Jumamosi, 4 Aprili 2026

BARAZA LA WAFANYAKAZI MAHAKAMA KANDA YA NJOMBE LAKETI

·  Jaji Nongwa awasihi Maofisa Utumishi kujali Maslahi ya Watumishi

Na ABDALLAH SALUM, Mahakama-Njombe

Baraza la Wafanyakazi Mahakama Kuu Kanda ya Njombe limefanya kikao chake huku Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Victoria Nongwa akiwaasa Maofisa Utumishi kujali maslahi ya watumishi walio chini yao hasa katika stahiki zao zinazohusu malimbikizo ya mishahara pamoja na posho wanazodai.

Kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi Mahakama Njombe kilifanyika tarehe 01 Aprili, 2026 ambapo Mhe. Nongwa alikuwa Mwenyekiti na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka Mkoa na Wilaya za Makete, Ludewa, Wanging’ombe lilikutana  kwa  ajili ya kujadiliana masuala mbalimbali ya kiutumishi pamoja na maslahi ya Wafanyakazi.

Jaji Nongwa alifungua kikao hicho kwa kusoma ajenda mbalimbali pamoja na kufanya  uchaguzi wa viongozi mbalimbali waliopendekezwa na wajumbe wa Baraza hilo  ambao walipigiwa kura huku Msimamizi wa Uchaguzi akiwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Njombe,  Mhe. Joseph Luambano.

Baada ya uchaguzi alipatikana Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Njombe, Mhe. Isack Mlowe na Naibu Katibu wa Baraza Kanda ya Njombe, Bi. Tumaini Jembe pamoja na Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa, Bw. Juma Nyenzi.

Wakati kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi la kinaendelea zilitolewa hoja mbalimbali zilizoibuka za watumishi ambazo zilihusu stahiki za wafanyakazi huku hoja nyingine zikijibiwa papo kwa hapo na hoja nyingine zikichukuliwa kwa ajili ya kwenda kuziwasilisha kwenye Baraza Kuu la Taifa la Mahakama ya Tanzania.

Mhe. Nongwa pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu Njombe, Bw. Richard Mbambe akiwa Katibu wa mpito wa Baraza la Wafanyakazi walihimiza Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) ambacho kiliwakilishwa na Kaimu Katibu wa TUGHE Mkoa wa Njombe, Bi. Zenaida Sanjo kutoa elimu kwa watumishi waliopo Mahakama za Mkoa wa Njombe na Mahakama za Wilaya Kanda hiyo juu ya umuhimu wa kujiunga na chama hicho.

Bi. Sanjo alitoa neno la shukrani kwa kushiriki katika mkutano huo na kutoa ahadi juu ya kuwapa elimu watumishi wote juu ya umuhimu wa kujiunga na TUGHE.

Aidha katika mkutano huo, lilifanyika zoezi kuchagua Mfanyakazi Bora wa Kanda ambapo lilifanyika kwa kushindanishwa kwa watumishi wawili waliokuwa na sifa za ufanyakazi bora wote kwa pamoja wakiwa na Vyeo vya Mwandishi Mwendesha Ofisi ambao walipigiwa kura kwa mara nyingine na hatimaye mtumishi mmoja Bi. Deodatha Mhagama alipita kwa kupata kura nyingi.

Kabla ya kufungwa kwa kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Njombe viongozi mbalimbali waliohudhuria walitoa neno la shukrani.

Jaji Mfawidhi  wa Mahakama Kuu ya Tanzania  Kanda ya Njombe na Mwenyekiti wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Kanda hiyo,  Mhe. Victoria Nongwa (katikati) akizungumza  na wajumbe wa kikao hicho waliohudhuria  (hawapo katika picha). Kulia ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Njombe, Mhe. Isack Mlowe na kushoto ni Naibu Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Kanda ya Njombe,  Bi. Tumaini Jembe.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Njombe,   Mhe. Joseph Luambano (kulia) akisimamia zoezi la kuesabu kura  za wajumbe waliopiga kura (hawapo katika picha). Katikati ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Ludewa Mjini, Mhe. Pius Ngosi Piusi  na  kushoto  Mtunza Kumbukumbu wa Mahakama ya Mwanzo Makambako, Bi. Aneth Mfikwa.


Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Njombe, Bw. Richard Mbambe akijibu hoja mbalimbali  za watumishi zilizoibuka kwenye kikao hicho hasa stahiki za watumishi wa Mahakama Kanda ya Njombe.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Tawi la Mahakama Mkoa wa Njombe, Bi. Happy Merere (kulia) akiwa na  Afisa Utumishi wa Mahakama ya Wilaya Njombe, Bi. Lusia Mpepo ambao ni Sekretarieti ya Mahakama Kuu Kanda ya Njombe wakisikiliza kwa umakini  hoja mbalimbali za kiutumishi  zilizokuwa zikitolewa kwenye kikao cha Baraza  la Wafanyakazi la Mahakama Kanda ya Njombe.

Kutoka upande wa kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama  ya Wilaya Njombe, Mhe. Matilda Kayombo, katikati ni Mtunza Kumbukumbu wa Mahakama ya Mwanzo Makambako, Bi. Aneth Mfikwa  na  kushoto  Kaimu Katibu wa TUGHE Mkoa wa Njombe, Bi. Zenaida Sanjo wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda  ya Njombe, Mhe. Victoria Nongwa (hayupo katika picha)  alipokuwa akizungumza katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama Kanda hiyo.


Sehemu ya wajumbe wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi Mahakama Kanda ya Njombe wakifuatilia kinachojiri katika kikao cha Baraza hilo. Aliyeketi nyuma kulia (mwenye miwani) ni Mwandishi Mwendesha Ofisi, Bi, Deodatha Mhagama  ambaye alipigiwa kura  na kushinda kwa kishindo kuchaguliwa kuwa Mtumishi Hodari/Bora wa Mahakama Kanda ya Njombe.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni