Ijumaa, 17 Aprili 2026

MAHAKAMA KUU MASJALA NDOGO SIMIYU YASHIRIKI MAADHIMISHO YA WIKI YA USULUHISHI

  •   Yawaelimisha Wadau wa Mahakama umuhimu wa Usuluhishi kupitia Kongamano maalum

Na NAUMI SHEKILINDI, Mahakama-Simiyu

Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ndogo ya Simiyu nayo imeungana pamoja na Mahakama nyingine nchini kuadhimisha Wiki ya Usuluhishi nchini ambayo iliyoanza tarehe 14 Aprili, 2026 na kufikia tamati tarehe leo tarehe 17 Aprili, 2026.

Katika Maadhimisho hayo, Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Simiyu imefanikiwa kufanya kongamano la Usuluhishi tarehe 16 Aprili, 2026 likiongozwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Hussein Mtembwa pamoja na wadau mbalimbali wa Mahakama wakiwemo Watumishi wa Mahakama, Polisi, Taasisi za kibenki, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Uhamiaji, Wakala wa Vipimo, TUGHE, Viongozi wa dini na wananchi.

 Mhe. Mtembwa alifungua kongamano hilo na kueleza kuwa lengo la Wiki ya Usuluhishi ni kupunguza muda wa mashauri mahakamani, kupunguza gharama za mashauri na kuwezesha suluhu ya haraka na ya kirafiki, “Mfano benki wanapofanya usuluhishi baina ya benki na mteja inajenga mahusiano mema na ya kirafiki baina ya benki na mteja” amesisitiza Jaji Mtembwa.

Aidha, Mhe. Mtembwa aliongeza kwa kusema, “Haki sio tu kuhukumu bali pia kusuluhisha,” alieleza kuwa usuluhishi una mchango mkubwa katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwani amani, usalama na utulivu ndio msingi utakaojenga umoja ndani ya nchi, vilevile Mahakama imejipanga kukuza dhana ya usuluhishi kama ilivyo kwenye Ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, (1977) na kwamba ana imani kongamano hilo litaleta tija kwa jamii.

Naye, Naibu Msajili Mfawidhi, Mhe. Elimo Daniel Massawe alitoa mada juu ya usuluhishi wa migogoro ya Tanzania ambapo alieleza maana ya usuluhishi, lengo, faida zake pamoja na mbinu za kufanya usuluhishi.

Mhe. Massawe alieleza kwamba, usuluhishi ni sehemu rasmi ya mfumo wa sheria unaotambuliwa na taratibu za Mahakama nchini, pia ni utaratibu unaowapa wahusika nafasi ya kusuluhisha mgogoro wao kwa hiari na kwa msaada wa mtu wa kati asiye na upendeleo, lakini pia mpatanishi sio mtoa uamuzi bali wahusika ndio wenye mamlaka ya mwisho.

Wakati wa kuhitimisha kongamano hilo, Kaimu Jaji Mfawidhi alisema kuwa, kongamano hilo litakua chachu katika kuimarisha usuluhishi na kuwaomba wadau waende kuwa Mabalozi wa Usuluhishi  kabla ya wadaawa kufika Mahakamani.

   Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Simiyu, Mhe. Hussein Mtembwa akifungua Kongamano la Usuluhishi kwa wadau waliohudhuria kongamano hilo lililofanyika tarehe 16 Aprili, 2026 katika Mahakama hiyo.


Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Simiyu, Mhe. Elimo Daniel Massawe akitoa mada juu ya Usuluhishi kwa wadau waliohudhuria Kongamano hilo.

   Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo Simiyu, Mhe. Elimo Massawe (aliyesimama) akimkaribisha Kaimu Jaji Mfawidhi, Mhe. Hussein Salum Mtembwa (katikati) kuzungumza  na wadau wakati wa Kongamano hilo.

    Wadau mbalimbali waliohudhuria kongamano wakisikiliza mada kutoka kwa Mhe. Elimo Daniel Massawe, Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Simiyu.

   Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Simiyu, Mhe. Hussein Mtembwa (katikati mstari wa mbele ) akiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali aliohudhuria Kongamano la Usuluhishi katika Mahakama Kuu Masjala ndogo Simiyu.


(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Mara) 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni