Ijumaa, 24 Aprili 2026

‘USIKILIZAJI, UMALIZAJI HARAKA WA MASHAURI UNA MCHANGO MKUBWA KWA TAIFA KIUCHUMI, KIJAMII’

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema leo tarehe 24 Aprili, 2026 kuwa, usikilizaji na umalizaji wa haraka wa mashauri yaliyopo mahakamani una mchango mkubwa kwa Taifa kiuchumi na kijamii

Akiwasilisha bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Mhe. Dkt. Homela ameeleza pia kuwa suala la kuharakisha usikilizaji wa mashauri mahakamani ni moja ya vipaumbele muhimu vya Mahakama ya Tanzania katika kuhakikisha kuwa Wananchi wote wanapata haki kwa wakati.

Ameliambia Bunge kuwa katika kipindi cha Julai, 2025 hadi Machi, 2026, kulikuwa na jumla ya mashauri 205,038 mahakamani na kati ya hayo, 45,187 yalianza mwaka 2024/ 2025, yaani yalikuwepo kabla ya tarehe 30 Juni, 2025, na mashauri 159,851 yalifunguliwa katika mwaka wa fedha 2025/2026.

“Kati ya mashauri 205,038 yaliyokuwepo, mashauri 166,553 yalisikilizwa na kuhitimishwa na mashauri 38,485 yanaendelea katika hatua mbalimbali. Aidha, mashauri yenye umri mrefu mahakamani ni 3,675,” Waziri Homela amesema.

Amebainisha kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, kasi ya uondoshaji wa mashauri mahakamani (case clearance rate) ni asilimia 104, huku uwezo wa umalizaji wa mashauri (disposal rate) ni asilimia 81.

Akizungumzia mchango wa usikilizaji na umalizaji wa haraka wa mashauri mahakamani kwa Taifa kiuchumi na kijamii, Waziri Homela ameeleza kuwa katika zoezi maalum la kusikiliza mashauri ya kiuchumi na kibiashara lililofanywa na Mahakama Oktoba na Novemba, 2025 lilifanikisha umalizaji wa mashauri 2,973.

“Kuhitimishwa kwa mashauri hayo kuliwezesha kuachilia jumla ya shilingi za Kitanzania trilioni 13.1 zilizokuwa zimeshikiliwa na mashauri hayo kuingia kwenye mzunguko wa uchumi,” amesema.

Akizungumzia ukaguzi na usimamizi wa shughuli za kimahakama katika ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo kwa Masjala Ndogo 20 za kimahakama, Mhe. Dkt. Homela amesema kuwa zoezi hilo limefanyika kwa asilimia 100.

“Matokeo ya ukaguzi huo yamewezesha kuongeza kasi ya umalizaji mashauri mahakamani kwa kuwa huambatana na ukaguzi wa jalada moja baada ya jingine,” Waziri Homela ameliambia Bunge wakati anawasilisha hotuba yake.

Ameeleza vilevile kuwa Magereza 129 kati ya 130 yaliyopo yalikaguliwa, sawa na asilimia 98.8 ikilinganishwa na ukaguzi wa kipindi kama hiki katika mwaka 2024/2025 uliofanyika kwa asilimia 80.2.

Waziri pia ameeleza kuwa katika mwaka 2025/2026, Mahakama ya Tanzania imeendelea kushirikiana na Wadau wake katika mnyororo wa haki jinai ili kuhakikisha mashauri yanamalizika kwa wakati.

Amebainisha kuwa tarehe 12 na 13 Machi, 2026 Mahakama iliitisha kikao kazi cha pamoja kilichohusisha Wadau kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Waziri Homela ametaja Wadau wengine waliohudhuria kikao kazi hicho kama Chama cha Wanasheria Tanganyika, Idara ya Ustawi wa Jamii, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza pamoja na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.

“Kupitia kikao hicho, wajumbe walijadili taarifa ya hali ya mashauri ya mlundikano hadi kufikia Desemba, 2025, hali ya mahabusi magerezani na mikakati ya kupunguza mlundikano pamoja na kuongeza matumizi ya TEHAMA kwenye usikilizaji wa rufaa na maombi,” amesema.

Kwa mujibu wa Mhe. Dkt. Homela, kikao hiki kimesaidia kupata ufumbuzi wa pamoja wa changamoto mbalimbali, ikiwemo kuongeza kasi ya umalizaji wa 36 mashauri mahakamani, na kila mdau kutekeleza wajibu wake kwa wakati.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, akiwasilisha bungeni jijini Dodoma Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027.


Viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia uwasilishaji wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria bungeni kuhusu mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

 

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likiendelea na shughuli zake jijini Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni