- Ni kufuatia usimamizi mzuri wa Miradi ya Ujenzi wa Mahakama
Na AIDAN ROBERT, Mahakama -Kigoma
Ujumbe wa Benki ya Dunia (WB) ukiongozwa na Kiongozi wa ujumbe huo, Bi. Christina Owuor umempongeza Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania (JDU), Mhe. Dkt. Angelo Rumisha baada ya kujionea maendeleo ya Miradi ya Ujenzi wa Mahakama za Mwanzo Bangwe, Heru juu na Manyovu walipoitembelea miradi hiyo hivi karibuni.
Ujumbe huo uliongozwa na Mhe. Dkt. Rumisha kufanya ukaguzi wa Ujenzi wa Miradi ya Mahakama za Mwanzo tatu (3) zinazojengwa mkoani Kigoma ili kuona maendeleo ya miradi hiyo.
Akitoa pongezi hizo, Kiongozi wa Ujumbe huo, Bi. Christina Owuor aliipongeza Mahakama ya Tanzania kupitia Kitengo cha Maboresho (JDU) kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo tatu zinazojengwa Kanda ya Kigoma.
“Mhe. Rumisha (Jaji), hongereni kwa ujenzi huu wa Mahakama hizi, nawapongeza sana kwa kuwa mmehakikisha ubora wa vifaa vya ujenzi vilivyotumika kujenga majengo haya ni vya kiwango kizuri sana na kwa kupitia ubora wa miradi hii, nadhani tutafikiria kuendelea kutoa miradi mingine kwenu maana mmeonesha thamani ya fedha imeonekana katika miradi hii ya Kanda ya Kigoma,” alisema Bi. Owuor.
Naye Jaji Rumisha alisema, “napokea pongezi hizi kubwa mlizotupatia kwa usimamizi bora wa ujenzi wa miradi hii mitatu, hakika tunashukuru kwa pongezi hizi kwani usimamizi wa miradi hii una weledi mkubwa wa watalaam wetu kusimamia kila hatua na ndio matokeo ya ufanisi huu wa miradi hii, aidha, nami niwapongeze wataalam wetu kwa kutumia vema utalaamu wao kwa tija ya Taasisi yetu.”
Kwa upande wake, Mkandarasi Mshauri Mwelekezi, Bw. Norman & Dawbarn aliwasilisha taarifa yake kuwa, ujenzi huo umefikia asilimia 98 kwa Mahakama zote tatu (3) na kwamba kwa sasa zinasubiriwa samani za ofisi ili majengo hayo yaweze kuanza kutoa huduma haraka iwezekanavyo.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ndogo ya Kigoma, Bw. Yusuph Mhoja alitoa shukrani zake kwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Maboresho, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha na kwa ujumbe wa Benki ya Dunia kufika mkoani humo kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo kwani tegemeo la wananchi wa Mkoa wa Kigoma ni kupata huduma karibu ili kuwapunguzia baadhi ya gharama za usafiri wanazozitumia kwa sasa kwenda kupata haki zao mahakamani.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania (JDU), Mhe. Dkt. Angelo Rumisha (wa kwanza kulia) akitoa maelekezo kwa Mkandarasi kumaliza haraka ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Bangwe Kigoma. Wa kwanza kushoto ni Kiongozi wa ujumbe kutoka Benki ya Dunia (WB), Bi. Christina Owuor.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo
cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania (JDU), Mhe. Dkt. Angelo Rumisha akitoa maelekezo kadhaa ya kiukaguzi kwa Wakandarasi katika umaliziwaji wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Heru Juu, akiwa
na Wajumbe wa Benki ya Dunia pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu.
Ukaguzi Mahakama ya Mwanzo Heru Juu-Kigoma
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha (aliyenyoosha mkono) akisema neno baada ya kupokea pongezi kutoka kwa Kiongozi wa Ujumbe wa Benki ya Dunia kufuatia ubora wa ujenzi uliofanyika kwenye miradi yote ya Mahakama Mwanzo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania (JDU), Mhe. Dkt. Angelo Rumisha (mbele) Viongozi kutoka Benki ya Dunia pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kigoma Bw. Yusufu Mhoja (aliyevaa koti la rangi la kijivu) na watumishi wa Mahakama hiyo wakikagua Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Heru Juu.
Picha ya pamoja katikati ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ya Tanzania (JDU), Mhe. Dkt. Angelo Rumisha (katikati). Wa pili kulia ni Kiongozi wa Ujumbe kutoka Benki ya Dunia (WB), Bi. christina Owuor, wa pili kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Bw. Yusuph Kasuka, wa kwanza kushoto ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kasulu, Mhe. Imakulata Shuli, na wengine ni Viongozi na wajumbe kutoka Benki ya Dunia pamoja na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Heru Juu.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni