Ijumaa, 17 Aprili 2026

Hitimisho Wiki ya Usuluhishi Dodoma

WATUMISHI IJC DODOMA WANUFAIKA NA MAFUNZO YA USULUHISHI

Na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama Kuu, Dodoma

Watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma wamepatiwa mafunzo maalum yanayohusu matumizi ya usuluhishi katika kushughulikia migogoro ya kiutawala na kikazi, ikiwa ni sehemu ya hitimisho la Wiki ya Usuluhishi kwenye Mahakama hiyo.

Mafunzo hayo yamefanyika leo tarehe 17 Aprili, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano, kuhitimisha Maadhimisho ya Wiki ya Usuluhishi. Mafunzo hayo yalilenga kuimarisha ufanisi kazini na kujenga utamaduni wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo.

Mafunzo hayo yalisimamiwa na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma na Mratibu wa Wiki ya Usuluhishi, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan, ambaye ametoa elimu ya kina kuhusu dhana nzima ya usuluhishi na matumizi yake katika mazingira ya kazi.

Amesisitiza kuwa usuluhishi ni nyenzo muhimu katika kuongeza tija, kuimarisha mahusiano ya kikazi na kupunguza migogoro isiyo ya lazima katika Taasisi za umma.

Mafunzo hayo yaliwashirikisha pia Viongozi wa Dini ambao walitoa mchango mkubwa katika kuelezea nafasi ya usuluhishi kwa mtazamo wa kidini.

Kwa upande wa dini ya Kikristo, Bw. Ford Saileni alitoa mafundisho yaliyolenga kuhimiza amani, msamaha na maridhiano kama msingi wa kutatua migogoro.

Aidha, kwa upande wa dini ya Kiislamu, Ustadh Bwana Haji kutoka Masjid Sunni Nunge Dodoma alieleza umuhimu wa suluhu (usuluhishi) kama sehemu ya mafundisho ya dini, akisisitiza haki, uvumilivu na maelewano katika jamii.

Mafunzo hayo hayakuwa ya kawaida, bali yalipambwa na shamrashamra mbalimbali zilizoongeza hamasa kwa washiriki. Vipengele vya maigizo vilivyowasilishwa na baadhi ya Watumishi pamoja na Wasanii walioalikwa vilionyesha kwa vitendo namna usuluhishi unavyoweza kutumika katika kutatua migogoro kwa njia ya kirafiki na yenye tija.

Watumishi walioshiriki walionesha kufurahishwa na mafunzo hayo, wakieleza kuwa yamewajengea uelewa mpana zaidi na kuwapa mbinu bora za kushughulikia changamoto za kikazi. Walibainisha kuwa elimu hiyo ina manufaa makubwa katika kuboresha utendaji wao pamoja na kuimarisha mshikamano kazini.

Kwa ujumla, mafunzo hayo yameacha alama chanya kwa Watumishi wa IJC Dodoma, yakionesha wazi umuhimu wa usuluhishi katika kujenga mazingira bora ya kazi na utoaji haki wenye ufanisi zaidi.

Ikumbukwe kuwa Wiki ya Usuluhishi nchini yalizinduliwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju, tarehe 13 Aprili, 2026. Maadhimisho hayo yalienda sambamba na kaulimbiu isemayo, “Kutumia Njia Mbadala ya Utatuzi wa Migogoro kama Mbinu Inayopendelewa ya Kutatua Migogoro nchini Tanzania.”

Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, ambaye pia ni Mratibu wa Wiki ya Usuluhishi, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan (aliyesimama) akizungumza wakati wa kutoa mafunzo ya usuluhishi kwa Watumishi wa Mahakama IJC Dodoma.

Mchungaji Ford Saileni (aliyesimama) akiwasilisha mada ya usuluhishi kwa upande wa dini ya kikristo katika mafunzo ya watumishi wa IJC Dodoma.

 

Ustadhi Mbwana Haji akiwasilisha mada ya usuluhishi kwa upande wa Kiislamu wakati wa mafunzo ya usuluhishi kwa watumishi wa Mahakama wa IJC Dodoma.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, ambaye pia ni Mratibu wa Wiki ya Usuluhishi, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo kutoka Wizara ya Katiba na Sheria. Waliokaa kushoto kwake ni Ustadh Mbwana Haji kutoka Masjid Sunni Nunge Dodoma na kulia kwake ni Mchungaji Ford Saileni.


 Meza Kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, ambaye pia ni Mratibu wa Wiki ya Usuluhishi, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo ambao Maofisa Usafirishaji wa IJC Dodoma. Waliokaa kushoto kwake ni Ustadh Mbwana Haji kutoka Masjid Sunni Nunge Dodoma na kulia kwake ni Mchngaji Ford Saileni.

 

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, ambaye pia ni Mratibu wa Wiki ya Usuluhishi, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki na wakufunzi wa mafunzo hayo ambao ni Mahakimu, Mawakili pamoja na Watumishi (waigizaji) waliopamba mafunzo hayo ya usuluhishi kwa watumishi.


Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni