WANAFUNZI UDOM WAPATA ELIMU KUHUSU USULUHISHI
Na
ARAPHA RUSHEKE-Mahakama Kuu, Dodoma.
Katika kuendelea kuadhimisha Wiki ya
Usuluhishi nchini, Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wamepata fursa
adhimu ya kupatiwa elimu muhimu ya usuluhishi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za
kuwaandaa vijana kuwa mabalozi wa amani na utatuzi wa migogoro katika jamii.
Elimu
hiyo imetolewa jana tarehe 16 Aprili, 2026 katika moja ya kumbi za mikutano
zilizopo ndani ya Chuo hicho, ambapo Wanafunzi walijitokeza kwa wingi kushiriki
na kujifunza kwa kina kuhusu mbinu mbadala za utatuzi wa migogoro, nje ya mfumo
wa kawaida wa Mahakama.
Watoa
mada katika mafunzo hayo walikuwa ni Wadau mbalimbali wa sekta ya sheria,
wakiwemo Mahakimu, Mawakili wa Serikali pamoja na Mawakili wa Kujitegemea. Wadau
hao waliotoa uzoefu wao wa vitendo na kusisitiza umuhimu wa usuluhishi katika
kuharakisha haki, kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani na kudumisha
mahusiano mema katika jamii.
Mafunzo
hayo yalisimamiwa na Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, ambaye pia ni
Mratibu wa Wiki ya Usuluhishi, Mhe. Dkt. Fatma Khalfan. Kupitia usimamizi wake, zoezi hilo
lilifanikiwa kwa kiwango cha juu, likiwaacha Wanafunzi na uelewa mpana pamoja
na hamasa ya kujifunza zaidi kuhusu taaluma ya sheria na mbinu za kisasa za
utatuzi wa migogoro.
Akizungumza
wakati wa mafunzo hayo, Mhe. Dkt Fatma alisisitiza kuwa kuwafikia Wanafunzi ni uwekezaji
muhimu kwa mustakabali wa Taifa, kwani wao ndio watakaobeba dhamana ya
kusimamia haki na amani katika jamii siku zijazo.
Kwa
upande wao, Wanafunzi walionesha mwamko mkubwa na shauku ya kujifunza,
wakieleza kuwa elimu hiyo imewafungua macho na kuwapa mtazamo mpya juu ya namna
bora ya kushughulikia migogoro bila migongano mikali.
Maadhimisho
ya Wiki ya Usuluhishi yanaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini,
yakilenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kutumia njia mbadala za
utatuzi wa migogoro, badala ya kutegemea Mahakama pekee.
Kwa ujumla, utoaji wa elimu hiyo kwa Wanafunzi wa UDOM, ambao wanachukua taaluma ya sheria ni hatua muhimu katika kujenga kizazi chenye uelewa, busara na uwezo wa kuleta suluhu za kudumu katika jamii, ikiwa ni msingi imara wa amani na maendeleo ya Taifa.
Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, ambaye pia ni Mratibu wa Wiki ya Usuluhishi, Mhe. Dkt.Fatma Khalfan, akiwa katika Ukumbi Chuo cha Udom pamoja na Wanafunzi wakisikiliza neno la ukaribisho kutoka kwa Mkufunzi, Dkt Gamba (hayupo pichani)).
Wanafunzi
wa Sheria Chuoni cha UDOM wakisikiliza kwa makini elimu ya usuluhishi kutoka
kwa watoa mada.
Jaji
wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, ambaye pia ni Mratibu wa Usuluhishi, Mhe.
Dkt. Fatma Khalfan, akifafanua jambo wakati wa utoaji elimu ya usluhishi kwa Wanafunzi
wanaosomea sheria UDOM.
Wakili
wa Kujitegemea, B. Elias Macibya, akifafanua jambo kuhusu usuluhishi wakati wa
mafunzo hayo.
Jaji
wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dodoma, ambaye pia ni Mratibu wa Usuluhishi, Mhe.
Dkt. Fatma Khalfan (aliyevaa mtandio wa blue) akiwa katika picha ya pamoja na
watoa mada pamoja na baadhi ya Wanafunzi mara baada ya mafunzo hayo.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni