikuwa nane sawa na asilimia 166.6, na Vituo vya Afya kutoka 34 mpaka kufikia 53 sawa asilimia 55.8, na kwa upande Shule za Sekondari awali zilikuwa 194 na sasa zipo 256 sawa na asilimia 31.9, ambapo shule za msingi awali zilikuwa 664 na sasa zimejengwa na kufikia 742 sawa asilimia 11.7.
“Hatua zote hizo zimeenda sambamba na ujenzi wa madarasa ya Shule za Sekondari kutoka 1,900 mpaka 3288 sawa na asilimia 70 na kwa Shule za Msingi vyumba vilikuwa 5401 na sasa tunaongea vyumba 6057 sawa na asilimia 12.1,” alisema Mkuu wa Wilaya huyo.
Aidha, aliongeza kwamba, kupitia Sera ya Taifa ya haki kwa wanawake na watoto wa kike inasisitiza umuhimu wa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kama njia ya kukuza usawa wa kijinsia na haki za wanawake hivyo maadhimisho hayo yanalenga kuongeza uelewa kuhusu changamoto zinazowakuta wanawake na wasichana kama vile unyanyasaji wa maneno, ukatili wa kijinsia, na ukosefu wa usawa wa kiuchumi.
Kadhalika maadhimisho hayo yanatambua
mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii na kukuza ushirikiano kati ya
wanawake na wanaume katika kufikia usawa wa kijinsia na Wanawake wametakiwa
kusimama imara katika kutetea haki na usawa wao na kuunga mkono juhudi za Serikali
katika kukuza haki za wanawake na wasichana.
Naye,
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Bi. Zainabu Buyogela alisema
kuwa, wanawake wanatakiwa kuchangamka na asiwepo hata mmoja anayekosa shughuli
inayompatia kipato ili watoe mchango wao katika uongozi na ujasiriamali
unaojitokeza katika maeneo yao, na kuwaonya wasichana wasiache kazi kwa ajili
ya kulinda ndoa au mahusiano.
Bi.
Zainabu alitumia fursa hiyo kumshukuru mwanamke nambari moja Tanzania ambaye ni
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kuongoza nchi kwa haki na usawa wa kijinsia.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Bw. Hassan Abbas Rugwa, alisema kuwa, Mkoa huo unaendelea kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo inayolenga kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuhakikisha wanapata fursa sawa katika uongozi, uamuzi na kushiriki shughuli za maendeleo.
Hata hivyo, Bw. Rugwa aliwahimiza wanawake kuwa wabunifu, kujiamini na kutumia maarifa waliyonayo ili kunufaika na fursa za mikopo, mafunzo ya ujasiriamali pamoja na nafasi za uongozi zinazopatikana katika jamii wanazotoka ili nao kuwa sehemu ya mafanikio katika nafasi hizo.
Aidha, aliwapongeza wanawake na
kuishukuru Serikali kuendelea kuweka sera na mikakati mbalimbali inayolenga
kuwainua wanawake kiuchumi, kijamii na kisiasa hatua inayochangia kuongeza
ushiriki wao katika maendeleo ya Taifa.
Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Valerian Tarimo (aliyevaa
sare ya kitenge) akiwa pamoja na Viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Kigoma katika sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wanamke Duniani iliyofanyika Wilaya ya Kakonko katika
viwanja vya Ofisi ya Kata ya Kasanda.
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mhe. Dinah
Mathamani akitoa hotuba yake wakati wa Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani zilizofanyika tarehe 08 Machi, 2026 katika viwanja vya ofisi ya kata ya Kasanda.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Bw. Abbas Rungwe akitoa neno katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Kata ya Kasanda Wilaya ya Kakonko.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania Mkoani Kigoma (UWT), Bi. Zainabu Buyogela akitoa neno wakati wa hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Kata ya Kasanda Wilaya ya Kakonko.
Wanafunzi wa Kidato cha Tano wa Shule ya Sekondari Mtendeli iliyopo Kata ya Kasanda wakitumbuiza mbele ya Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mhe. Dinah Mathamani (hayupo katika picha) wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Kata ya Kasanda Wilaya ya Kakonko.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni