Ijumaa, 24 Aprili 2026

MAGEUZI YA SEKTA YA SHERIA KUIMARISHA MAHAKAMA, IJA LUSHOTO

Na HALIMA MNETE- Mahakama, Dodoma

Serikali imeendelea kuimarisha Mhimili wa Mahakama pamoja na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, katika jitihada za kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati, kwa usawa na kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria.

Akiwasilisha bungeni mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2026/2027 leo tarehe 24 Aprili, 2026, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera, amesema mageuzi yanayoendelea yanalenga kuifanya Mahakama kuwa Mhimili imara unaochochea maendeleo ya Taifa.

Aidha, Waziri Homela amelieleza Bunge jijini Dodoma kuwa katika jitihada za kuimarisha mifumo ya utoaji haki, Serikali pia imeendelea kuboresha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kupitia mifumo kama Mahakama Mtandao na e-CMS, ambayo imerahisisha usikilizaji wa mashauri na upatikanaji wa nyaraka kwa wakati.

Kwa upande wa elimu na mafunzo, amesema kuwa IJA imeendelea kuwa kitovu muhimu cha kujenga uwezo wa watendaji wa Mahakama. Kupitia chuo hicho, mafunzo ya kitaaluma na kiutawala yamekuwa yakitolewa ili kuongeza ufanisi, maadili na weledi katika utoaji haki.

Aidha, Waziri Homela ameeleza kuwa IJA imeendelea kushiriki katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kusogeza huduma za haki karibu na jamii, hususan kwa makundi yenye uhitaji.

Sambamba na hayo, Serikali imeendelea kuhimiza matumizi ya mbinu mbadala za utatuzi wa migogoro (ADR) ili kupunguza mzigo wa mashauri mahakamani na kuharakisha upatikanaji wa haki bila urasimu mrefu.

Katika hotuba hiyo, Waziri Homera alitoa shukrani za kipekee kwa uongozi wa Mhimili wa Mahakama kwa mchango wao katika kuimarisha utoaji wa haki nchini.

Aidha, amempongeza Mhe. George Masaju kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania. Uteuzi wake unadhihirisha umahiri na uzoefu alionao katika Sekta ya Sheria kwa ujumla, ikiwemo Mhimili wa Mahakama.

Katika hotuba hiyo, Mhe. Homera ametoa pia shukrani za kipekee kwa uongozi wa mhimili wa Mahakama kwa mchango wao katika kuimarisha utoaji wa haki nchini. Amewataja Viongozi wengine wa juu wa Mahakama akiwemo Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha IJA, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Prof. Elisante Ole Gabriel, na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya.

Mhe. Homera alisisitiza kuwa uongozi huo umeendelea kuwa nguzo muhimu katika mageuzi ya kimfumo ndani ya sekta ya sheria na kuongeza imani ya Wananchi kwa vyombo vya utoaji haki. “Sekta ya Sheria siyo tu msimamizi wa sheria pekee, bali ni injini ya uthabiti wa Taifa na kichocheo cha maendeleo ya uchumi katika kufikia malengo ya DIRA 2050.”

Waziri Homera alieleza kuwa uongozi huo umekuwa mstari wa mbele kusukuma mageuzi ya kimfumo ndani ya Mahakama, hususan katika kuongeza matumizi ya teknolojia, kuboresha usimamizi wa mashauri na kuimarisha uwajibikaji.

Alisisitiza kuwa mchango wa viongozi hao umeendelea kujenga imani ya Wananchi katika Mhimili wa Mahakama na kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na kwa usawa.

Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha Mahakama pamoja na Taasisi zake ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wote, kwa wakati na kwa usawa, ikiwa ni msingi muhimu wa amani, utulivu na maendeleo ya Taifa.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera akionesha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Picha chini, akisoma hotuba ya bungeni Dodoma kuhusu mpango na makadirio hayo.


Viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia uwasilishaji wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria bungeni kuhusu 
mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni