Na WAANDISHI WETU, Mahakama -Serengeti Mara
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. George Masaju, amewataka waumini wa Kanisa la Waadventista Wa Sabato na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kuwa wanyenyekevu hata baada ya kubarikiwa na kupata mafanikio, hivyo wanapaswa kuendeleza uhusiano wao mzuri na Mungu.
Mhe. Masaju ameyasema hayo akiwa Mgeni Maalum katika Hafla ya Ufunguzi wa Kanisa la Waadventista Wa Sabato Musati Central na Harambee ya Ujenzi wa Shule pamoja na Zahanati, iliyofanyika leo tarehe 18 Aprili, 2026 katika Kijiji cha Musati Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
“Ninayo furaha kubwa sana leo kukutana nanyi, jambo hili ni kubwa wengi wetu Mungu anapotubariki tunakuwa na kiburi kwahiyo hatua hii inaonesha jinsi ambavyo Mhe. Dkt. Nyansaho alivyo mnyenyekevu,”amesema Jaji Mkuu.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mhe. Masaju ametoa pongezi kwa waumini wa kanisa hilo pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho, ambao kwa dhati wameshiriki katika ujenzi wa kanisa hilo sambamba na kuendesha zoezi la kuchangia ujenzi wa shule na zahanati kijijini hapo.
Aidha, Jaji Mkuu amesisitiza kuhusu umuhimu wa kufanya kazi na kuwataka watu wafanye kazi kwa bidii wakijishughulisha na shughuli halali kama kilimo, uvuvi na ufugaji huku wakiilinda amani kwa sababu amani ikitoweka watu hawataweza kufanya shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.
Ameongeza kuwa uwepo wa kanisa hilo utasaidia katika kujenga jamii yenye umoja na amani kwani maovu yatakemewa jambo litakalohakikisha uwepo wa amani, usalama, ulinzi wa maadili pamoja na ulinzi wa mila na desturi za Kitanzania.
Kanisa hilo ambalo limezinduliwa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Hamis Ulega (MB) ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla hiyo.
Ujenzi wa Kanisa hilo umegharimu kiasi cha shilingi za kitanzania milioni 500.
Aidha katika Hafla hiyo, imeendeshwa harambee maalum ya kuchangia ujenzi wa Shule pamoja na Zahanati ambapo Jaji Mkuu ameshiriki pia kuchangia katika zoezi hilo.
Pamoja na Jaji Mkuu hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Hamis Ulega (MB), aliyekuwa Mgeni Rasmi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob John Mkunda, Wakuu wa Mikoa ya Mara na Tabora, Wakuu wa Wilaya za mkoani Mara, baadhi ya Wabunge wa Mkoa wa Mara, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya, Madiwani, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Viongozi mbalimbali na Wananchi kwa ujumla ambao mwenyeji wao alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho.
Mgeni Rasmi Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega (MB) (wa nne kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kanisa la Waadventista Wasabato Musati Central na Harambee ya Ujenzi wa Shule pamoja na Zahanati leo tarehe 18 Aprili, 2026 Mugumu Wilaya ya Serengeti mkoani Mara. Kushoto kwake ni Mgeni Maalum Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju, mwenye shati jeupe ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho pamoja na Viongozi wengine walioshiriki katika hafla hiyo.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Kanisa la Waadventista Wasabato Musati Central na Harambee ya Ujenzi wa Shule pamoja na Zahanati leo tarehe 18 Aprili, 2026 Mugumu Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.



















Hakuna maoni:
Chapisha Maoni