Jumamosi, 18 Aprili 2026

MAHAKAMA DAR ES SALAAM YAOKOA ZAIDI YA MILIONI 60 KUTOKA KATIKA MATUMIZI YA KARATASI

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imefanya tathmini ya matumizi ya karatasi na matumizi ya kieletroniki na kubaini kuwa, imefanikiwa kuokoa zaidi ya Shilingi Milioni 64.

Hayo yamebainishwa jana tarehe 17 Aprili, 2026 katika Kikao cha Menejimenti ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo ni moja ya Yatokananyo ya kikao kilichofanyika tarehe 18 Julai, 2025 ambapo moja ya maazimio ilikuwa ni kutathmini gharama zilizokuwa zinatumika kununua karatasi, wino pamoja na kalamu kabla ya Mahakama kuachana na matumizi ya karatasi (paperless) na kutumia njia ya mtandao.

Akitoa mchanganuo Mahakama Kuu pekee, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Sumera Manoti amesema Mahakama hiyo imefanikiwa kuokoa shilingi 21,418,724/= kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam imeokoa shilingi 21,496,555/= ikijumlisha na Mahakama zake zote za Wilaya yaani Ilala, Temeke na Kigamboni.

Kwa upande wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Bw. Manoti amesema imefanikiwa kuokoa shilingi 16,653,508 pamoja na Mahakama zake za Wilaya yaani Kinondoni na Ubungo.

Ameongeza kuwa, Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani imeokoa kiasi cha shilingi 9,200,000/= pamoja na Mahakama zake za Wilaya yaani Kibaha, Bagamoyo, Kisarawe, Mkuranga, Rufiji, Kibiti na Mafia.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amewapongeza Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Kanda hiyo na kueleza kuwa, amepokea pia pongezi kutoka Gereza la Mahabusu Segerea kwa utendaji kazi mzuri wa Kanda hiyo na kueleza kuwa, pongezi hizo sio zake ni za Wafawidhi maana wao ndio wana mashauri hayo na wamejitahidi kuyaondoa. Pamoja na pongezi hizo amewataka kukaa kwa amani.

Aidha, Mhe. Maghimbi amewatahadharisha wajumbe hao kuwa kuna viashiria vya mlundikano wa mashauri kukaribia hivyo, amewaomba kujitahidi kuyafanyia kazi mashauri hayo ili kuondokana na mlundikano ambao umekuwepo kipindi cha nyuma lakini kwa juhudi na mshikamano walifanikiwa kuyaondoa kabisa hivyo yasije kurudi tena. 

“Mwanzo wa mwaka waanze ndio wakati wa kupanga mikakati jinsi gani umeyazuia, unayachukua hayo yenye viashiria unayafanyi kazi vikao vya kuyasukuma ili mmalizane nayo,” alisema Jaji Maghimbi.

Katika jitihada za kuhakikisha huduma za Mahakama zinasogezwa karibu na wananchi, Jaji Mfawidhi huyo amewataka Wafawidhi kupitia Uongozi wa Serikali za vijiji kuomba kupatiwa viwanja vya kujenga Mahakama za Mwanzo kwa Kata zilizopo katika maeneo yao. Baadhi ya Wilaya ambazo tayari zimeshapata viwanja. Mhe. Maghimbi amewataka kufuatilia hati za maeneo hayo.

Sambamba na kikao hicho wajumbe wamepata fursa ya kujifunza kuhusu Mfuko wa Wekeza Maisha (UTT AMIS) na kujua faida zinazopatikana kupitia mfuko huo.

Miongoni mwa maazimio ya kikao hicho ni pamoja na kuandaa  ya uandishi wa muhtasari  wa vikao, Dira ya Taifa ya 2050 na huduma kwa wateja kwa Maofisa Mahakama Kanda ya Dar es Salaam, Kanda kuandaa mafunzo maalum kwa Maofisa  wa Mahakama  kwa ajili ya kuwajengea uwezo katika kusikiliza mashauri na uandishi wa hukumu, Mahakimu Wafawidhi kuwajulisha Mahakimu walio chini yao pamoja na Watendaji juu ya umuhimu wa  takwa la kisheria la kufungua akaunti maalum ya Mirathi, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya, Maofisa Utumishi na Maofisa Tawala kufuatilia upatikanaji wa viwanja na hati kwa ajili ya Kata ambazo hazina Mahakama za Mwanzo.

Wajumbe wa Kikao cha Menejimenti cha Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam  wakifuatilia kikao hicho kilichofanyika jana tarehe 17 Aprili, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni.

Baadhi wa wajumbe wa kikao cha Menejimenti wakifuatilia somo kwa meneja masoko wa mfuko wa uwekeza wa Pamoja (UTT) Bi. Paskazia Charles (hayupo pichani).


Meneja Masoko wa Mfuko wa Wekeza Maisha (UTT) Bi. Pakazia Charles  akiwapa somo wajumbe wa Kikao cha Menejimeneti cha Mahakama Kanda ya Dar es Salaam.


 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kikao cha Menejimenti, Mhe. Salma Maghimbi (katikati), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam, Mhe. Livin Lyakinana (kushoto) na Mtendaji wa Mahakama Kuu kanda ya Dart es Salaam, Bw. Sumera Manoti wakiwa katika kikao hicho.

Meza kuu wakiwa na katika picha ya pamoja na Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Kutoka kushoto waliosimama ni Mhe. Aziza Mbadjo, Mhe. Hussein Mushi na  Mhe. Franco Kiswaga. 

 Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Kada mbalimbali wa Makhakama Kanda ya Dar es Salaam ambao ni wajumbe wa Kikao cha Menejimenti.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Mara)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni