Alhamisi, 23 Aprili 2026

MAHAKAMA MOROGORO YATOA MAFUNZO KUHUSU MFUMO WA KUHIFADHI MWENENDO MAHAKAMA ZA MWANZO

Na ASHA JUMA- Mahakama Morogoro.

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Morogoro, imeendesha mafunzo maalumu kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo pamoja na Makarani kuhusu matumizi ya mfumo wa kuhifadhi mienendo, vielelezo na hukumu ikiwa ni sehemu ya kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji haki.

Mafunzo hayo yalifanyika jana tarehe 22 Aprili, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano uliopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Morogoro, sambamba na njia ya mtandao (online) ili kuwezesha ushiriki mpana.

Mafunzo hayo yaliendeshwa na kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Morogoro, kikiongozwa na Mkuu wa Kitengo hicho pamoja na Mwanzilishi wa mfumo huo, Bw. Justine Kemhe. Aidha, mafunzo hayo yalifunguliwa rasmi na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Morogoro, Mhe. Amiri Msumi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Msumi alikishukuru kitengo cha TEHAMA kwa ubunifu wao katika kuanzisha mfumo huo unaoitwa unaoitwa Primary Court Depository, akieleza kuwa ni hatua muhimu katika kuboresha utendaji kazi wa Mahakama. Pia aliwahimiza washiriki kutoa ushirikiano wa kutosha pale changamoto zitakapojitokeza ili kuhakikisha mfumo unaboreshwa zaidi.

“Hongereni sana kwa kutafsiri mawazo ya watu na kuyaweka katika utekelezaji. Nawasihi Mahakimu na watumiaji wote wa mfumo huu kuwasilisha changamoto na maoni yao ili kuboresha mfumo huu,” alisema Mhe. Msumi.

Mfumo wa Primary Court Depository ni sehemu ya jitihada za kuendeleza matumizi ya TEHAMA katika Mahakama ya Tanzania. Mfumo huu unasaidia kurahisisha upatikanaji wa mienendo ya mashauri kutoka Mahakama za Mwanzo pamoja na kuhifadhi kumbukumbu hizo kidijitali, hivyo kupunguza usumbufu wa kutafuta nyaraka kwa njia za kawaida.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA alibainisha umuhimu wa kuongeza vifaa vya TEHAMA kama kompyuta na skana ili kuhakikisha mfumo huo unafanya kazi kwa ufanisi zaidi. Aliongeza kuwa mfumo huo tayari umeanza kutumika katika baadhi ya Masjala nyingine, zikiwemo Simiyu na Geita.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi  wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Janeth Kinyage, alisisitiza umuhimu wa washiriki kuzingatia maelekezo waliyopewa wakati wa mafunzo hayo, akieleza kuwa mfumo huo utarahisisha kazi na kuondoa changamoto ya upatikanaji wa mienendo ya mashauri.

Mafunzo haya yanatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika utendaji kazi wa Mahakama za Mwanzo kwa kuongeza ufanisi, uwazi na uhifadhi bora wa kumbukumbu za mashauri kwa njia ya kisasa (kidijitali).

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Morogoro, Mhe.Amiri Msumi, akifungua mafunzo hayo.

Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA pamoja na Mwanzilishi wa mfumo huo, Bw. Justine Kemhe, akitoa mafunzo juu ya mfumo wa Primary Court Depository.

Mahakimu  pamoja na Makarani wakifuatilia mafunzo hayo kwa njia  ya mtandao na njia ya kawaida.


Habari hii imehririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.


 


 


 

  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni